Uongozi Yanga wamshangaa Folz, wajibu tuhuma

Muda mfupi baada ya Kocha Romain Folz kudai alichoshwa na maisha ndani ya Yanga na kusema sababu za nje ya uwanja zilichangia kumfanya atimuliwe, klabu hiyo imejibu mapigo huku ikimtakia kila la kheri kocha huyo msaizidi wa zamani wa Mamelodi Sundowns.

Ofisa Habari na Mahusiano wa Yanga, Ally Kamwe amesema kuwa uamuzi wa kuachana na Folz ulitokana na makubaliano ya pande zote mbili hivyo inashangaza kuona kocha huyo raia wa Ujerumani akiibuka na kuichafua klabu yao kwa sasa.

“Mpira unachezwa hadharani na kila mmoja aliona timu ilivyokuwa wakati ikiwa chini ya Folz na inavyocheza hivi sasa. Yanga ni klabu kubwa ambayo haiwezi kupoteza muda wake kujibu mambo ambayo hayana msingi.

“Tulifuata taratibu zote katika kuachana na Folz na tukamtakia kila la kheri. Klabu yetu inaendeshwa kwa weledi na viongozi wake hawakurupuki katika ufanyaji wa maamuzi. Binafsi na hata klabu hatujazisikia au kuziona tuhuma hizo kwa sasa ila kama ni kweli, uongozi utaangalia taratibu za kisheria zikoje na kuona hatua gani tutachukua.

“Bado klabu inaendelea kumpa heshima yake kocha Folz na inamtakia kila la kheri katika majukumu yake na tunamuombea mafanikio zaidi,” amesema Kamwe.

Mapema jana, jarida la KICKOff katika toleo la Januari, Folz, ambaye alishinda taji moja wakati wa kipindi chake klabuni hapo, alifichua kuwa kufukuzwa kwake hakukutokana na matokeo uwanjani, bali ni matatizo ya nje ya uwanja ambayo hakuweza tena kuyavumilia.

“Ninafanya kazi ili kushinda, hivyo kukusanya mataji huwa ni jambo zuri kila wakati. Kufukuzwa kwangu kulikuwa ni matokeo ya upuuzi mwingi ambao mimi na benchi langu la ufundi tulilazimika kuupitia.

“Maandalizi yetu yalivurugwa sana ndani ya klabu, na nilikuwa napinga hali hiyo kwa nguvu zote. Bila hayo, nisingepoteza hata mchezo mmoja naweza kukuhakikishia hilo.

“Hivi sivyo ninavyofanya kazi, na sivumilii upuuzi. Nilifukuzwa baada ya kipigo changu cha kwanza na cha pekee, nikiwa nimefungwa bao moja tu kwa jumla. Kipigo hicho hakikuhusiana nami wala benchi langu la ufundi,” amesema Folz.

Folz amesema kuwa yeye na benchi lake la ufundi walitimiza vyema wajibu wao.

“Matokeo yalikuwa mazuri, na timu ilikuwa inaanza kuwa imara sana, hasa upande wa mbinu. Kushinda Ngao ya Jamii ilikuwa ni wakati mzuri.

“Nilitimiza wajibu wangu na nikaleta kombe. Hayo ndiyo yote. Siwezi kusema zaidi ya nilichosema. Nafikiri ni lazima nibaki kuwa mtaalamu,” amesema Folz.

Folz alitimuliwa na Yanga baada ya kuiongoza katika mechi mbili tu za Ligi Kuu ambazo ilishinda moja dhidi ya Pamba na nyingine ambayo ilitoka sare na Mbeya City.

Aliipa taji la Ngao ya Jamii kwa kuiongoza kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Simba.

Hata hivyo kichapo cha bao 1-0 kutoka kwa Silver Strikers ya Malawi katika mechi ya ugenini ya raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika, Oktoba 18, 2025 kilifanya uongozi wa Yanga kuamua kumtimua.