BENCHI la ufundi la Kagera Sugar limedai halitaki kufanya makosa yatakayowagharimu katika mechi zilizobaki za Ligi ya Championship na kukwamishwa kurejea Ligi Kuu Bara.
Ili kutimiza malengo ya safari ya matumaini, Kagera imetangaza vita kwa wapinzani ikituma ujumbe kuwa sasa kila mechi ni fainali na haipo tayari kupoteza.
Timu hiyo ya mkoani Kagera ilishuka daraja msimu uliopita kutoka Ligi Kuu, ambapo inashiriki Championship ikiwa kileleni kwa alama 36 katika michezo 14 sawa na Geita Gold iliyoshuka Ligi Kuu misimu miwili iliyopita ikiwa na Mtibwa Sugar ambayo imesharejea katika ligi hiyo msimu huu.
Kagera katika michezo 14 imeshinda 11 na sare tatu, imefunga mabao 27 na kuruhusu sita, sawa na Geita Gold ambapo timu hizo mbili hazijapoteza mechi yoyote.
Meneja wa Kagera Sugar, Bernard Sikira amesema kwa namna walivyoisuka timu kuanzia usajili, kiufundi, kisaikolojia na kimbinu wana matumaini makubwa ya kupanda daraja.
Sikira mwenye leseni D ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF), amesema benchi la ufundi, uongozi na wachezaji wanafanya kazi kwa ushirikiano wakiwa na dhamira ya kuipa heshima timu baada ya kugundua walipokosea msimu uliopita. “Jambo la msingi ni kwamba tuna nidhamu, makocha ambao wanaelewa timu inataka nini, tumekaa kambini kwa muda na tumetengeneza kitu ambacho walimu wanakiamini,” amesema Sikira.
“Falsafa ya Kagera na wachezaji, makocha na viongozi wote tumekuwa na dhamira moja. Kwa hiyo kila kitu kinakwenda kwa sababu ya ushirikiano, umoja, upendo. Nafikiri hivyo ndiyo vinatufanya tuwe hapa tulipo sasa hivi.”
Sikira amesema timu inapata nguvu ya kufanya vizuri kutokana na imani wanayopewa na mashabiki wa Kagera ambao wanawaunga mkono kwenye mechi.
