NDOTO ya kiungo mkabaji Ahmed Bakari ‘Pipino’, kutamani kucheza timu moja na supastaa raia wa Uganda, Khalid Aucho inakwenda kutimia baada ya kusajiliwa na Singida Black Stars.
Simba, Yanga na Azam FC msimu uliopita ziligonga mwamba kupata saini ya Pipino akiwa KMC, lakini imekuwa rahisi kwa Singida kumsainisha mkataba wa miaka mitatu na tayari kakutana na Aucho.
Kiwango alichokionyesha msimu uliopita ambapo alisajiliwa na KMC dirisha dogo akitokea kituo cha soka cha Magnet, kilimvutia aliyekuwa kocha wa timu ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ Hemed Suleiman ‘Morocco’ kumjumuisha katika kikosi kilichocheza michuano ya Baraza la Vyama vya Soka Kusini mwa Afrika (COSAFA), ambapo alichaguliwa mchezaji bora wa mechi dhidi ya Eswatini ambayo Stars ilishinda mabao 2-1.
Pipino amesema:”Nilikuwa namfuatilia Aucho tangu yupo Yanga nilitamani. Napenda anavyotumia akili kubwa katika kukaba na kutuliza timu, japokuwa sijapata muda wa kukaa naye ili nijifunze vitu vingi kutoka kwake, ila nina furaha kuona hilo linatimia.
Aliongeza: “Baada ya mazoezi kuna wachezaji wengi ambao wamenifuata na kuniambia dogo pambana utafika mbali mmojawapo ni Elvis Rupia.
“Nimejiunga SBS ya wachezaji wenye levo tofauti, najua ush-ndani ni mkubwa, inacheza michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika, naziona ndoto zangu kuna mahali zitafika, lakini nashukuru KMC iliyoona kipaji changu na ikaniamini.”
