KUNA vita nyingi zinakwenda kushuhudiwa leo Jumanne katika fainali ya Kombe la Mapinduzi 2026 kwenye Dimba la Gombani kisiwani Pemba na Azam itacheza dhidi ya Yanga.
Hii ni fainali ya kwanza katika Kombe la Mapinduzi inazikutanisha Azam na Yanga tangu 2007 ilipoanza michuano hiyo rasmi kwa kushirikisha timu kutoka nje ya Zanzibar.
Licha ya kwamba timu hizo sio mara ya kwanza kucheza fainali ya michuano hii na kubeba ubingwa kila moja, lakini safari hii kuna ladha tofauti tunakwenda kuishuhudia zinapokutana.
Tayari zimechezwa fainali kadhaa za Mapinduzi zikihusisha timu kutoka Bara. Azam imewahi kucheza dhidi ya Simba pekee, huku Yanga ikicheza dhidi ya Mtibwa na Simba.
Majira ya saa 1:00 usiku, kipute kitaanza kupigwa kwenye Uwanja wa Gombani kumsaka bingwa mpya wa Kombe la Mapinduzi.
Mbinu za makocha wa timu zote mbili, Florent Ibenge wa Azam na Pedro Goncalves wa Yanga, zinatarajiwa kutoa mechi nzuri leo kutokana na kile tulichoshuhudia kuanzia makundi hadi nusu fainali.
Mara moja pekee tumeshuhudia Azam ikitanguliwa kufungwa bao, lakini ikajipanga vizuri na kusawazisha kisha kupata ushindi.
Mbali na hilo, mara moja Azam imeongoza lakini mpinzani akasawazisha na matokeo kuwa sare. Kwa Yanga, haijawahi kutanguliwa wala kuruhusu bao.
Hii yote inatokana na mbinu bora za makocha hao wakitumia zaidi viungo wa kati kuiweka timu kuwa imara muda wote wa mechi.
Yanga ilikuwa inamtegemea Mohamed Damaro na Duke Abuya eneo la kiungo wa kati wakicheza chini, kisha Maxi Nzengeli akiibia kule juu. Pia wakati mwingine Damaro na Abuya wanapishana kwenda juu.
Mechi ya leo, Damaro anakosekana kutokana na kadi nyekundu aliyoonyeshwa mechi ya nusu fainali dhidi ya Singida Black Stars, hivyo kuna uwezekano Mudathir Yahya akaanza kutokana na kupona majeraha.
Azam mechi tatu zilizopita ilimkosa Sadio Kanoute aliyekuwa majeruhi, lakini mazoezi ya mwisho ameonekana akifanya pamoja na timu ikiashiria kupona na huenda akawepo leo.
Hata hivyo, wakati yeye hayupo, nahodha Himid Mao na James Akaminko walikichafua sana pale kati na wanaweza kuendelea kukichafua kwani ushirikiano wao umelipa kwa kuivusha timu hadi fainali.
Dimba la kati anapokuwepo Abuya ambaye amekabidhiwa kitambaa cha unahodha katika michuano hii, huku Mudathir na Maxi wakiimarisha Yanga, kule Azam Akaminko na Himid, lazima pachimbike.
Katika kushambulia, makocha wote wanatumia pembeni, lakini kila mmoja amechagua upande wake.
Azam inatumia zaidi upande wa kulia anapocheza Nathaniel Chilambo na Cheikna Diakite. Pia Azam ni wazuri katika kutumia mipira ya kutenga kiasi ambacho Kocha Mkuu wa Simba, Steve Barker alikiri hilo kikosi chake kilipopoteza kwa bao 1-0, kupitia shambulizi lililoanzia mpira wa kona.
Yanga upande wake imara wa mashambulizi ni wa kushoto kule anapocheza Pacome Zouzoua na Chadrack Boka.
Pia timu zote zinatumia katikati kujenga mashambulizi na kutawanya pembeni.
Jephte Kitambala wa Azam, ndiye kinara wa mabao aliyebaki katika mashindano haya akiwa nayo mawili. Ndiye mshambuliaji tegemeo wa Azam kuelekea mechi hii ya fainali.
Safu ya ulinzi ya Yanga inapaswa kumchunga kwani amekuwa hatari kwa wapinzani tangu atue msimu huu.
Tayari mshambuliaji huyo ameitungua Simba katika mechi ya ligi alipokutana nayo kwa mara ya kwanza. Pia anakwenda kucheza dhidi ya Yanga kwa mara ya kwanza.
Mbali na Kitambala, kuna Zidane Sereri, anayeunda pacha naye safu ya ushambuliaji ya Azam. Naye amefunga bao moja. Pia aliifunga Simba msimu uliopita, hivyo sio mgeni wa mechi kubwa.
Yanga ina Pacome Zouzoua, amefunga na kutoa asisti, ni mmoja wa wachezaji hatari eneo la kutengengeneza mashambulizi. Azam imchunge sana.
Mwingine ni Maxi Nzengeli. Ana tuzo zake mbili za mchezaji bora, hiyo inaonyesha ni mtu hatari ndani ya uwanja. Amefunga bao moja.
Yote kwa yote, kila upande una kazi ya kufanya kuhakikisha inabeba ubingwa. Azam iliyofunga mabao sita katika mechi nne, ina kazi ya kuipenya ngome ya Yanga ambayo haijaruhusu nyavu zake kutikiswa hadi sasa ikishuka dimbani mara tatu.
