:::::::::
Dar es Salaam
Serikali imetangaza kuwa kivuko cha MV Kazi kitaanza rasmi kutoa huduma kesho baada ya kukamilika kwa ukarabati wake, hatua inayolenga kurejesha usafiri wa uhakika kwa wananchi wanaotumia feri ya Kigamboni na Kivukoni.
Akizungumza leo jijini Dar es Salaam, Kaimu Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA), Mosses Mabamba, amesema ukarabati wa kivuko hicho umekamilika kwa mafanikio.
Amesema kazi zilizofanyika ni pamoja na kubadilisha injini na mifumo ya umeme, ukarabati uliodumu kwa siku nne na kugharimu shilingi milioni 30.
Mabamba ameeleza kuwa majaribio ya mwisho yatafanyika kesho asubuhi na endapo yatakamilika bila changamoto, kivuko hicho kitaanza kutoa huduma kuanzia saa nane mchana.
Kwa mujibu wa TEMESA, kivuko cha MV Kazi kina uwezo wa kubeba abiria 200 kwa safari moja, hali itakayosaidia kupunguza msongamano na kurejesha hali ya kawaida ya usafiri katika eneo hilo.
Wananchi wanaotegemea kivuko hicho wameeleza kufurahishwa na kurejea kwa huduma hiyo, wakisema itarahisisha shughuli zao za kila siku ikiwemo kwenda kazini, shuleni na kufanya biashara.
Hata hivyo, wananchi hao wameiomba Serikali kuendelea kuboresha na kuimarisha huduma za vivuko ili kuepuka adha zinazojirudia mara kwa mara.
Wakati huo huo, Serikali imesema inaendelea kutekeleza mpango wa muda mrefu wa kuboresha usafiri wa majini, ikiwemo ukarabati wa kivuko cha MV Magogoni.
Kivuko hicho kinatarajiwa kuanza kutoa huduma mwezi Aprili na kitakuwa na uwezo wa kubeba abiria 2,000 na magari 60 kwa safari moja.








