RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi Zanzibar, leo Januari 13, 2026 amezindua rasmi viwanja vya michezo vya Gombani vilivyopo Wilaya ya Chake Chake katika mkoa wa Pemba Kusini.
Katika uzinduzi huo, Dk Mwinyi ameongozana na viongozi mbalimbali wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) akiwamo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla na Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo Zanzibar, Riziki Pembe Juma.
Kabla ya kufanyika uzinduzi huo, Dk Mwinyi alikagua na kupata maelezo kuhusu viwanja vidogo viwili vilivyopo pembezoni mwa  uwanja mkubwa.
Akizugumza katika uzinduzi huo, Dk Mwinyi amesema Uwanja wa Gombani utakuwa ni miongoni mwa ongezeko la viwanja vikubwa vya kimataifa ambavyo vipo Zanzibar.
Mbali na hayo, Dk Mwinyi amewashukuru wananchi waliojitokeza kwa wingi na kufanikiwa kuujaza uwanja huo kabla ya kushuhudia fainali ya Kombe la Mapinduzi 2026 kati ya Azam dhidi ya Yanga iliyoanza saa 10:30 jioni.
Uzinduzi huo ulinogeshwa na burudani mbalimbali ikiwamo halaiki ya watoto na wasanii chipukizi kutoka Kisiwani Pemba sambamba na msanii marufu Siti Amina.
Ikumbukwe kuwa, Januari 8, 2025, Rais Mwinyi aliweka jiwe la msingi la ukarabati wa uwanja huo na ujenzi wa viwanja vingine vidogo vilivyopo pembeni ambavyo ni vya mpira wa miguu na kikapu.
Uwanja wa Gombani umefanyiwa ukarabati mkubwa, ikiwemo uwekaji wa paa jipya, ujenzi wa kuta, vyumba vya wachezaji, eneo la watu mashuhuri, maegesho, uwekaji wa minara ya taa, mifumo ya maji na umeme.
Kwa mujibu wa taarifa za ukarabati huo wa awamu ya pili, umegharimu kiasi cha Dola za Marekani 4,250,000 na umefanywa na Kampuni ya REFORM SPORTS kutoka Uturuki.