Hata hivyo, Azam imekuwa na rekodi ya kufunga bao kila mechi iliyocheza, hivyo timu kesho kazi ipo katika kuendeleza mwendo wao huo dhidi ya timu isiyofungika.
Yanga ina kazi ya kulinda lango lake na kuweka rekodi ya kumaliza bila nyavu zake kutikiswa, huku pia ikihitaji bao kuifanya pia ifunge kila mechi.
Azam inasaka taji la sita baada ya kubeba mwaka 2012, 2013, 2017, 2018 na 2019, inasaka nafasi ya kutanua rekodi yao kwani hivi sasa ndio timu iliyobeba mara nyingi, huku Yanga ikilisaka kwa mara ya tatu ikiifukuzia Simba yenye manne. Tayari Yanga imelichukua mwaka 2007 ikiifunga Mtibwa na 2021 ilipoichapa Simba.
Yanga hii inakuwa fainali ya nne katika historia ya Kombe la Mapinduzi ikifanya hivyo mwaka 2007, 2011, 2021 na sasa 2026. Azam ni fainali ya saba, kati ya sita zilizopita imebeba ubingwa mara tano na kukosa moja mwaka 2022 ilipochapwa na Simba.
Wakato Yanga na Azam hii ikiwa mara ya kwanza zinakutana katika fainali ya Kombe la Mapinduzi, rekodi zinaonyesha mara ya mwisho zilikutana katika fainali ya Kombe la FA iliyochezwa Zanzibar Juni 2, 2024 kwenye Uwanja wa New Amaan Complex. Yanga ilishinda kwa penalti 6-5 baada ya muda wa kawaida matokeo kuwa 0-0. Leo Azam ina nafasi ya kulipa kisasi cha kupoteza dhidi ya Yanga mara ya mwisho zilipocheza Zanzibar.
Kwa upande wa makocha, Pedro Goncalves wa Yanga anasaka taji lake la kwanza tangu atue kikosini hapo, huku pia Florent Ibenge wa Azam naye analitolea macho taji hilo ashinde kwa mara ya kwanza akiwa klabuni hapo.
Azam iliyokuwa kundi A, ilianza safari ya kusaka taji la sita kwa kutoka 1-1 dhidi ya Singida Black Stars, kisha ikaifunga Mlandege 2-0 na kumalizia kuichapa URA 2-1.
Hatua ya nusu fainali, ilikwenda kuichapa Simba bao 1-0, hivyo hadi kumaliza michuano hii, Azam itakuwa imekutana na timu tatu zilizomaliza nne bora ya Ligi Kuu Bara msimu uliopita ambazo ni Singida, Simba na Yanga.
Kwa upande wa Yanga ilikuwa kundi C, imeshinda mechi zote ikianza kuifunga KVZ 3-0, ikaja kuichapa TRA United 1-0, nusu fainali ikaifunga Singida Black Stars 1-0.
Kuna wachezaji kadhaa wanaweza kukosekana baada ya kupata majeraha katika mashindano haya, hali hiyo inaweza kufanya kuziona sura mpya zikaibuka leo ili kuziba mapengo yaliyopo na umuhimu wa mechi yenyewe.
Sadio Kanoute wa Azam anaweza kuwepo au asiwepo, hii itategemea na uimarikaji wake baada ya kupona kutoka kwenye majeraha.
Lassine Kouma na Aziz Andabwile upande wa Yanga wana hatihati kubwa ya kuwepo, waliumia mechi za mwanzoni, huku pia Damaro anayetumikia adhabu ya kadi nyekundu aliyoonyeshwa hatua ya nusu fainali, hayupo.
Damaro alikuwa mchezaji tegemeo eneo la kiungo mkabaji, hivyo kukosekana kwake itamlazimu Kocha wa Yanga, Pedro Goncalves kumpa majukumu mwingine. Iwe Duke Abuya au Mudathir Yahya ambaye amepona hivi karibuni.
Kiungo mkabaji aliyebaki, Mousa Bala Conte amerudishwa kucheza beki wa kati baada ya Andabwile ambaye naye ni kiungo aliyekuwa akicheza beki wa kati kuumia. Hata hivyo, kuna beki mwingine wa kati, Nizar Abubakar Othuman ‘Ninju’ ambaye mechi iliyopita dhidi ya Singida aliishia benchi, akacheza Conte, kabla ya hapo alicheza dhidi ya KVZ na TRA United.
Frank Assinki amebaki kuwa beki wa kati pekee tegemeo, hivyo kunaweza kutokea mabadiliko makubwa eneo hilo leo kutokana na uhaba wa viungo na mabeki wa kati.
Kocha wa Yanga, Pedro Goncalves, amesema: “Kufika fainali ni sehemu ya kuyafikia malengo yetu tuliyojiwekea wakati tunakuja kushiriki mashindano haya. Tunautaka ubingwa lakini pia tupo hapa kuimarisha kikosi kuelekea mechi za CAF ndio maana natoa fursa kwa wachezaji tofauti tuliokuja nao.”
Kocha wa Azam, Florent Ibenge naye amesema: “Niliweka malengo ya kucheza mechi tano katika mashindano haya na hiyo inakwenda kutimia siku ya fainali. Lakini pia malengo ya ubingwa yapo palepale.
“Ubingwa utatupa nafasi nzuri ya kuona wapi tumefanikiwa kwani tunakabiliwa zaidi na mechi ngumu ya CAF ugenini dhidi ya Nairobi United.”
