Undani biashara ya viungo vya sehemu za siri baada ya ukeketaji – 2

Musoma. Sehemu ya viungo vya uzazi vya wanawake baada ya ukeketaji huuzwa kwa siri labda zaidi ya ilivyo kwa dawa za kulevya, uchunguzi wa Mwananchi umebaini.

Uchunguzi uliofanyika Desemba, 2025 katika wilaya za Butiama, Musoma, Tarime na Serengeti mkoani Mara, umebaini uwepo wa biashara hiyo.

Wakati wa uchunguzi, Mwananchi ilifuata taratibu zote zinazotakiwa na lingeweza kununua sehemu hizo za siri iwapo lingetaka kufanya hivyo, lakini lilisitisha muamala baada ya kuthibitisha kuwa biashara hiyo haramu ilikuwa ikiendelea.

Uchunguzi ulibaini viungo vinavyotokana na ukeketaji kutoka kwa mwathirika mmoja huuzwa kuanzia Sh1 milioni kulingana na makubaliano yanayofikiwa, hali inayofanya biashara hiyo kuwa miongoni mwa shughuli haramu zenye faida kubwa katika eneo hilo.

Viongozi wa jadi na ngariba wanadaiwa kusambaza na kuuza viungo hivyo kwa wamiliki wa boti za uvuvi.

Inadaiwa wamiliki hao huamini kuwa matumizi ya viungo hivyo wakati wa uvuvi huvutia mavuno makubwa ya samaki na huwalinda dhidi ya mikosi na majanga.

Licha ya kuwapo sheria zinazopiga marufuku ukeketaji na biashara ya viungo vya binadamu nchini Tanzania, vitendo hivyo vinaendelea kutokana na utekelezaji hafifu wa sheria hizo.

Miongoni mwa hizo ni Kifungu cha 118 cha Sheria ya Mtoto, Sura ya 13 ya mwaka 2019, pamoja na vifungu vya 21, 22 na 169A vya Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16, marejeo ya mwaka 2022.

Kwa jumla zinakataza unyonyaji wa watoto kwa madhumuni yoyote, ikiwamo biashara haramu ya viungo na sehemu za mwili, zinaharamisha ukeketaji na kuweka wazi adhabu kwa wasiochukua hatua kwa kosa la ukeketaji.

Kutokana na ukiukwaji wa sheria unaofanyika, wasichana wanaokeketwa wanakabiliwa na hatari kubwa za kiafya, msongo wa mawazo na athari za kisaikolojia.

Ili kuchunguza madai ya biashara hiyo, Desemba 22, 2025 Mwananchi ilisafiri hadi Wilaya ya Musoma, mkoani Mara.

Kutokana na biashara hiyo kufanyika kwa siri, Mwananchi ilitafuta msaada kutoka chanzo cha siri kilicho karibu na jamii ya wavuvi.

Awali, chanzo hicho kilishtushwa na taarifa ya uwepo wa biashara hiyo lakini hakikuyapuuza madai hayo.

Chanzo hicho kilionya kuwa jukumu la uchunguzi huo lingekuwa gumu na la hatari, likihitaji uvumilivu, kujizuia kihisia na muda mrefu wa kujenga uaminifu.

Kwa mujibu wa chanzo hicho, kazi hiyo ingehitaji kuchanganyika na kujenga ukaribu miongoni mwa wamiliki wa boti za uvuvi wanaotajwa kuwa wahusika wakuu katika biashara hiyo haramu.

Ni ushauri wa chanzo hicho, muhusika kutoka Mwananchi ajitambulishe kama mwekezaji mtarajiwa, anayepanga kuendesha boti za uvuvi na kuanzisha kiwanda cha kuchakata samaki katika eneo hilo.

Baada ya kukubaliana kuhusu mkakati huo, pande hizo mbili zilitengana kwa muda.

Baadaye usiku, chanzo hicho kilipendekeza kukutana na wakala ambaye angewezesha mawasiliano na msambazaji wa kuaminika wa viungo hivyo. Makubaliano yalifikiwa mkutano ufanyike asubuhi iliyofuata.

