Dar es Salaam. Wanachama wa Chama cha Mapinduzi (CCM) na Watanzania wametakiwa kuacha tofauti zao ili kuchochea amani na mshikamano wa kitaifa kwa maendeleo ya nchi.
Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu wa CCM, Dk Asha-Rose Migiro katika kikao kazi na viongozi na wanachama wa chama hicho, alipokuwa akihitimisha ziara yake mkoani Dar es Salaam.
Katika kikao hicho kilichofanyika leo Jumanne Januari 13, 2026, Dk Migiro amesema sera za chama hicho zinasisitiza usawa wa watu wote, akisisitiza huo ndio msingi wa Serikali.
“Ahadi kuu ya mwana CCM inasema watu wote ni sawa, kila mtu bila kujali itikadi za vyama, kabila, dini wala rangi anatakiwa kuwa na fursa sawa na kushiriki katika maendeleo ya Taifa.
“Kwa msingi huo, tunapaswa kusimama pamoja na kushikamana kama Taifa katika kulinda Amani. Hii ndiyo maana ya falsafa ya kazi na utu,” amesema.
Katika kufanikisha ajenda hiyo, Dk Migiro ametoa wito kwa mabalozi wa mashina kusimamia maeneo yao kwa kuwatambua na kuwaunganisha wananchi ili kujenga daraja la ushirikiano kuanzia chini hadi juu.
“Licha ya kuonekana kama nafasi za chini, mashina ndiyo nguzo kuu katika maendeleo kwani kila jambo hata miradi inayojengwa inaanzia huko,” amesema.
Akieleza sababu za kuichagua Ilala kuhitimisha ziara hiyo, Dk Migiro amesema wilaya hiyo ina nafasi yake kipekee katika siasa za nchi na mkoa huo.
“Ilala ina nafasi ya kipekee katika siasa za nchi na Mkoa wa Dar es Salaam, imetoa Spika wa Bunge la Tanzania, imetoa Meya na Naibu Meya wa jiji hili,” amesema.
Sababu nyingine ni kuwa ndiyo kitovu cha biashara katika jiji hilo kuu la kibiashara nchini na makao makuu ya Serikali.
“Ikulu ya Magogoni pia ipo Ilala na kitovu cha biashara, Kariakoo kipo wilaya hii,” amesema.
Mjumbe wa halmashauri kuu ya CCM Taifa, Simba Gadafi, amesisitiza kuthamini nafasi ya viongozi wa mashina.
Gadafi amesema wajumbe hao wa mashina ni viongozi muhimu kwa ustawi wa chama na maendeleo ya nchi kwa kuwa ndio wapo katika ngazi ya chini zaidi ya jamii.
“Hawa viongozi wa mashina, ni mabalozi muhimu mno kwa ustawi wa chama na jamii kwani wao ndio wanaishi na jamii huko wanajua wapi kuna wezi, wapi kuna majambazi na kila kitu,” amesema.
Akizungumzia mafanikio ya chama hicho kwa mkoa wa Dar es Salaam, amesema wakati Taifa likipata uhuru, Dar es Salaam ilikuwa na shule saba pekee za sekondari ambapo wasichana zilikuwa tatu na za wavulana mibili pekee na zahanati nne pekee.
Amesema kwa sasa Taifa limepiga hatua kubwa zaidi kimaendeleo ambapo kila kata ina shule na zahanati hali iliyofanya wananchi wa Dar es Salaam kukiunga mkono chama hicho.
Amesema maendeleo yaliyojengwa na chama hicho katika jiji hilo yameendelea kukipa ushindi chama hicho.
Akizungumza katika kikao hicho Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Kenani Kihongosi amewataka viongozi wa na wanachama wa chama hicho kufanya kazi na kueneza habari njema za kazi zinazofanywa na Serikali ya chama hicho bila hofu.
Amesema, CCM imefanya mengi makubwa katika maendeleo ya nchi akisema hakuna mtu wala genge la watu linalopaswa kuhofiwa na viongozi wakaacha kufanya kazi za kutumikia Taifa.
“CCM imefanya makubwa katika hii nchi, miradi tunaiona hivyo hatupo hapa kuwa wanyonge,” amesema.
Aidha, ametoa wito kwa vijana kuacha kulaghaiwa na watu waliopo nje ya nchi kuharibu amani ya nchi akiwataka kusimamia Serikali na kutolea taarifa miradi inayosuasua ili ichukue hatua stahiki.
“Demokrasia yotote duniani lazima ijali mahitaji ya msingi ya wananchi wake, wananchi lazima wapate malazi, chakula na mavazi.
“Zipo Demokrasia tunachochewa huko nje tuzikatae, tusikubali kuchochewa kuchoma nchi yetu na tutoe taarifa katika miradi iliyotolewa fedha inayosuasa ili Serikali ichukue hatua,” amesema.
Akitoa Salaam za mkoa, Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, amesema mkoa wa Dar es Salaam umepokea fedha nyingi za miradi ya maendeleo ambayo inaendelea kujengwa maeneo mbalimbali.
“Mkoa wetu wa Dar es Salaam kwa fedha za miradi tulizopokea tunashukuru Serikali na tunaahidi kusimamia ukamilishaji wa miradi hiyo. Kwa Ilala pekee, tumepokea Sh317 bilioni zikilenga kujenga miundombinu ya elimu, afya, maji na barabara kwa ajili ya ustawi wa wananchi,” amesema Mpogolo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila.
Amesema katika fedha hizo, tayali Manispaa ya Ilala imeanza mradi wa ujenzi wa vituo vya afya vitano katika maeneo mbalimbali yakiwemo Vingunguti, Pugu na Mongolandege.
Aidha, amesema miradi mingine iliyoanza ni ujenzi wa shule za kisasa ili kutokomeza tatizo la uhaba wa madarasa katika manispaa hiyo.
“Katika kutatua changamoto ya miundombinu ya elimu, tayali tumeanza ujenzi wa shule nane za maghorofa unaoendelea sehemu mbalimbali nchini kupitia fedha hizi,” amesema.
Amesema ujenzi wa miundombinu ya elimu unaenda sambamba na uboreshaji wa miundombinu ya shule za msingi na sekondari katika wilaya hiyo.
“Mbali na miundombinu hiyo, zaidi ya bilioni 37 zimetengwa kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya barabara katika manispaa yetu ya Ilala,” ameongeza.
Ili kufikia lengo la kujenga umoja na amani, Mkuu huyo wa wilaya amewataka viongozi kuwatumikia wananchi kwa upendo na unyeyekevu katika kutekeleza majukumu yao.