Katika ya umeme bado pasua kichwa Unguja, Serikali yasema…

Unguja. Licha ya Shirika la Umeme Zanzibar (ZECO) kuingia makubaliano na kampuni mbalimbali kwa lengo la kutatua changamoto ya umeme, bado kisiwa cha Unguja kina upungufu wa zaidi ya megawati 30 za nishati hiyo.

Hali hiyo inachangia kukosekana kwa umeme mara kwa mara katika baadhi ya maeneo, jambo linalotajwa kuleta changamoto kwa wananchi na mfumo mzima wa biashara.

Pia, imeelezwa kuwa jenereta zinazotumika kusaidia upatikanaji wa umeme ziliwekwa mwaka 2010, wakati kisiwa hicho kilipokabiliwa na changamoto ya umeme baada ya kuungua kwa waya uliopo chini ya bahari, uliolazwa kutoka Kilomoni, Tanzania Bara hadi Fumba, Unguja.

Wakieleza kero wanazopata, baadhi ya wananchi wamesema huduma ya umeme inazidi kudorora kwani hukatika bila mpangilio maalumu na ZECO haitoi taarifa yoyote juu ya hilo.

Kassim Hamdani, mkazi wa Kisauni, amesema laini yao imekuwa maarufu kwa kuzimwa kwa umeme ikidaiwa kuna maboresho.

“Tunajiuliza hivi ZECO kila siku wanafanya maboresho kwenye laini ya Fumba? Kwa kweli tunateseka, wakati mwingine wanakata dakika mbili au tatu kisha wanawasha. Hatujui lengo lao ni lipi,” amesema.

Naye mfanyabiashara wa samaki, Ngwali Juma Mahmoud, amesema kwa sasa wanalazimika kugandisha barafu kutoka sehemu nyingine ili kuepusha bidhaa zao kuharibika na kuingia hasara.

Asma Mbaraka Hashim amesema shirika la umeme linapaswa kuwaambia wananchi kama wanafanya mgao ili waandae mazingira ya kuhifadhi vitu vyao vizuri.

Amesema ZECO inatakiwa kutafuta vyanzo vipya vya umeme ikiwemo jua, upepo na mawimbi ya bahari, ambavyo vinaweza kukidhi mahitaji ya watumiaji wote badala ya majenereta yanayozidiwa na ongezeko la wananchi.

Kutokana na malalamiko hayo, Meneja Mkuu wa ZECO, Haji Haji amesema shirika hilo limewasha majenereta yaliyopo Mtoni, Unguja, ili kupunguza changamoto ya upatikanaji wa umeme.

Amesema matengenezo ya majenereta hayo yakikamilika, kutakuwa na uhakika wa kupata umeme kwa wastani wa megawati 20 hadi 21.

Amefahamisha kuwa licha ya Serikali kuchukua hatua mbalimbali kuhakikisha umeme unapatikana muda wote, pia inaendelea na mazungumzo ya kuzalisha umeme kwa kutumia maji kupitia meli ya kuzalisha umeme kwa hatua za muda mfupi.

Desemba mwaka jana, shirika hilo liliingia makubaliano ya Sh427 bilioni kwa ajili ya kuimarisha miundombinu ya umeme kwa kuondoa njia zenye uwezo mdogo wa milimita 50 na kuweka zenye milimita 150.

ZECO ilitiliana saini na kampuni ya Elecmech Switchgears ya Dubai mkataba wa Sh385 bilioni kwa lengo la kuimarisha miundombinu ya umeme.

Ilielezwa kuwa mradi huo utatekelezwa kwa miaka saba na utakuwa na maeneo manne, ikiwemo uwekaji wa vifaa vya kuhifadhi umeme wa megawati 20 na ujenzi wa kituo cha kuzalisha umeme wa jua chenye uwezo wa megawati 30.

Kwa sasa Zanzibar inapokea umeme kupitia gridi ya Taifa kutoka Tanzania Bara kwa msongo wa kilovolt 132 kwa Unguja na kilovolt 33 kwa Pemba, hata hivyo haupokewi kwa kiwango kinachotakiwa na hivyo kusababisha upotevu wa umeme.

Nyingine ni ufungaji wa vifaa vitakavyowezesha kugundua tatizo linapojitokeza na ubadilishaji wa njia na mfumo wa kusafirisha umeme kwa kilomita 210.

Pia, ZECO imesaini mkataba wa Sh42 bilioni na kampuni ya Central Electricals International Limited kuimarisha mfumo wa umeme wa Mji Mkongwe, ambapo mradi huo utajenga vituo viwili vya kupokea na kusambaza umeme pamoja na njia za usafirishaji.

Meneja huyo amesema miradi hiyo itaondoa njia zilizopo zenye uwezo mdogo kwa lengo la kuziimarisha ili zisafirishe umeme mwingi kutokana na ongezeko la matumizi.

“Ukomo wa njia za kusafirisha umeme zilizopo unalifanya shirika hili kutokuwa na njia mbadala zaidi ya kuukata ili kuepusha athari zisizotarajiwa,” amesema Haji.

Amesema miradi hiyo itasaidia kuhifadhi umeme na kutoa huduma kwa wananchi hata wakati utanapokosekana kwenye gridi.

Meneja Haji amesema Zanzibar itaondokana na tatizo la “zima–washa” ya umeme, kwani hali hiyo inasababishwa na uchakavu wa miundombinu, hivyo uwepo wa vifaa vya kuhifadhi umeme utaondoa changamoto hiyo.

Akifafanua mipango ya Serikali, Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Nishati na Madini Zanzibar, Joseph Kilangi amesema wanaendelea na utafiti wa kubadilisha njia ya zamani ya usafirishaji umeme iliyokuwa na uwezo wa kubeba megawati 45 ili iweze kusafirisha hadi megawati 100.

Amesema kisiwa hicho kinakabiliwa na upungufu wa umeme kutokana na kuzidiwa kwa matumizi katika njia zote mbili za megawati 45 na 100 kutoka Tanzania Bara.

Vilevile amesema kukamilika kwa mikataba hiyo kutaondoa tatizo la mafundi wa ZECO kuchukua muda mrefu kugundua hitilafu na kuirekebisha, kwani kwa sasa wanatumia mbinu za kizamani kufanya uchunguzi.

Kwa upande wa Waziri wa wizara hiyo, Nadir Abdullatif, amesema mkataba huo una umuhimu mkubwa kisiwani kwani unahusisha teknolojia za kisasa zitakazorahisisha utendaji kazi wa shirika na kuondoa changamoto za umeme.