Kwa mujibu wa mchunguzi, mkutano ulifanikiwa, wakala akaahidi kumuunganisha ama na mmiliki wa boti ya uvuvi au wavuvi wanaohusika moja kwa moja na biashara hiyo.

Hata hivyo, wakala na wasambazaji watarajiwa walionesha tahadhari kubwa, wakieleza shaka dhidi ya watu wasiowajua, hasa kwa kuwa biashara hiyo inatawaliwa zaidi na wanaume na mtandao uliojikita katika usiri mkubwa.

Wakala alipendekeza kusafiri hadi Kinesi, eneo la pembezoni mwa Wilaya ya Musoma, ambako alidai viungo hivyo vingepatikana kwa urahisi, kwani wamiliki wa boti na wavuvi katika maeneo mengine walikuwa wameanza kuwa na wasiwasi.

Jitihada za kumfikia mvuvi aliyekuwa Kinesi hazikufanikiwa. Baadaye alipopatikana walikutana eneo moja la burudani na kujadili suala hilo lakini kwa siri na tahadhari kubwa.

Wakati wa kikao hicho, wakala na mvuvi walieleza Desemba ni kilele cha upatikanaji wa viungo hivyo kutokana na kuwepo matukio mengi ya ukeketeji.

Alitaka apatiwe Sh1 milioni ili kufanikisha upatikanaji wa kiungo kimoja, tena kwa haraka zaidi.

Mchunguzi aliomba punguzo la bei hadi Sh700,000 akiahidi kulipa Sh250,000 na kumalizia Sh450,000 zilizosalia wakati wa kukabidhiwa mzigo.

Wawili hao walieleza viungo hivyo hutumiwa na wavuvi wakati wa shughuli za kawaida za uvuvi, pia huchanganywa na maji wakati wa kusafisha boti, desturi inayoaminika kuongeza mavuno ya samaki.

Baada ya kufikia makubaliano hayo, wakala na mvuvi waliondoka, wakiahidi kukabidhi viungo hivyo jioni ya siku iliyofuata.

Saa 2:00 usiku siku iliyofuata, mchunguzi alipigiwa simu akielekezwa kukutana na watu hao kwa ajili ya makabidhiano ya viungo hivyo.

Hata hivyo, mchunguzi aliomba kuahirishwa ununuzi akitaja changamoto alizokumbana nazo mwenzake aliyekuwa jijini Dar es Salaam, aliyepaswa kuwezesha malipo yaliyobaki kupitia njia za kibenki.

Mchunguzi wa Mwananchi aeleza lengo kuu la kuthibitisha uwepo wa biashara hiyo haramu lilikuwa limefikiwa na kwamba, kukamilisha muamala huo kusingekuwa na faida yoyote ya kiuandishi wala kimaadili.

Akizungumzia yaliyobainika katika uchunguzi, Mkurugenzi wa Utetezi na Mageuzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Fulgence Massawe anasema Sheria ya Kupambana na Usafirishaji Haramu wa Binadamu ya mwaka 2008 inakataza waziwazi uuzaji na usafirishaji wa binadamu pamoja na viungo vyao.

“Iwapo shughuli kama hizi zinafanyika ni makosa makubwa ya jinai. Sheria inapiga marufuku si tu usafirishaji wa watu bali pia biashara ya viungo na sehemu za mwili wa binadamu,” anasema.

Massawe anasema kesi za awali zinazohusisha watu wenye ualbino zilionesha wazi jinsi sheria za kupambana na usafirishaji haramu zinavyotumika katika makosa yanayohusisha biashara ya viungo vya mwili.

Anasema Kanuni ya Adhabu, pamoja na Sheria ya Makosa ya Kujamiiana ilianzisha Kifungu cha 169 kinachokataza ukeketaji na kutoa adhabu kali kwa wahusika.

Anasema Sheria ya Mtoto inalinda zaidi watoto dhidi ya mila na desturi hatarishi, ikiwamo ukeketaji.

Licha ya ulinzi huo wa kisheria, Tanzania bado imo miongoni mwa nchi ambazo ukeketaji unaendelea, kwa kiasi kikubwa kutokana na udhaifu wa mifumo ya utekelezaji.

