Matumaini mapya vivuko vya Kigamboni wanafunzi wakiombewa kuvushwa bure

Dar es Salaam. Wakati kesho shule za msingi na sekondari nchini zikifunguliwa, Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (Temesa), imeomba msaada wanafunzi kuvushwa bure kwenye vivuko vya Kampuni ya Azam vinavyovusha watu kati ya Kivukoni na Kigamboni baada ya kile chao cha ‘Mv Kazi’ kuharibika.

Temesa pia imeeleza kuwa, Kivuko cha Mv Magogoni kilichokuwa kwenye matengenezo tangu mwaka 2022 kinatarajiwa kuwasili nchini Aprili, 2026 tayari kwa kutoa huduma.

Hayo yamesemwa leo Jumatatu Aprili 12 na Kaimu Mtendaji Mkuu wa Temesa, Moses Mabamba alipozungumza na waandishi wa habari kuhusu hatua walizochukua baada ya kuharibika kwa kivuko hicho  pekee cha ‘Mv Kazi’ ambacho ndio kilikuwa kikifanya.

“Kivuko hiki kiliharibika tangu Januari 6, 2026, tuliamua kukitengeneza na  kuongeza injini nyingine mbili ukiacha mbili zilizokuwa mwanzoni.

Kivuko cha ‘Mv Kazi’ kikiwa kimeegeshwa Kivukoni baada ya kusimama kwa siku sita bila kufanya kazi

Pia tulifanya marekebisho katika mifumo yote ya umeme na kiuendeshaji ili kiweze kufanya kazi wakati wote badala ya kilivyokuwa kikifanya kazi na kusimama,” amesema Mabamba.

Hata hivyo, amesema baada ya kukamilika kwa marekebisho hayo  kesho wanatarajia kukifanyia majaribio baharini kabla ya kuanza kubeba abiria na ni takwa la kisheria na usimamizi wa vyombo vya majini.

Kutokana na hilo, mtendaji huyo amesema  wamewaombea wanafunzi waliokuwa wakivushwa bure na kivuko hicho, kubebwa na vivuko vya Azam.

“Nadhani wote mnajua kuwa kesho shule zinafunguliwa na kwa kuwa kivuko chetu hakijatengemaa tumeomba wenzetu Azam watusaidie kuwabeba wanafunzi ambao katika vivuko vyetu siku zote huvushwa bure bila kuwatiza hela yoyote.

“Katika hili kikubwa mwanafunzi awe katika sare za shule au awe na kitambulisho na katika upandaji watakuwa na foleni yao,” amesema Mabamba.

Aidha amesema majarabio hayo yanatarajiwa kufanyika asubuhi na mpaka kufika saa nane mchana kitakuwa tayari kwa kuanza kufanya kazi ya kubeba abiria.

Pia ametumia nafasi hiyo kuwaomba radhi wananchi waliopata usumbufu katika siku zote hizo, kivuko kilipokuwa kwenye matengenezo.

Kivuko cha Mv kazi kina uwezo wa kubeba abiria 200 na magari 20 kwa wakati mmoja huku ukarabati wake ikielezwa  umetumia siku nne na kugharimu Sh30 milioni.

Akizungumzia kuhusu kivuko kikubwa kuliko vyote cha Mv Magogoni ambacho kilikuwa katika matengenezo nchini Kenya tangu Februari 2022, Mabamba amesema kinatarajiwa kuwasili nchini Aprili,2026.

“Mpaka ninavyozungumza sasa kivuko hicho matengenezo yake yamefikia asilimia 81.3, hivyo ni matarajio yetu hadi kufika Aprili mwaka huu kitakuwa kimewasili nchini tayari kwa kuanza kutoa huduma.”

Kivuko cha Mv Kigamboni kina uwezo wa kubeba abiria 2000 na magari 60 kwa wakati mmoja.

Abiria wakiwa wanashuko katika vivuko ambavyo kesho vitatumika kuwabeba wanafunzi bure

Wakati   kivuko cha Mv Kigamboni amesema nacho ifikapo Oktoba 2026,kitakuwa kimerejea kutoka kwenye matengenezo makubwa na hapo ndio kivuko cha Mv Kazi nacho tutakipeleka kwenye matengenezo kama hayo.

Alipoulizwa kama kuna mpango wowote wa kuleta kivuko kipya ukiacha hivyo vilivyopo, Mabamba amesema hakuna mpango huo kwa kuwa wanaamini vivuko vyote vikiwa vizima vina uwezo wa kuwahudumia wananchi bila shida.

Wakitoa maoni yao kwa nyakati tofauti wananchi wanaotumia vivuko hivyo akiwamo Juliana Didas, amesema taarifa hizo ni njema kwao ukizingatia baadhi walikuwa hawana uwezo wa kulipia Sh500.

“Kawaida vivuko hivi vya Serikali tunalipa Sh200,hivyo kuna watu bajeti yao ni Sh400 kuvuka kila siku, hivyo kurudi kwa kivuko cha Serikali ni jambo la kushukuru “amesema Juliana.

Job Masinyilo, amesema kivuko cha Mv kazi ubovu wake umekuwa mara kwa mara jambo lililokuwa likiwapa wasiwasi watu wanaokipanda.

Hata hivyo, ameshauri kuongezwa kwa kivuko hicho, walau viwe vinapishana kwa kuwa ilikuwa ikiwalazimu kusubiri hadi nusu saa kivuko kifike kutoka upande wa pili.