Vodacom Yaendeleza Mpango wa Kapu la Vodacom Kupitia Kampeni ya “Back to School” Kusaidia Elimu Nchini

Vodacom Tanzania imeendeleza mpango wake wa Kapu la Vodacom kwa kuzindua msimu mwinginewa ‘Back to School’, hatua inayothibitisha dhamira ya muda mrefu ya kampuni katika kusaidia jamii kupitia elimu. Kupitia kampeni hii, Vodacom inalenga kuwasaidia wazazi na wanafunzi kurejea shuleni kwa kuwapatia mamia ya makapu ya vifaa vya shule (Kapu la Shule) kwa familia na wanafunzi wanaohitaji msaada zaidi katika mikoa mbalimbali nchini.

Mpango wa Kapu la Vodacom ulianza kama jitihada za kusaidia jamii wakati wa msimu wa sikukuu, lakini sasa umebadilika na kuwa harakati kubwa ya mshikamano na kujali, ikihakikisha elimu inaendelea kuwa kipaumbele kwa kila mtoto. Kupitia mpango huu, Vodacom inasimama bega kwa bega na wazazi pamoja na wanafunzi katika maandalizi ya mwaka mpya wa masomo, huku ikisaidia kupunguza mzigo wa gharama ambao huwa ni mkubwa hasa mwezi wa Januari.

Akizungumza kuhusu mpango huu, Mkurugenzi wa M-Pesa Vodacom Tanzania, Epimack Mbeteni alisema kuwa elimu ndiyo msingi wa maendeleo ya jamii na taifa kwa ujumla. Alisema kuwa kuendeleza Kapu la Vodacom zaidi ya msimu wa sikukuu ni uwekezaji wa moja kwa moja katika mustakabali wa watoto na Taifa la Tanzania.

Aliongeza kuwa mpango wa “Kapu la Vodacom Back to School” hauhusiani tu na utoaji wa misaada, bali ni kuhusu kujenga mshikamano wa kijamii na kuhakikisha kila mtoto anapata nyenzo muhimu za kufanikisha masomo yake. Alisisitiza kuwa huu si msaada wa hisani, bali ni jitihada za pamoja za kujali na kusonga mbele kama jamii moja.

Vodacom imeendelea kudhihirisha dhamira yake ya kuleta mabadiliko chanya na endelevu kupitia miradi inayowawezesha familia na kuimarisha mifumo ya elimu nchini. Kampeni ya Kapu la Vodacom ilizinduliwa rasmi mwishoni mwa Novemba mwaka jana, ikiwa na lengo la kusherehekea na kushirikiana na wateja wake kwa kuwapatia furaha na shukrani katika maeneo mbalimbali ya nchi.

Kwa ujumla, mpango huu unalenga kuleta uzoefu wa kipekee kwa wateja, kuimarisha uhusiano kati ya Vodacom na jamii, pamoja na kudhihirisha dhamira ya kampuni ya kuendelea kuwa karibu na wateja na jamii zake wakati wote.


Meneja Mauzo wa Vodacom Tanzania Plc eneo la Kawe na Bagamoyo Naomi Kasera (kulia) akikabidhi Kapu kwa Mzazi Fransisca Mosha ( Kushoto) na Mwanafunzi wa shule ya msingi Bunju A, Njma Juma (katikati) katika muendelezo wa kampeni ya “Tupo Nawe Tena na Tena” ikilenga kugawa makapu yenye vifaa vya shule kwa wateja mbalimbali nchini. Kampeni hiyo imeendelea kugawa makapu katika shule tofauti hapa nchini, Hafla hii imefanyika mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam kwa lengo la kuwaunga mkono wazazi katika msimu huu wa Watoto kurudi mashuleni kwa kutoa baadhi ya vifaaa vya shule vitakavyo wezesha Watoto kuendelea na masomo yao.