Kesi ‘vigogo wa Kigamboni’ wanaodai kuchepusha fedha za Tamisemi, kuunguruma leo

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imepanga leo Jumanne, Januari 13, 2026 kuanza kusikiliza ushahidi wa upande wa Jamhuri katika kesi ya kuchepusha fedha na kuisababishia Wizara ya Tamisemi hasara ya Sh165 milioni, inayowakabili washtakiwa 13, wakiwemo wakuu wa Idara wa Manispaa ya Kigamboni.

Hatua hiyo inatokana na upelelezi wa kesi hiyo kukamilika na washtakiwa kusomewa maelezo ya mashahidi na vielelezo.

Pia, Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) amewasilisha kibali cha kuruhusu kesi hiyo kusikilizwa kwenye mahakamani hapo.

Washtakiwa katika kesi hiyo ya uhujumu uchumi namba 21510 ya mwaka 2025 ni aliyekuwa mkuu wa idara ya fedha na mhasibu wa Manispaa ya Kigamboni, Jonathan Manguli(38).

Wengine ni aliyekuwa mhasibu wa manispaa hiyo Godfrey Martiny (44); Aliyekuwa mkuu wa kitengo cha udhibiti taka na usafi wa mazingira wa manispaa hiyo, Juvenalis Mauna(53); Josephat Mutembei( 39)na ofisa ugavi msaidizi wa manispaa hiyo, Bibiana Mdete(53).

Pia yupo, aliyekuwa ofisa ugavi, Henry Rugayi (38); mhasibu, Annie Maugo (43); ofisa hesabu kutoka Tamisemi Dodom,a Tumsifu Christopher (46) na ofisa hesabu, Aidan Mpozi (61) wote kutoka Manispaa ya Kigamboni.

Wengine ni wafanyabiashara Hamis Manfred (40), Paulo Mwakyusa (43), Godwin Cheyo (33) na Jennifer Manguli (30).

Washtakiwa hao wanakabiliwa na mashtaka 10 yakiwemo, kutakatisha fedha na kuongoza genge na kufanya ubadhilifu, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Tarehe hiyo imepangwa na Hakimu Mkazi Mkuu, Hassan Makube, anayesikiliza kesi hiyo.

Tayari washtakiwa hao wameshapewa nyaraka muhimu ikiwemo maelezo ya mashahidi na vielelezo kabla ya kesi hiyo kuanza usikilizwaji.

Kati ya mashtaka hayo 10; matatu ni ya kutumia nyaraka kwa lengo la kupotosha mwajiri wao; mawili ni ya kuongoza genge la uhalifu; mawili ni ya ubadhilifu wa fedha; moja ni kuchepusha fedha, kutakatisha fedha na kuisababishia hasara Tamisemi.

Katika kesi ya msingi, Washtakiwa wanakabiliwa na shtaka la kuongoza genge la  uhalifu linalowakabili washtakiwa wanane kati yao, ambapo wanadaiwa kati ya Julai Mosi, 2022 na Desemba 30, 2023 maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam na Dodoma, wakiwa watumishi wa umma  kwa kuvunja sheria na kushindwa kutimiza majukumu yao walifanya ubadhilifu wa fedha kiasi cha Sh165 milioni.

Shtaka la pili ni kuongoza genge la uhalifu linalowakabili wafanyabiashara wanne ambao ni Manifred, Mwankyusa, Cheyo na Manguli ambao wanadaiwa kati ya Julai Mosi, 2022 na Desemba 30, 2023 ndani ya Jiji la Dar es Salaam, washtakiwa wakiwa sio watumishi wa umma na kwa kushirikiana na watumishi wa Umma, kwa makusudi waliongoza genge ka uhalifu kwa kufanya ubadhilifu wa fedha kiasi cha Sh165 milioni.

Shtaka la tatu ni kuchepusha fedha linalowakabili  mshtakiwa Maugo, Kachira na Mpozi, ambapo wanadaiwa kati ya Julai Mosi, 2022 na Septemba 5, 2023 katika ofisi za Tamisemi Dodoma, wakiwa wahasibu , kwa masilahi yao binafsi walichapisha na kuhamisha fedha kiasi cha Sh169 milioni, ambazo zilitakiwa zitumike kwa ajili ya miradi mbalimbali ya Tamisemi.

