ALIYEKUWA kocha msaidizi wa Mamelodi Sundowns, Romain Folz, amezungumzia kufukuzwa kwake na Yanga, akieleza kuwa ilikuwa ‘matokeo ya mambo mengi ya kipuuzi’.
Folz, ambaye pia aliwahi kuzinoa AmaZulu na Marumo Gallants za Afrika Kusini, alijiunga na Yanga Julai 2025 akiwa na lengo la kuendeleza mafanikio katika klabu hiyo na kuleta ushindani katika michuano ya kimataifa.
Hata hivyo, muda wake jijini Dar es Salaam ulikuwa mfupi, ukidumu kwa zaidi ya miezi mitatu, huku ripoti zikidai kuondoka kwake kulisababishwa na kipigo cha bao 1-0 dhidi ya Silver Strikers katika mechi ya kwanza ya raundi ya pili ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, Oktoba mwaka jana.
Akizungumza na KICKOff Magazine katika toleo la Januari, Folz, ambaye alishinda taji moja la Ngao ya Jamii akiwa Yanga kwa kuifunga Simba kwa bao 1-0, alisema kufukuzwa kwake hakukutokana na matokeo uwanjani bali matatizo ya nje ya uwanja ambayo hakuweza tena kuyavumilia.
“Matokeo yalikuwa mazuri na timu ilikuwa imara sana, hasa upande wa mbinu za kiufundi. Kushinda Kombe la Ngao ya Jamii ilikuwa hatua chanya,” alisema Folz na kuongeza;
“Nafanya kazi ili kushinda, hivyo kukusanya mataji ni jambo zuri kila wakati. Kufukuzwa kwangu kulikuwa matokeo ya mambo mengi ya kipuuzi ambayo mimi na benchi langu la ufundi tulilazimika kukabiliana nayo.”
“Hii siyo namna ninavyofanya kazi na sivumilii upuuzi. Nilifukuzwa baada ya kupoteza mechi yangu ya kwanza na ya pekee, nikiwa nimeruhusu bao moja tu kwa jumla. Hilo pigo halikuhusu mimi wala benchi langu la ufundi.”
“Maandalizi yetu yalivurugwa sana ndani ya klabu na nilikuwa napinga hali hiyo kwa nguvu zote. Kama mambo hayo yasingekuwepo, nisingepoteza hata mechi moja, ninalihakikishia hilo,” aliongeza Folz ambaye ni raia wa Ufaransa.
“Nilifanya wajibu wangu na nikaleta kombe. Hayo ndiyo yote. Siwezi kusema zaidi ya nilichosema. Nadhani ni lazima nibaki mtaalamu.”
Folz aliyeitumikia Yanga kati ya Julai-Oktoba 18 mwaka jana, aliiongoza timu hiyo katika mechi nane akishinda sita, sare moja na kupoteza moja akiruhusu bao moja pia akifungwa na Silver Strikers ya Malawi na nafasi yake kushikiliwa kwa muda na Patrick Mabedi kabla ya kuletwa Pedro Goncalves raia wa Ureno.
