Maeneo yatakayoamua urais wa Museveni, Bobi Wine

Dar es Salaam. Joto la kisiasa nchini Uganda linazidi kupanda huku maeneo haya  yanatarajiwa kuamua kati ya Rais Yoweri Museveni na Robert Ssentamu, maarufu Bobi Wine nani kuibuka na ushindi kwenye uchaguzi huo utakaofanyika Alhamisi ijayo.

Kampeni za urais zilianza Septemba 29, 2025 huku za wabunge zikianza Novemba 10 na zinahitimishwa leo Jumanne, Januari 13, 2026 ikiwa ni siku mbili kabla ya wananchi wa taifa hilo kuamua nani awe rais au mbunge kwa kipindi cha miaka mitano ijayo.

Wagombea wanane wanachuana kwenye nafasi hiyo ya juu huku ushindani mkubwa ukiwa kati ya Rais Museveni anayetetea nafasi hiyo dhidi ya na Bobi Wine ambaye ni msanii wa muziki.

Tume ya Uchaguzi ya Uganda (EC) imeidhinisha vyama 27 kushiriki uchaguzi mkuu wa ubunge na urais, huku wagombea urais wakiwa wanane, wakiwemo Museveni wa chama tawala cha National Resistance Movement (NRM) na Bobi Wine wa National Unity Platform (NUP).

Rais Museveni, mwenye umri wa miaka 81, anapigania muhula wa saba baada ya kukalia kiti hicho tangu 1986, huku Bobi Wine, kiongozi wa upinzani amepata umaarufu mkubwa, akimtikisa  Rais Museveni kutokana na kuungwa mkono na kizazi kipya kinachotaka mabadiliko.

Kwa mujibu wa Tume hiyo, idadi ya wapiga kura waliyojiandikisha ni milioni 21.68, ikionyesha ongezeko ikilinganishwa na uchaguzi wa mwaka 2021 ambapo waliojiandikisha walikuwa milioni 18.1 pekee. Waliojitokeza kupiga kura walikuwa milioni 10.7.

Takwimu zinaonesha wanawake ni wengi kidogo kuliko wanaume, jambo linaloibua mjadala kuhusu ushawishi wa kura zao, hasa katika maeneo ya mijini na pembezoni mwa miji mikubwa.

Historia na ripoti za vyombo vya habari chini humo vinaonesha ushindi hautaamuliwa nchi nzima pekee, bali kwa mafanikio ya wagombea katika maeneo yenye uzito mkubwa wa kisiasa na idadi ya wapiga kura.

Wachambuzi kutoka nchini humo wanalitaja Jiji la Kampala na wilaya zake zinazozunguka kama kitovu cha uamuzi, ambapo Bobi Wine alipata ushindi mkubwa mwaka 2021 katika awamu yake ya kwanza ya kuwania nafasi ya juu ya uongozi, hali inayothibitisha nguvu ya upinzani mijini.

Aidha, Kampeni zake mijini zinatajwa kuwa zinategemea hasira ya vijana dhidi ya matatizo ya kijamii, ukosefu wa ajira, gharama ya maisha, na madai ya ukandamizaji wa kisiasa, dhidi ya uzoefu na historia ya Museveni anayoitumia kama silaha kurejea kiti hicho.

Mashariki mwa Uganda, Busoga, pia linatajwa kama eneo muhimu lenye wapiga kura wengi wapya. Hata hivyo, wachambuzi nchini humo wanasema eneo hili limekuwa linabadilika kisiasa.

Inaelezwa kwa chaguzi zilizopita chama tawala (NRM) kilikuwa na ushawishi zaidi, lakini sasa upinzani unaongezeka, jambo linalofanya eneo hilo kuwa ngome yenye mchuano mkali.

Magharibi mwa Uganda na maeneo ya vijijini yanatajwa kuwa ngome za Museveni, ambapo chama tawala kimejenga mtandao mpana wa wafuasi, na historia yake ya kuleta utulivu baada ya machafuko ya kisiasa silaha inayosalia kuwa faida kubwa kwake.

Mbali na ngome za kijiografia, ushawishi binafsi wa wagombea unatajwa pia kuwa moja ya eneo muhimu katika kumpata mshindi wa kiti cha urais katika uchaguzi huo.

Museveni anajieleza kama kiongozi mwenye uzoefu na dhamana ya amani, akisisitiza mafanikio yake katika miundombinu, kilimo na usalama, huku akionya kuwa mabadiliko ya ghafla yanaweza kuhatarisha maendeleo.

Bobi Wine, mwenye takribani miaka 40, anajenga umaarufu wake kama alama ya mabadiliko, akitegemea zaidi kura za vijana na wapiga kura wa mijini wanaotaka mageuzi ya uongozi.