Massawe anasema changamoto za utekelezaji zinatokana na vipaumbele vinavyoshindana serikalini pamoja na asili ya siri ya vitendo hivyo, hali inayofanya ugunduzi na ufuatiliaji wa kisheria kuwa mgumu.

Katika ngazi ya kikanda, anasema Bunge la Afrika Mashariki limefanya jitihada za kupitisha sheria kali zaidi zinazolenga kutokomeza kabisa ukeketaji.

Hata hivyo, utekelezaji unabaki kuwa changamoto kubwa, hasa pale viongozi wa kisiasa wanapokuwa na hofu ya kukabiliana na masuala muhimu ya kiutamaduni.

“Katika Mkoa wa Mara, mbunge au diwani anaweza kuepuka kulizungumzia suala hili kwa hofu ya upinzani. Viongozi wa jadi wana ushawishi mkubwa, wakati mwingine kuzidi mamlaka za Serikali. Wanapoamua jambo lifanyike, mara nyingi hutekelezwa, hata kama kwa siri,” anasema.

Massawe anasema ingawa baadhi ya matukio huripotiwa, ukeketaji unaendelea kufanyika kwa siri hata katika maeneo ya mijini kama vile Dar es Salaam na Pwani.

Mkuu wa Dawati la Jinsia Mkoa wa Mara, Charles Ezekiel, anapinga madai kuwa viungo vya uzazi vinavyopatikana kupitia ukeketaji vinauzwa mkoani humo.

“Hizo ni tetezi tu. Hatuna taarifa zozote kuhusu biashara ya viungo vinavyotokana na ukeketaji. Hata hivyo, polisi kwa kushirikiana na wadau wengine tutachunguza madai hayo ili kubaini ukweli,” anasema.

Ezekiel anakiri kuwapo ukeketaji miongoni mwa baadhi ya jamii za Wakurya mkoani humo, akihusisha vitendo hivyo na imani za kitamaduni.

Sebastian Kitiku, Mkurugenzi wa Maendeleo ya Watoto katika Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, anasema wizara haina taarifa za kuwapo biashara yoyote inayohusisha viungo vya binadamu vitokanavyo na ukeketaji.

“Hatujui kama viungo hivi vinauzwa, vinaweza kununuliwa na nani, au jinsi miamala yake inavyofanyika. Ikiwa biashara hii ipo, ni kinyume cha sheria na haijaidhinishwa. Shughuli yoyote ya namna hiyo hufanyika kwa siri kubwa kwa sababu ni kinyume cha sheria,” anasema na kuongeza:

“Hivi sasa, hatuna taarifa rasmi zinazoonesha kuuzwa kwa viungo hivyo. Hata hivyo, ikiwa ushahidi utapatikana, itakuwa wazi kuwa yeyote anayehusika anashiriki katika biashara haramu.”

Anasema ukeketaji umejikita katika tamaduni na mila, huku makabila mbalimbali yakitofautiana katika mtazamo kuhusu viungo vya siri vya wanawake kulingana na imani zao.

“Kwenye baadhi ya jamii za wafugaji, ikiwamo sehemu za Singida na miongoni mwa Wamasai, kuna imani kuwa kutumia viungo hivyo kwenye mazizi ya mifugo huwezesha mifugo kuzaliana na kustawi,” anasema.

 “Sitashangaa kama wavuvi mkoani Mara wana imani kama hiyo. Hizi siyo dhana za peke yao, zinaonesha malezi ya kijamii yaliyodumu kwa muda mrefu ndani ya baadhi ya jamii nchini.”

Kikitu anasema imani kama hizo zinaweza kuwapo katika mikoa mingine, ikiwamo ya jamii za wavuvi mkoani Mara.

Anakiri baadhi ya desturi zinazohusiana na ukeketaji zinaweza kuonekana za kushangaza au zisizo na ukweli kwa wageni, lakini ni halisi ndani ya jamii fulani.

“Unaweza kushangaa kuwa bado watu wanaamini vitu hivi leo, lakini hii ndiyo hali halisi tunayoshughulika nayo,” anasema.