Uganda yazima intaneti kuelekea uchaguzi mkuu, VPN marufuku

Uganda. Serikali ya Uganda imeziagiza kampuni za mitandao ya simu, wenye leseni pamoja na watoa huduma zinazohusiana na huduma hizo nchini humo kuzima intaneti.

Sambamba na hatua hiyo pia imeagiza kusitiza za simu za kimataifa kuanzia leo Jumanne Januari 13, 2026 ikiwa ni siku mbili kabla ya Uchaguzi Mkuu unatotarajiwa kufanyika Alhamisi wiki hii.

Katika barua iliyotolewa leo Jumanne na Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Mawasiliano ya Uganda (UCC), Nyombi Thembo, imeeleza kuwa serikali pia imesitisha utoaji wa kadi mpya za simu (SIM cards).

Hata hivyo, mabadiliko ya SIM (SIM swaps) na uboreshaji wa SIM (SIM upgrades) yameruhusiwa, lakini kwa masharti maalumu yaliyowekwa.

Pia, mamlaka hiyo imeziagiza kampuni hizo kuzima huduma za Mitandao Pepe ya Kibinafsi (VPN) za simu katika mitandao yao.

Kwa mujibu wa Thembo, agizo hilo limetokana na pendekezo kutoka kwa Kamati ya Usalama ya Taasisi Mbalimbali (Inter-Agency Security Committee) kuelekea uchaguzi ambao Rais Yoweri Museveni anagombea ili kutetea nafasi yake.

Kusitishwa huko kunaanza kutekelezwa kuanzia leo Jumanne saa kumi na mbili jioni Jumanne, na kutaendelea hadi amri ya kurejeshwa kwa huduma itakapotolewa na UCC.

“Hatua hii ni muhimu ili kudhibiti kuenea kwa kasi kwa taarifa za upotoshaji mtandaoni, udanganyifu wa uchaguzi, pamoja na kuzuia uchochezi wa vurugu ambao unaweza kuathiri usalama wa taifa wakati wa kipindi cha uchaguzi,” amesema Thembo.

Kwa mujibu wa UCC, mawasiliano yote ya intaneti ya umma imesema yamezuiwa katika kipindi hiki.

Mawasiliano ya intaneti ya umma yaliyolengwa ni pamoja na majukwaa ya mitandao ya kijamii, tovuti, video mtandaoni, huduma binafsi za baruapepe na programu za kutumiana ujumbe.

 “Kusitishwa huku kunahusu huduma za intaneti kupitia simu za mkononi (Mobile Broadband), nyaya za fibre optic, mistari ya kukodishwa (Leased Lines), intaneti ya waya isiyohamishika (Fixed Wireless Access), viunganishi vya redio ya microwave, pamoja na huduma za intaneti ya setilaiti,” ameongeza Thembo.

Hata hivyo, huduma maalumu ambazo zimeruhusiwa kutumika ni zile zisizo za intaneti ya simu. Hivyo endapo waendeshaji watabainika kufanya matumizi yasiyo sahihi, watasitishiwa huduma.

Ameongeza kuwa upatikanaji wa mifumo hiyo iliyotengwa utaruhusiwa kwa watumishi walioidhinishwa na utafanyika kupitia njia salama zilizowekwa kama vile anwani maalumu za IP, VPN au njia binafsi za mawasiliano.

Uganda inakadiriwa kuwa na watumiaji wa intaneti milioni 10.6, kulingana na takwimu za UCC, hali inayoonesha uzito wa kiuchumi na kijamii wa upatikanaji wa huduma za mawasiliano.

Wakati wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2021, serikali ya Uganda iliweka zuio la kitaifa la intaneti lililodumu kwa takribani saa 100.

Kwa mujibu wa makadirio ya TOP10VPN, zuio kama hilo liliigharimu Uganda hasara ya takribani Sh 390 bilioni za Uganda na kuiweka nchi hiyo miongoni mwa tano duniani kuwahi kupata hasara za kiuchumi zinazotokana na kuzimwa kwa intaneti.