Kigoma. Kesi ya kupinga matokeo ya uchaguzi wa mbunge jimbo la Kigoma bado ngoma nzito, ndio maneno unaweza kuyatumia kuelezea uamuzi wa Mahakama, kukataa ombi la kusimamisha usikilizaji wa shauri hilo kwa muda usio na kikomo.
Shauri hilo la uchaguzi, limefunguliwa na wapiga kura wanne wa jimbo hilo, Johary Kabourou, Loum Mwitu, Pendo Kombolela na Luma Akilimali dhidi ya Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo hilo na Mbunge wa Jimbo hilo, Clayton Chipando, maarufu BabaLevo.
Lakini, katika shauri hilo namba 28949 la 2025, ambalo wapiga kura hao wanaomba matokeo yaliyompa ushindi Baba Levo yabatilishwe na uitishwe uchaguzi mdogo, wamemuunganisha Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG).
Ombi la kuomba shauri hilo usimame kwa muda usio na ukomo kusubiri uamuzi wa rufaa iliyopelekwa Mahakama ya Rufani, liliwasilishwa na mdaiwa wa kwanza ambaye ni Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Kigoma mjini na AG.
Hata hivyo, baada ya kusikiliza hoja za pande mbili, Jaji Victoria Nongwa wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Kigoma, alilikataa ombi hilo na kusema shauri litaendelea kwa hatua ya usikilizwaji wa awali kama ilivyokuwa imepangwa.
Uamuzi huo umetolewa Januari 9, 2026 na nakala ya uamuzi huo kupatikana Januari 12, 2025 katika tovuti ya TanzLII ambayo ni tovuti ya Serikali ya Tanzania inayochapisha maamuzi, sheria na kanuni bure mtandaoni.
Jaji Nongwa alisema baada ya kukamilika kwa taratibu za awali, shauri hilo lilipangwa kusikilizwa hoja za awali Januari 9, 2025 ambapo mawakili wa mlalamikiwa wa kwanza na wa tatu wakaibua hoja ya kuahirisha shauri.
Mlalamikiwa wa kwanza na wa tatu waliwakilishwa na mawakili wa Serikali, Mark Mulwambo, Lesi Majalala, George Kalenda na Erick Rumisha, wakati mlalamikiwa wa pili, Baba Levo akiwakilishwa na wakili Daniel Lumenyela na Emmanuel Msasa. Walalamikaji katika shauri hilo la uchaguzi waliwakilishwa na wakili John Seka.
Kwa nini walitaka kesi isimame
Wakili Mulwambo aliiarifu mahakama wamewasilisha taarifa ya rufaa Mahakama ya Rufani ambayo ilitolewa na mlalamikiwa wa kwanza na tatu Desemba 23, 2025 ikiambatana na ombi la kupatiwa nyaraka zote muhimu.
Kutokana na hatua hiyo, wakili alisema shauri lililopo mbele ya mahakama hiyo haliwezi kuendelea siku ya leo, hadi pale rufaa waliyokata Mahakama ya Rufani kupinga uamuzi mdogo wa mahakama itakaposikilizwa na kutolewa uamuzi.
Rufaa hiyo ni kupinga uamuzi mdogo wa kukataa pingamizi la awali walalamikiwa la kutaka shauri hilo lifutwe wakidai halijakidhi vigezo vya kisheria na halina sifa. Wakili huyo aliongeza kusema rufaa yenyewe bado haijawasilishwa mahakamani na muda bado wanao na kueleza kitendo cha kuwasilisha taarifa ya rufaa kinaanzisha rufaa, na taarifa hiyo inatosha kusimamisha shauri hilo.
Alirejea uamuzi wa kesi mbalimbali kuwa taarifa ya kukata rufaa inapowasilishwa mahakamani, mahakama inatakiwa kusimamisha usikilizwaji wake mara moja hivyo mahakama ya chini haipaswi kuendelea kusikiliza shauri hilo.
Wakili Lumenyela anayemwakilisha mlalamikiwa wa pili (Baba Levo) aliungana na wasilisho la wakili wa Serikali na aliongezea uamuzi wa mahakama ya rufani.
Walalamikaji walivyojibu mapigo
Akijibu hizo, wakili Seka anayewawakilisha walalamikaji alisema maombi yaliyoletwa yanakatazwa na sheria ya Mamlaka ya Rufani, kifungu cha 5(2)(d).
Alisema kifungu kinatamka kwamba hakuna rufaa, au maombi ya marejeo ambayo yatafanywa au yanaweza kufanywa kwenda Mahakama ya Rufani endapo maombi hayo au rufaa hiyo inahusiana na jambo ambalo halimalizi shauri.
Alieleza jambo lililokatiwa rufaa halijamaliza shauri ndio maana wako mahakamani na kusema shauri lina maslahi ya umma na pia lina muda maalumu wa kuanza na kumalizika kwa mujibu wa kanuni za kuendesha mashauri ya uchaguzi 2025.
