Tabora. Matumizi ya nishati mbadala yameendelea kutajwa kuwa suluhu ya kudumu ya kukabiliana na uharibifu wa mazingira na changamoto za kiafya zinazotokana na matumizi ya nishati isiyo rafiki kwa mazingira, huku wadau wakihimizwa kuwekeza na kuhamasisha matumizi yake kwa wananchi.
Katika muktadha huo, washiriki wa kozi ya 14 kutoka Chuo cha Taifa cha Ulinzi Tanzania (NDC) wapo mkoani Tabora kwa ziara ya siku sita ya mafunzo kwa vitendo, yenye lengo la kulinganisha nadharia waliyojifunza darasani na utekelezaji wa sera na mipango ya Serikali katika mazingira halisi.
Ziara hiyo ni sehemu ya tathmini ya utekelezaji wa sera za kitaifa katika nyanja za kiuchumi, kisiasa na kijamii, ambapo washiriki wametembelea kiwanda cha kutengeneza majiko banifu, mashine za kuzalisha mkaa mbadala pamoja na uzalishaji wa mkaa huo.
Akizungumza leo Januari 13, 2026 wakati wa ziara hiyo, Kaimu Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Ulinzi Tanzania, Brigedia Jenerali Charles Ndiege amesema matumizi ya nishati mbadala yanapaswa kuendelea kuhamasishwa kutokana na mchango wake katika kulinda mazingira na kuboresha afya za watumiaji.
Amesema kupitia ziara hiyo, wanatazama kwa kina namna sera za kitaifa zinavyotekelezwa katika ngazi ya mikoa, ikiwemo sera za afya, mazingira, usalama, elimu, kijamii na kisiasa, akisisitiza kuwa miradi ya mkaa mbadala ni miongoni mwa suluhu za kupunguza uharibifu wa mazingira.
“Tukiwa na miradi kama hii maeneo mengi na bei ikawa rafiki, itawawezesha wananchi na taasisi kutumia mkaa mbadala, kuhifadhi misitu yetu na kuboresha afya za watu kwa kupunguza hewa chafu,” amesema Ndiege.
Kwa upande wake, Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Tabora ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Kaliua, Gerald Mongela amesema mkoa huo upo salama na washiriki wa kozi hiyo wataendelea kuwa salama katika kipindi chote cha ziara yao.
Aidha, Kanali Samwel Oloko kutoka nchini Kenya, ambaye ni mshiriki wa kozi hiyo, amesema mafunzo ya vitendo wanayoyapata ni fursa muhimu kwao kuyatumia katika mataifa yao.
“Sasa takataka nyingi zina thamani kwa kuwa zinaweza kutumika kuzalisha nishati na kulinda mazingira,” amesema Oloko.
Naye mshiriki wa kozi hiyo kutoka Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA), Godfrey Fumbuka amesema usalama wa mazingira ni msingi wa ulinzi wa Taifa.
Muonekano wa mkaa mbadala ukiwa unawaka kwenye jiko tayari lwa ajili kupikia.
“Mazingira yakiharibika, watu hawawezi kuishi kwa amani, na hatimaye usalama wa taifa huathirika. Ni muhimu kutumia nishati mbadala kulinda mazingira,” amesema.
Kwa upande wake, mkurugenzi wa kiwanda cha kuzalisha mkaa mbadala, Leonard Kushoka ameishukuru Serikali kwa kuendelea kuwaunga mkono wawekezaji wa ndani, huku akiomba kupanuliwa kwa masoko ya bidhaa hiyo.
“Bado soko la mkaa mbadala halijapanuka vya kutosha, ilihali ni bidhaa rafiki kwa mazingira na inastahili kupata masoko makubwa zaidi,” amesema Kushoka.
