LIGI Kuu ya Wanawake (WPL) na leo tena

LIGI Kuu ya Wanawake (WPL) inaendelea leo kwa mechi nne ngumu zitakazopigwa kwenye viwanja tofauti ikiwa ni raundi ya nane.

Hadi sasa Simba Queens inaongoza msimamo wa ligi hiyo kwenye mechi saba ikiwa na pointi 19, Yanga Princess nafasi ya pili na pointi 18, mabingwa watetezi nafasi ya tatu na pointi 17 huku Fountain Gate Princess ikiwa nafasi ya nne na pointi 13.

Miongoni mwa mechi zinazosubiriwa kwa hamu ni ile itakayozikutanisha JKT v Ruangwa Queens iliyopo nafasi ya 11 kwenye msimamo mechi itakayopigwa Uwanja wa Majaliwa, huku timu zote zikihitaji pointi tatu kwa malengo tofauti katika msimamo wa ligi.

WP 01

JKT chini ya kocha Kessy Abdallah itaingia kwenye mchezo huo ikilenga kupata ushindi na kurejea kileleni mwa msimamo baada ya sare mbili ilizopata na kudondosha pointi nne.

Kocha huyo amesema wamejipanga kuhakikisha wanatumia vyema faida ya kucheza nyumbani na kurekebisha makosa yaliyojitokeza katika michezo iliyopita.

Ruangwa Queens kwa upande wao wanahitaji pointi hizo ili kujinasua kwenye nafasi za chini za msimamo wa ligi, jambo linalofanya mechi hiyo kuwa ngumu na ya ushindani mkubwa.

WP 02

Katika Uwanja wa Nyamagana, Alliance Girls watawakaribisha Bilo Queens katika mchezo unaotarajiwa kuwa wa kasi. Alliance Girls wameonyesha uimara mkubwa wanapocheza nyumbani msimu huu, hali inayowapa matumaini ya kupata ushindi mwingine mbele ya mashabiki wao.

Bilo Queens itaingia ikiwa na dhamira ya kuvunja rekodi hiyo, wakijua kupoteza pointi ugenini kunaweza kuwaumiza katika mbio za kusaka nafasi bora kwenye msimamo wa ligi.

Mchezo mwingine utapigwa Uwanja wa Tanzanite Kwaraa na Fountain Gate Princess wataikabili Yanga Princess. Huu ni mmoja wa michezo mikubwa ya raundi hiyo kutokana na historia na ubora wa vikosi vya timu hizo.

WP 03

Kocha wa Yanga Princess, Edna Lema amesema maandalizi yamekuwa mazuri na wachezaji wake wako tayari kupambana kwa nguvu zote.

“Tunajua Fountain Gate ni timu ngumu, lakini tumejipanga kucheza kwa nidhamu na kupambana hadi dakika ya mwisho kupata pointi,” amesema Edna.

Uwanja wa Samora, Ceasiaa Queens watakuwa nyumbani dhidi ya Mashujaa Queens. Ceasiaa wanahitaji ushindi huo ili kuimarisha nafasi yao kwenye msimamo ikiwa mkiani na pointi moja pekee.