Iliendelea kudaiwa mahakamani hapo kuwa mshtakiwa huyo anadaiwa shtaka la nne ni ubadhilifu wa fedha linalomkabili mshtakiwa Manguli, Martiny na Mauna, ambapo wanadaiwa kati ya Septemba 5, 2022 na Desemba 30, 2023 katika ofisi za Manispaa ya Kigamboni wakiwa watumishi wa Manispaa hiyo, kwa nyadhifa zao za Uhasibu, Mkuu wa Idara ya Fedha na Mkuu wa Idara ya Udhibiti Taka na usafi wa Mazingira, walibadilisha matumizi ya Sh128 milioni kwa masilahi yao binafsi, fedha ambazo ziliwafikia mikononi mwao  kama wahasibu.

Pia, kati ya Septemba 5, 2022 na Desemba 30, 2023 katika ofisi za Manispaa ya Kigamboni, wakiwa wahasibu walifanya ubadhilifu kwa kubadilisha fedha kiasi cha Sh36.8 milioni, fedha ambayo iliwafikia mikononi mwao kama wahasibu.

Shtaka la sita ni matumizi ya nyaraka kwa nia ya kumposha mwajiri wao ambaye ni Manispaa ya Kigamboni inayomkabili Manguli na Mutembei, ambapo wanadaiwa Februari 2, 2023 katika ofisi za manispaa hiyo, kwa nafasi zao za  mhasibu na mhandisi na kwa nia ovu na kwa makusudi walimdanganya mwajiri wao kwa kutumia nyaraka iliyokuwa na taarifa zisizosahihi za taarifa ya ukaguzi wa vifaa, kuonyesha mkandarasi ameshusha tripu 220 za morum na kukodi greda kutoka kampuni ya Konya Investment Co Ltd na , jambo ambalo walijua wanampotosha mwajiri wao.

Shtaka la saba ni matumizi ya nyaraka kwa nia ya kumposha mwajiri, linalomkabili Mdete, ambapo Februari 2, 2023 katika ofisi za Manispaa ya Kigamboni, mshtakiwa akiwa ofisa ugavi msaidizi, kwa nia ovu dhidi ya mwajiri wake, alitumia nyaraka.

Iliyokuwa na taarifa potofu ya vifaa kuonyesha mkandarasi ameshusha tripu 220 za morum na kukodi greda kutoka kampuni ya Konya Investment Co Ltd na kukodi greda, wakati wakijua kuwa wanampotosha mwajiri wao.

Vilevile, mshtakiwa Rugayi anadaiwa Machi 27, 2023 katika ofisi za Manispaa hiyo, mshtakiwa akiwa ofisa ugavi aliwasilisha nyaraka ya iliyokuwa na taarifa potofu ya vifaa, akionyesha kampuni ya Mbogholo Investment imepeleka tripu ya moramu kwenye  lori moja la futi 12 na kukodi greda, wakati akijua anampotosha mwajiri wake.

Shtaka la tisa ni kutakatisha fedha linalowakabili washtakiwa 12, isipokuwa mshtakiwa wa tano( Mdete) ambapo kati ya Julai Mosi, 2022 na Desemba 30, 2025 katika Jiji la Dar es Salaam na Dodoma, washtakiwa walijihusisha na muamala wa fedha kiasi cha Sh165milioni, wakati wakijua fedha hizo ni mazalia ya kosa tangulizi la uchepushaji fedha.

Pia, washtakiwa wote wanadaiwa katika kipindi hicho, kwa pamoja na huku wakifahamu na kwa nia ovu waliisababishia hasara Tamisemi ya Sh165 milioni.

Hata hivyo, mshtakiwa Mdete yupo nje kwa dhamana baada ya kutimiza masharti ya dhamana na pia hana shtaka la kutakatisha fedha.

Kwa mara ya kwanza, washtakiwa hao walifikishwa mahakamani hapo, Septemba 3, 2025 na kusomewa kesi ya uhujumu uchumi namba 21510 wa mwaka 2025.