Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imempa siku saba mshtakiwa Jamaal Saad, atafute wakili wa kumtetea, baada Peter Kibatala aliyekuwa anamtetea katika kesi ya uhujumu uchumi, kujiondoa.
Saad ni mshtakiwa wa tatu katika kesi ya kuwasilisha nyaraka za uongo katika bandari ya Dar es Salaam, na kujipatia zaidi ya Sh10 bilioni zilizotokana na shehena ya mafuta.
Mshtakiwa huyo na wenzake sita wanakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi namba 5195 ya mwaka 2025, yenye mashtaka 13 yakiwemo ya kula njama, kuwasilisha nyaraka za uongo katika bandari ya Dar es Salaam.
Hayo yamelezwa leo Jumatatu, Januari 13, 2026 wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya upande wa mashtaka kuwasomewa maelezo ya mashahidi na vielelezo washtakiwa hao.
Kabla ya wakili Kibatala kujiondoa kumtetea mshtakiwa huyo, wakili wa Serikali, Pancrasia Protas akishirikiana na Neema Kibodya alidai kuwa kesi hiyo imeitwa kwa ajili ya washtakiwa kusomewa maelezo yao pamoja na mashahidi.
Washtakiwa wanaokabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi, wakiwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu. Picha na Hadija Jumanne
Kibodya alitoa maelezo hayo, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Gwantwa Mwankuga.
Wakili Kibodya baada ya kutoa maelezo hayo, wakili wa utetezi, Glory Ulomi ambaye amemwakilisha Wakili Peter Kibatala aliieleza Mahakama hiyo kuwa Kibatala amejiondoa kumtetea mshtakiwa Saad.
“Mheshimiwa hakimu, wakili anayemtetea mshtakiwa wa tatu katika kesi hii, (Kibatala) amejiondoa na hayuko tayari kuendelea kumtetea mshtakiwa huyo hadi pale watakapofanya mazungumzo na mshtakiwa huyo,” amedai wakili Ulomi.
Ulomi baada ya kutoa taarifa hiyo, Wakili Kibodya alisema kwa kuwa wakili wa Saad amejiondoa, Mahakama impe nafasi mshtakiwa mwenyewe aseme kama yupo tayari kuendelea ili upande wa mashtaka tuwasomee maelezo.
Saad alipopewa nafasi, aliomba Mahakama impe muda ili aweze kutafuta wakili mwingine wa kumtetea.
“Mheshimiwa hakimu, naomba Mahakama yako inipe nafasi ili niweze kutafuta wakili mwingine wa kunitetea,” amesema mshtakiwa.
Hakimu Mwankuga alikubaliana na ombi la mshtakiwa huyo na kumpa siku saba ili atafute wakili wa kumtetea.
Baada ya kueleza hayo, hakimu Mwankuga aliahirisha kesi hadi Januari 21, 2026.
Mbali na Saad, washtakiwa wengine ni Joseph Matage; Grace Matage ambaye ni Mkurugenzi wa kampuni ya RHG General Traders Ltd na pia ni wakala wa forodha; Mubinkhan Dalwai; Stanley Tibihenda, Edward Omeno na Bushira Ally, ambao wote ni wakazi wa jijini Dar es Salaam.
Hata hivyo, washtakiwa wote wapo rumande kutoka na shtaka la kutakatisha fedha linalowakabili halina dhamana.
Kwa mara ya kwanza washtakiwa hao walifikishwa mahakamani hapo Februari 28, 2025 na kusomewa mashtaka yao.
Kati ya mashtaka hayo 13; matano ni ya kughushi nyaraka, matano ni ya kuwasilisha nyaraka za uongo katika Bandari ya Dar es Salaam, moja la kuongoza genge la uhalifu, jingine ni kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu pamoja na kuzitakatisha.
Katika shtaka la kuongoza genge la uhalifu linalowakabili washtakiwa wote, inadaiwa kati ya Juni Mosi na Novemba 30, 2024 katika Jiji la Dar es Salaam na maeneo mengine, washtakiwa kwa nia ovu, waliandaa genge la uhalifu kwa lengo la kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu, ambazo ni dola za Marekani 4,627,459.14 sawa na zaidi ya fedha za Kitanzania Sh6 bilioni.
Katika shtaka moja wapo la kughushi nyaraka, washtakiwa hao wanadaiwa kati ya Julai Mosi na Agosti 12, 2024 katika Jiji la Dar es Salaam, kwa njia ya udanganyifu, walioghushi nyaraka ya uongo iitwayo Delivery Order yenye kumbukumbu namba APU 04638 ya Agosti 12, 2024 kwa kuonyesha kuwa ni halali na imetolewa na kampuni ya Nyota Tanzania Ltd, kupitia wakala wa meli Maersk Group, wakati wakijua kuwa nyaraka hizo ni za uongo.
Katika shtaka moja wapo la kuwasilisha nyaraka ya uongo, washtakiwa wanadaiwa Agosti 12, 2024 kwa njia ya udanganyifu waliwasilisha nyaraka hizo katika Bandari ya Dar es Salaam kwa lengo la kuonyesha kuwa ni halali na imetolewa na kampuni ya Nyota Tanzania Ltd kupitia wakala wa meli Maersk Group, wakati wakijua kuwa ni uongo.
Vilevile katika shtaka la kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu, washtakiwa wanadaiwa kati ya Juni Mosi na Novemba 30, 2024 jijini Dar es Salaam, kwa njia ya udanganyifu walijipatia kilo 6,367,262 za mafuta ya kupikia aina Camar zenye thamani ya dola za Marekani 4,627,459 ambazo ni sawa na zaidi ya Sh10 bilioni mali ya kampuni ya AAstar Trading PTE Ltd kwa kudanganya kwamba bili halisi ya shehena ya mafuta ilitolewa na kampuni ya Nyota Tanzania Ltd kupitia Maersk Group, wakati wakijua kuwa ni uongo.
Kuhusu shtaka la kutakatisha fedha, wanadaiwa kati ya Juni Mosi na Novemba 30, 2024, washtakiwa kwa pamoja walijihusisha na miamala ya fedha yenye thamani ya dola za Marekani 4,627,459 kwa kuziweka kwenye akaunti ilizofunguliwa katika benki ya Equity yenye jina la Makange Logistics and Traders Company Limited, wakati wakifahamu kuwa miamala hiyo ni mazalia ya kosa tangulizi la kughushi nyaraka.