Katika uchaguzi wa 2021, uliompa Museven ushindi, Bobi Wine alipata takribani kura milioni 3.47 sawa na asilimia 34.8 dhidi ya Mseven aliyepata kura milioni 5.85 sawa na asilimia 58.6, jambo lililompa hamasa kuamini anaweza kumtikisa Rais Museveni licha ya malalamiko ya ukiukaji wa haki za kisiasa ya mara kwa mara.

Mbali na kupata kura hizo ambazo zimekuwa mtaji kwenye siasa zake na kujizoelea umaarufu ndani na nje ya Uganda, chama chake kilipata wabunge 57 kati ya 529.

Chama tawala cha NRM kilikuwa na wabunge 336, chama cha FDC wabunge 32. Vingine na wabunge kwenye mabano ni FDC (9), UPC (9), JEMA na PPP vikiambulia mbunge mmoja mmoja.

Kutokana na hali hiyo, kampeni zake zinazojikita kupambana na ufisadi, ukosefu wa ajira, na ukandamizaji zinatajwa kuwa zimekuwa silaha yake inayoendelea kuvutia wapiga kura wanaotamani mabadiliko ya mfumo.

Ezekiel Kamwaga, mchambuzi na mfuatiliaji wa siasa za kikanda kutoka Tanzania, anasema kwa siasa za Uganda na mwenendo wa uchaguzi haoni kama Bobi Wine anaweza kumwangusha Museven kwa sasa, akisema bado jamii hasa maeneo ya pembezoni mwa miji mikubwa ya Uganda wanaonekana kusalia na imani kwa Rais Museven.

“Pamoja na nguvu ya Bobi Wine, bado Museven anayo nafasi ya kuibuka kidedea kwenye uchaguzi huu kwani ana nguvu ya kimfumo na bado waganda wengi wanaonekana kuamini kuwa uzoefu wake unaotokana na ukongwe kwenye kiti hicho anaweza kuendeleza Taifa hilo,” anasema Ezekiel Kamwaga.

Profesa Sabiiti Makara, mchambuzi wa siasa wa nchini Uganda anaonesha hofu juu ya wapiga kura kunyimwa haki pia anagusia uelewa mdogo wa jamii katika masuala ya kisiasa kuwa kunaathiri mwenendo wa uchaguzi nchini humo.

“Kuna umuhimu wa wapiga kura kujua haki zao, kuchagua kwa kufahamu, na kuzuia vurugu katika kampeni.  Uelewa wa namna bunge linavyofanya kazi unapaswa kuongezeka ili kupunguza kukosa ufahamu kuhusu mchakato wa upigaji kura,” anasema.

Benjamin Katana, mwanaharakati wa upinzani wa chama cha (NUP) anasema kuna wasiwasi juu ya utendakazi wa Tume ya Uchaguzi, na chama cha NUP kinaangalia taratibu za kuhakikisha uchaguzi unaendeshwa kwa uwazi na kwa mujibu wa sheria.

Ofisi ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa (UN) kupitia taarifa yake imeonesha hofu ya kukosekana kwa mazingira ya uchaguzi huru na wa haki ikidokeza kuonewa kwa upinzani katika uchaguzi huu.

“Uchaguzi unafanyika katika mazingira ambapo kuna ukandamizaji mkubwa dhidi ya wapinzani, wanaharakati, waandishi wa habari na waendesha kampeni za upinzani, jambo linalofanya mchakato wa uchaguzi kuwa wa shaka,” inaeleza ripoti ya UN.

Katika uchaguzi wa Uganda, mgombea wa urais anapaswa kupata zaidi ya asilimia 50 ya kura ili kushinda moja kwa moja, vinginevyo duru ya pili inaandaliwa. Wapiga kura pia watachagua wabunge 353 wawakilishi wa majimbo, huku viti maalumu vinavyotengwa kwa wanawake, vijana, wenye ulemavu na makundi mengine.

Hata hivyo, Museveni amekuwa madarakani tangu 1986, akishinda muhula sita mfululizo licha ya malalamiko ya kuzuia upinzani na kudhoofisha ushindani wa kidemokrasia kutoka upande huo.

Kadri siku za uchaguzi zinavyosogea, balozi za mataifa ya nje wakiwemo wa Marekani, wametoa tahadhari kwa raia wao waliopo Uganda kuhusu uwezekano wa machafuko ya kisiasa na hatua kali za kiusalama kabla na baada ya uchaguzi.

 Tahadhari hizi zinajengwa juu ya historia ya chaguzi zilizopita nchini humo ambapo vyombo vya usalama vililalamikiwa kutumia nguvu kupita kiasi dhidi ya waandamanaji na wafuasi wa upinzani, huku Serikali ikisisitiza hatua zote ni za kulinda amani na usalama wa taifa.

Aidha, hali ya siasa na chaguzi katika ukanda wa Afrika kwa siku za hivi karibuni ambapo mataifa kadhaa yameshuhudia msuguano mkali na mizozo ya kisiasa na mapinduzi ya kijeshi kwa baadhi ya maeneo, inatajwa pia kuongeza hofu hiyo ya kiusalama kuelekea uchaguzi huo.