Somali. Serikali ya Somalia imesema imefuta makubaliano yote iliyoingia na Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), ikitaja kile ilichokiita tabia ya umoja huo kudhoofisha uhuru na umoja wa nchi hiyo.
Taarifa ya kufutwa kwa mikataba hiyo iliyotolewa leo Jumatatu Januari 13, 2026, inagusa mikataba na ushirikiano unaohusiana na bandari tatu, pamoja na ushirikiano wa kiusalama na kijeshi baina ya pande hizo mbili.
Mgogoro huo unadaiwa kusababishwa na uungaji mkono wa kimyakimya wa UAE kwa hatua ya Israel kuitambua Somaliland, eneo lililojitenga, kama taifa huru.
“Baada ya kutathmini kwa makini maendeleo ya hivi karibuni na kwa kutumia mamlaka yake ya kikatiba, Baraza la Mawaziri linafutilia na kubatilisha makubaliano yote yaliyopo na Umoja wa Falme za Kiarabu,” amesema Waziri wa Habari wa Somalia, Daud Aweis Aden Duale.
Serikali hiyo imesema kuwa uamuzi huo unawahusu taasisi zote za serikali ya shirikisho, taasisi zinazohusiana nazo na tawala za kikanda, ikiwemo makubaliano na ushirikiano wote katika bandari za Berbera, Bosaso na Kismayo.
Hatua hii pia imekuja baada ya muungano unaoongozwa na Saudi Arabia nchini Yemen kusema kuwa UAE ilimsafirisha kwa siri kiongozi mmoja wa wanaotaka kujitenga nje ya nchi hiyo kupitia Berbera.
Mogadishu ilielezea tukio hilo kama “madai ya matumizi yasiyoidhinishwa ya anga ya taifa la Somalia na viwanja vyake vya ndege.”
Abu Dhabi ilijenga na inadhibiti bandari ya maji marefu pamoja na kambi ya kijeshi iliyoko katika mji wa Berbera, Somaliland.
Baraza la Mawaziri la Somalia limeagiza Wizara ya Mambo ya Nje kuijulisha rasmi UAE kuhusu uamuzi wa kufuta makubaliano hayo na kuratibu utekelezaji wake, sambamba na kuwafahamisha washirika wa kimataifa na wa kikanda.
Somalia ilisema kuwa inaendelea kuwa wazi kwa ushirikiano wa kimataifa unaojengwa juu ya heshima ya pande zote, utambuzi wa umoja na uhuru wake, pamoja na kuzingatia kanuni za kikatiba na za kimataifa.
Somaliland ilijitangaza kuwa huru mwaka 1991 lakini haikutambuliwa na taifa lolote hadi mwezi uliopita, wakati Israel ilipokuwa nchi ya kwanza kufanya hivyo, jambo lililosababisha upinzani mkali wa haraka kutoka jumuiya ya kimataifa.
Hata hivyo Umoja wa Falme za Kiarabu haujatoa taarifa kuhusiana na uamuzi uliochukuliwa na Serikali ya Somalia.