Wakili Seka alisema kuahirisha shauri hili kwa muda usiojulikana, miezi sita ikipita linakufa kwa mujibu wa sheria (by operation of law) na mahakama hii, kwa kuwa itakuwa imeahirisha shauri kwa muda usiojulikana, haitakuwa hata na mamlaka ya kuongeza muda hivyo haki za walalamikaji, zitapotea na hakuna mamlaka nyingine au mahakama nyingine inayoweza kuwarejeshea haki hiyo.
Kwa mujibu wa Wakili Seka alisema kuegemea katika uamuzi wa shauri la Legal and Human Right Centre (LHRC) ambayo walalamikiwa waliirejea katika mawasilisho yao kutaleta vurugu, kutaminya haki na tutavunja sheria.
Aliendelea kueleza kuwa upande wa walalamikiwa hawakusema ni kwa namna gani wanaweza kudhurika endapo mahakama hii itaendelea na mchakato wa kusikiliza malalamiko ya walalamikaji na kuyatolea uamuzi wa mwisho.
Aliongeza kusema hukumu itakapotoka bado watakuwa na haki ya kukata rufaa na kueleza kuwa usikilizaji wa shauri hili mpaka mwisho utasaidia Mahakama ya Rufani kusikiliza rufaa yenyewe na sio hatua hii ambapo sheria inakataza.
Kuhusu uwepo wa taarifa ya kusudio la kukata rufaa Mahakama ya Rufani, Wakili Seka alisema unaweza kuweka kusudio na usikate rufaa na kuegemea katika msemo wa Kiswahili ‘sisi sote tunanuia kwenda mbinguni, sio lazima twende’.
Wakili Seka alirejea kanuni ya 27 ya Kanuni za Mashauri ya Uchaguzi wa Wabunge za Mwaka, 2025 inayoelekeza kuwa usikilizwaji wa shauri utakapoanza utaendelea moja kwa moja isipokuwa tu kama kuna sababu ambazo zitaandikwa katika mwenendo, hivyo shauri linapaswa kuendelea kusikilizwa na sio kuahirishwa.
Akiwasilisha hoja mbadala aliiomba mahakama kama itaona ipo haja ya kuahirisha shauri hilo, basi uahirishwaji huo usiwe kwa muda usiojulikana bali kwa muda maalumu na kwamba kwenda Mahakama ya Rufani kufanya kile ambacho sheria haiwaruhusu kufanya, ni kupoteza muda.
Katika uamuzi wake mdogo, Jaji Nongwa alisema amesikiliza mawasilisho ya pande mbili na ubishani ni kama mahakama hii ina mamlaka ya kuendelea kusikiliza shauri hili wakati kuna taarifa ya nia ya kukata rufaa Mahakama ya Rufani.
“Kwanza kabisa nakubaliana na wakili Mulwambo, kila mtu ana haki ya kukata rufaa dhidi ya uamuzi wowote na haki hii ni ya kikatiba kama ilivyoainishwa katika Ibara ya 13(6)(a) ya Katiba ya Tanzania sura ya 2 Rekebu ya 2023,”alisema Jaji.
Hata hivyo, alisema haki hiyo ina masharti ambayo yamewekwa na sheria na katika shauri hili wakili Seka alirejea kifungu cha 5(2)(d) ambacho sasa ni kifungu cha 8(2)(d) cha Sheria ya Mamlaka ya Rufani sura ya 141 8 Rekebu ya 2023.
Jaji alisema kifungu hicho kinakataza rufaa au marejeo dhidi ya uamuzi au amri ambazo hazimalizi kesi mahakamani na kuongeza marejeo waliyoyarejea mawakili wa Serikali hayahusu mashauri ya uchaguzi kama lilivyo shauri hilo.
“Sheria ya uchaguzi imefafanua juu ya muda wa kufungua shauri la uchaguzi, muda ya kusikiliza shauri la msingi na rufaa na mahakama yenye mamlaka ya kusikiliza rufaa lakini haijaeleza maamuzi yanayopaswa kukatiwa rufaa,” alisema.
Jaji alisema Mahakama pia ilitaja uamuzi unaoweza kukatiwa rufaa ikiwa ni kama mtu alichaguliwa kiuhalali au amekoma kuwa mbunge, kama shauri lilifunguliwa Mahakama Kuu na kama limesikilizwa hadi mwisho.
“Ukisoma mashauri yote ya uchaguzi niliyorejea ni wazi uamuzi ambao haumalizi shauri huwezi kukatia rufaa. Katika shauri letu hakuna ubishi baada ya uamuzi juu pingamizi la awali kutolewa shauri hili linaendelea na hatua zingine za usikilizwaji.”
“Niongeze kwa kusema ukiachana na mashauri ya madai ya kawaida, mashauri ya uchaguzi yanagusa masuala ya kikatiba hivyo mahakama haipaswi kubanwa sana na ufundi, lakini pia mashauri hayo yamewekewa muda maalumu wa kusikilizwa ambayo ni miezi sita kama ambavyo nimeeleza katika uamuzi huu,” alisema Jaji.
Kutokana na uamuzi huo wa kukataa kusimamisha kesi kusubiri uwasilishaji wa rufaa ya walalamikiwa mahakama ya Rufani, Jaji Nongwa amepanga Januari 20, 2026 kuwa ndio siku usikilizwaji wa awali wa shauri hilo utafanyika.
