Dodoma. Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda amewataka watenda wa wizara hiyo kujipanga vizuri na kujifunga mkanda katika kutekeleza majukumu yao, kwani hatakuwa tayari kumvumilia mtumishi atakayeshindwa kwenda na kasi yake.
Makonda amesema hayo saa chache baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kumwapisha Ikulu ya Chamwino, Dodoma leo Jumane, Januari 13, 2026 na baadaye kukabidhiwa ofisi na aliyekuwa waziri wa wizara hiyo, Profesa Palamagamba Kabudi.
Katika mabadiliko madogo ya Baraza la Mawaziri wiki iliyopita, Rais Samia alimteua Makonda ambaye alikuwa na naibu waziri wa wizara hiyo kuwa waziri kamili akichukua nafasi ya Profesa Kabudi ambaye aliteuliwa kuwa Waziri wa Nchi- Ofisi ya Rais- Kazi Maalumu.
Mabadiliko mengine, Rais alimteua aliyekuwa Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Patrobas Katambi kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani akichukua nafasi ya George Simbachawene ambaye uteuzi wake ulitenguliwa.
Mara baada ya uapisho huo, Makonda alikwenda moja kwa moja kukabidhiwa ofisi na Profesa Kabudi mbele ya viongozi mbalimbali wa wizara hiyo, akiwemo Naibu Waziri wake, Hamis Mwijuma maarufu Mwana FA pamoja na Katibu Mkuu wa wizara ambaye pia ni Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa.
Makonda ambaye ni pia ni mbunge wa Arusha Mjini (CCM) amesema tofauti yake na mtangulizi wake, Profesa Kabudi ni kasi, hivyo utakapofanyika uzembe hatokuwa na muda wa kutafuta rejea badala yake atachukua umuazi.
“Tofauti ya Profesa Kabudi na mimi ni kasi, sitakuwa na muda wa kutafuta rekodi. Kila mtendaji afunge mkanda wake vizuri. Hili ndilo limechangia kunifikisha hapa. Tabia yangu inajulikana, sina tabia ya unafiki. Siwezi kukuchekea wakati moyoni nimekununia. Furaha na hasira yangu utaiona.
“Mimi muda wa kusubiri sina, kwa umri wangu huu nisipokuwa na kasi ya kutimiza ndoto za Rais Samia ambaye Watanzania wamemwamini wakamchagua, nitakuwa siandiki alama njema,” amesema Makonda.
“Niwaombe waendaji katika idara na taasisi zote kila mmoja akae kwenye kiti chake na aenee, watu wa utamaduni wamebakiza jukumu moja tu la kuomba vibali. Wao kwenye wilaya na mikoa kazi yao ni kufuatilia vibali ili wapate hela, hakuna kazi nyingine inayofanyika huko hili nataka libadilike,” amesema.
Makonda amesema matarajio yake ni kuona ndani ya mwaka mmoja watendaji na watumishi wa wizara nyingine wanatamani kujiunga na wizara hiyo kutokana na mabadiliko yatakayokwenda kufanyika.
“Tunakwenda kubadilisha hadi namna ya kuvaa, ukiwa unafanya kazi kwenye wizara hii unavaa vibaya hautaingia ndani ya geti. Kuanzia kwenye muonekano lazima tuhakikishe tunaiwakilisha wizara yetu kikamilifu, tukafanye kazi kwa bidii na ujisikie fahari kila kona watu wanajua kazi yako,” amesema.
Akizungumzia vipaumbele vyake katika wizara hiyo amesema atakwenda kupeleka ushawishi serikalini kuomba kiasi cha fedha kati ya Sh1 bilioni hadi Sh2 bilioni kwa ajili ya kuwakopesha vijana waliojiajiri kwenye mitandao ya kijamii na televisheni za mtandaoni waweze kununua vifaa vya kisasa.
“Vijana wengi wa Taifa hili wamejiajiri kwenye habari, hasa online TV na mitandao ya kijamii, tutaomba mamlaka kupitia Rais Samia atupatie fedha kiasi cha Sh1 bilioni hadi bilioni 2 tuwakopeshe vijana wa kwenye mitandao wawe na vifaa vya kazi vya kisasa,” amesema.
Eneo lingine alilopanga kulifanyia kazi ni kuanzisha kitengo cha mawasiliano ya lugha mbalimbali za kimataifa ndani ya wizara hiyo ili kuongeza wigo wa utoaji taarifa zinazohusu Tanzania kimataifa.
“Tunatamani wizara yetu iwe na kitengo cha mawasiliano ya lugha mbalimbali za kimataifa, tutakuwa na timu maalumu ambayo kazi yake kutengeneza habari na kuzipeleka kwenye vyombo vya kimataifa ili habari zetu zijulikane duniani,” amesema.
Katika michezo amesema anatamani kuona maandalizi ya michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027 ambayo yanaandaliwa na nchi tatu za Tanzania, Uganda na Kenya yaanze sasa, ikiwezekana yaanzishwe mashindano ya Pre AFCON yatakayoendeshwa kwenye sekondari zote nchini ili kuwaandaa Watanzania na kuchagiza vipaji vya vijana.
Awali, Profesa Kabudi amemtaka Makonda kusimamia maagizo 49 ambayo ni matokeo ya kikao kazi kilichofanywa kwa idara na taasisi zilizo chini ya wizara hiyo.
“Hakuna wizara kijiwe, kijiwe mnaamua nyie wenyewe. Nawaomba wafanyakazi mumpokee waziri wenu na mpeni ushirikiano kama mlionipa mimi.
Wizara hii ni muhimu sana, sikujua umuhimu wake hadi pale nilipoteuliwa, wizara hii ndiyo fahari ya taifa letu, ndiyo kisima na hifadhi ya utambulisho wa taifa letu,” amesema Profesa Kabudi.
Kuhusu maagizo hayo, Makonda amesema atayatumia kwenye majukumu yake ndani ya wizara hiyo ya kumweleza Profesa Kabudi kwamba akisikia kelele za watumishi, ajue ni utekelezaji wa maagizo hayo ambayo atayasimamia kikamilifu.
Kwa upande wake, Mwana FA amemshukuru Profesa Kabudi kwa aina yake ya ualimu aliyompatia katika kipindi cha uongozi wake ndani ya wizara hiyo.