SIMBA ipo katika mazungumzo na Mbeya City kwa ajili ya kumbeba jumla mshambuliaji, Baraka Mwangosi baada ya kuridhishwa na uwezo aliouonyesha katika michuano ya Mapinduzi Cup 2026.
Mwangosi alikuwa na kikosi cha Simba visiwani Zanzibar kwa majaribio katika michuano ya Kombe la Mapinduzi inayofikia tamati leo kwa kupigwa mechi ya fainali kati ya Azam FC na Yanga, ikielezwa benchi la ufundi limevutiwa na uwezo wake hivyo limeutaka uongozi kuhakikisha unapata saini ya mchezaji huyo wa zamani wa Mbuni FC ya Championship.
Chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya Simba kimeliambia Mwanaspoti,Simba imeonyesha nia ya kunasa saini ya mshambuliaji huyo kwa lengo la kumtengeneza aweze kuwa sehemu ya kuchukua nafasi ya Suleiman Mwalimu ‘Gomez’ ambaye anacheza kwa mkopo Simba akitokea Wydad ya Morocco.
“Ni taarifa za kweli ni mchezaji mzuri na ana uwezo mkubwa anachokosa ni uzoefu akijengwa vizuri atakuja kuwa msaada mkubwa sio tu kwa Simba, bali hata kwa timu ya taifa, Taifa Stars kwani ni mchezaji mdogo na mwepesi wa kuelewa akielekezwa,” kimesema chanzo hicho kutoka Simba na kuongeza;
“Tumekuwa tukiamini katika nyota wa kimataifa eneo la ushambuliaji kwa muda mrefu ni wakati wa kutengeneza wazawa waweze kutupunguzia gharama, ukiondoa Gomez ambaye anacheza kwa mkopo hatuna namba tisa wa ndani tukifanikiwa kumpata huyu itatusaidia.”
Chanzo hicho kilisema hawamsajili Mwangosi kwa ajili ya kumpa presha ya kuipambania timu kipindi hiki, lengo lao ni kumuandaa kwa mahitaji ya baadaye akiingia katika mifumo yao.
Mwanaspoti lilifanya jitihada ya kuwatafuta Mbeya City ili waweze kuzungumzia dili hilo, Ofisa Habari wa timu hiyo, John Jerome alithibitisha uwepo wa mazungumzo baina ya timu hizo mbili kwa ajili ya biashara ya mshambuliaji huyo.
“Simba imefuata taratibu zote juu ya Mwangosi ambaye alianza kwa majaribio na sasa wamerudi mezani kwa ajili ya biashara ya kumhitaji mchezaji huyo,” amesema Jerome na kuongeza;
“Mazungumzo bado yanaendelea Simba wapo tayari kwa biashara kinachoendelea ni makubaliano ya pande zote mbili mambo yakienda vizuri taarifa itatolewa ila hadi muda huu tunazungumza Mwangosi ni mchezaji wa City.”
Katika Ligi Kuu Bara inayotarajia kurejea wiki ijayo Mwangosi hajafunga bao lolote, ila anaasiti moja wakati Mbeya iliyorejea katika Ligi hiyo msimu huu ikishika nafasi ya 13 katika msimamo ikiwa na pointi nane kupitia mechi 10 ikishinda mbili, sare mbili na kupoteza mechi sita ikifunga mabao saba na kufungwa 13, ikiwa timu ya pili kuruhusu mabao mengi nyuma ya KMC iliyofungwa 14 kupitia mechi tisa, huku Fountain Gate ikiwa ya tatu kwa kufungwa 12.
