Rais Samia: Mahakama Huru ni Nguzo ya Utawala Bora na Maendeleo ya Taifa.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema hakuna taifa linaloweza kufikia maendeleo endelevu na ustawi wa wananchi wake bila kuwepo kwa usimamizi mzuri wa haki unaosimamiwa na Mahakama huru, yenye uwezo na uadilifu.

Rais Samia ametoa kauli hiyo leo Jumanne Januari 13, 2025 jijini Dodoma wakati akifungua Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Chama cha Mahakimu na Majaji Tanzania (TMJA), unaoongozwa na kauli mbiu “Jukumu la Mahakama Huru Katika Utoaji Haki.”

Dkt. Samia amesema uwepo wa Mahakama huru ni nguzo muhimu ya utawala bora na ni msingi wa upatikanaji wa haki kwa wananchi, akisisitiza kuwa uhuru wa Mahakama lazima uende sambamba na uwajibikaji, uadilifu, nidhamu, utii wa sheria na uzalendo kwa taifa.

“Serikali itaendelea kuulinda na kuheshimu uhuru wa Mahakama, lakini uhuru huo hauna budi kuenda sambamba na uwajibikaji na maadili ya kazi.”

Aidha, Rais Samia amesema Dira ya Taifa ya 2025–2050 imejengwa juu ya misingi ya utawala bora, amani, usalama na utulivu, akibainisha kuwa mhimili wa Mahakama una nafasi muhimu katika kujenga taifa lenye haki na ustawi wa kudumu.

Mkutano huo wa TMJA unawakutanisha majaji na mahakimu kutoka maeneo mbalimbali nchini kwa lengo la kujadili masuala ya uboreshaji wa utoaji haki na kuimarisha utendaji wa Mahakama.