KIKOSI cha Simba kinaendelea na kambi ya mazoezi kujiandaa na mechi mbili za kimataifa dhidi ya Esperance ya Tunisia zitakazopigwa mwisho mwa mwezi huu, lakini kuna nyota wa zamani wa timu hiyo ameamua kuvunja ukimya na kutoa ushauri ambao wanasimba wakiufanyia kazi huenda ukawabeba.
Nyota huyo wa zamani ni Amir Maftah aliyewahi kuwika na timu hiyo baada ya kuitumikia Yanga, amesema kitu kinachoweza kuirejesha klabu Msimbazi katika ushindani na hata kurejesha mataji klabuni hapo ni kupata viongozi vijana watakaoendana na kasi ya dunia.
Maftah aliitolea mfano Yanga kwa kusema imekuwa tishio ndani na nje ya nchi kutokana na kuongozwa na viongozi vijana wenye maono na mipango inayoendana na kasi ya soka la kisasa lililopo duniani.
Amesema Yanga inayoongozwa Hersi Said anayeonekana katika mechi mbalimbali za kimataifa, kitaifa na kwenda kufanya skauti ya wachezaji wa viwango vya juu, wanaoisaidia klabu hiyo kucheza kwa kiwango, lakini hata wanavyoiendesha klabu ni tofauti na ilivyokuwa miaka ya nyuma.
“Nianze kwa kusema nawaheshimu sana viongozi waliopo Simba majina yao yamefanya makubwa katika nchi hii mfano Crescentius Magori, Azim Dewji, Mohammed ‘Mo’ Dewji na wengineo, lakini maisha yanakwenda kasi yana mabadiliko makubwa mno,” amesema Maftah na kuongeza:
“Panda shuka za Simba zinahitaji viongozi vijana ambao watakuwa na kasi ya kufanya vitu kwa kasi ya dunia ya sasa na hata kuhudhuria matukio mbalimbali ya kimataifa, ambako kuna kitu watakwenda kukiongeza kwa manufaa ya klabu na ligi kwa ujumla.”
Nyota huyo aliyewahi pia kuitumikia Mtibwa Sugar, amesema ni wakati wa uongozi wa Simba kukaa chini na kuwatafuta vijana wenye uwezo mkubwa wa kuendana na kasi ya kuongoza klabu, alisisitiza anaona ndiyo njia pekee ya kurejesha heshima, vinginevyo haoni kama hata msimu huu wanaweza wakafanya makubwa kama utulivu ukikosekana.
“Mpira unaonekana wazi hata wakisajili wachezaji na kuwaleta makocha kisha wakawaacha haitasaidia, bora wakubaliane na ukweli mchungu ambao baadaye utawapa kicheko na kulinda heshima zao, kama hawaamini vijana basi wenyewe wabadilike na kwenda na kasi ya soka la kisasa,” amesema Maftah.
