Dar es Salaam. Wakati tatizo la bakteria ukeni likiwasumbua wanawake wengi, utafiti umebaini kuwapo uwezekano mkubwa kwa mwanamume kubeba bakteria hao na kusababisha madhara kwa mwanamke atakayejamiiana naye.
Utafiti uliochapishwa na Jarida la Tiba la The New England Journal of Medicine (NEJM), umebadili mtazamo wa muda mrefu wa kitabibu kuhusu Bacterial Vaginosis (BV) na maambukizi yake.
BV ni tatizo la kiafya linalotokana na mabadiliko ya bakteria ukeni ambalo siyo la aibu wala la kupuuzwa.
Ni hali ya maambukizi ya uke inayotokea pale uwiano wa bakteria wa kawaida ukeni unapovurugika na wale wabaya kuongezeka kuliko wazuri, inayohitaji utambuzi sahihi na matibabu ya kitaalamu ili kuepuka madhara ya muda mrefu.
Utafiti uliochapishwa na Jarida la NEJM la Uingereza, Machi 2025, umebainisha jambo ambalo madaktari wamekuwa wakilihisi kwa muda mrefu lakini hawakuwa na ushahidi wa kisayansi kuwa BV huambukizwa kwa njia ya kujamiiana na wanaume ni wabebaji wa kimyakimya wanaohitaji kutibiwa sawa na wenza wao wa kike.
Vilevile, utafiti umebaini bakteria hukaa kwenye uume, hasa ndani ya mrija wa mkojo (urethra) na kwenye govi wakati wa kujamiiana.
Inabainishwa katika utafiti kuwa, bakteria hao hupitishwa kutoka kwa mwenza mmoja kwenda kwa mwingine, hivyo kuunda mzunguko wa maambukizi ambao hauwezi kukatizwa kwa kumtibu mwanamke pekee.
Utafiti huo ulihusisha wenza 150 wa jinsia tofauti, wakiwamo wanawake wenye BV ambao walitibiwa kwa kutumia antibiotiki za kawaida, lakini nusu ya wanaume walipata matibabu ya vidonge na dawa ya kupaka.
Kwa mujibu wa watafiti, kumtibu mwanamke pekee ni sawa na kujaribu kuzima moto, huku mtu mwingine akiendelea kuuwasha.
Madaktari na wataalamu wa afya ya uzazi wanasema matokeo ya utafiti huo ni mapinduzi katika namna BV inavyopaswa kutazamwa na kutibiwa, wakisisitiza kuendelea kumtibu mwanamke pekee ni kosa la kitabibu linalowaumiza wagonjwa kwa muda mrefu.
Daktari bingwa wa magonjwa ya wanawake katika Chuo Kikuu cha George Washington, Sarah Cigna, ambaye ni mtafiti mkuu kwenye utafiti huo amesema BV kutazamwa kama tatizo la uke pekee kulisababisha madaktari kushughulikia nusu tu ya tatizo, huku wanaume wakiachwa kama wabebaji wasioonekana na wanawake wakirudia kuambukizwa mara kwa mara.
“Kutozingatia mchango wa wanaume kumesababisha wanawake kupokea dozi za mara kwa mara za antibiotiki ambazo mara nyingi hazileti suluhisho la kudumu zaidi ya nusu ya wagonjwa hupata tena BV ndani ya miezi sita,” amesema.
“Baadhi ya madaktari huogopa kuiita BV ugonjwa wa zinaa kwa kuhofia unyanyapaa unaweza kuwazuia watu kutafuta matibabu. Hata hivyo, kuichukulia kama suala la afya linalohusu wenza wote kunaweza kuwasaidia watu kuelewa na kukabiliana nayo vizuri zaidi.”
Hoja kama hiyo imetolewa na daktari bingwa wa magonjwa ya wanawake, Michael Harris, anayeeleza utafiti huo umeweka wazi kile ambacho madaktari wengi walikuwa wakihisi kwa miaka mingi.
“Tumekuwa tukiona wanawake wanarudi hospitalini mara kwa mara na BV ileile licha ya kutumia dawa. Hii ilitufanya tujiulize maambukizi yanarudi vipi? Sasa tunajua kuwa mara nyingi yanarudi kutoka kwa mwenza wa kiume ambaye hakuwahi kutibiwa,” amesema Dk Harris.
“Mwanamume anaweza kubeba bakteria hawa bila dalili zozote. Anaonekana mzima kabisa, lakini anapofanya tendo la ndoa anawarudisha kwa mwenza wake. Hii ni sababu kubwa kwa nini haiponyeki kwa urahisi.”
Akizungumza na Mwananchi, leo Jumanne Januari 13, 2026 Dk Salma Mwangala, ambaye ni bingwa wa magonjwa ya wanawake amesema wagonjwa wake mara nyingi hujilaumu au huona aibu.
“Wanawake hujihisi kama wanafanya kosa au hawana usafi, kumbe tatizo haliko kwao pekee. Mfumo mzima wa matibabu umekuwa ukiwapuuza wanaume,” amesema.
Kwa upande wake, Dk Joseph Kweka, amesema utafiti huo unapaswa kubadilisha miongozo ya matibabu.
“BV siyo tu ugonjwa wa uke. Ni maambukizi yanayohusisha wenza wawili. Tukitaka kuupunguza na kuumaliza, lazima tubadilishe sera na kuanza kutibu wanandoa au wapenzi wote kwa pamoja,” amesema.
BV siyo ugonjwa wa zinaa moja kwa moja, lakini unahusiana na kujamiiana.
Hutokea zaidi kwa wanawake walio katika umri wa uzazi na ni moja ya sababu kuu za kutokwa uchafu usio wa kawaida ukeni.
Kwa baadhi ya wanawake hawana dalili za BV, lakini za kawaida ni uchafu mweupe au kijivu ukeni, harufu kali (kama ya samaki) ambayo huongezeka baada ya kujamiiana.
Kwa baadhi huwashwa au kuhisi kuungua ukeni.
Maumivu wakati wa kukojoa au kujamiiana.
Baadhi ya sababu zinazotajwa kusababisha hali hiyo ni kubadilisha wapenzi mara kwa mara, kuosha uke kwa kemikali, kutotumia kondomu na kuvuta sigara.
Iwapo BV haitatibiwa inaweza kuongeza hatari ya kupata maambukizi ya zinaa, kusababisha matatizo wakati wa ujauzito (kujifungua kabla ya wakati na mtoto kuzaliwa na uzito mdogo)
Vilevile, kuongeza hatari ya maambukizi baada ya upasuaji wa uzazi.
BV inatibika lakini ni muhimu kutumia dawa kama ulivyoelekezwa na mtaalamu wa afya, kuepuka kujitibu bila vipimo, kumaliza dozi hata kama dalili zimepotea.