Watumishi, wanasiasa waaswa kupima afya kuepuka vifo vya mapema

Dodoma. Watumishi na wanasiasa wametakiwa kuwa na utaratibu wa kupima afya zao mara kwa mara ili kuepuka vifo vya mapema vinavyoweza kuzuilika, iwapo magonjwa yatagundulika katika hatua za awali.

Wito huo unakuja katika kipindi ambacho kumeshuhudiwa vifo kadhaa vinavyotokana na magonjwa yasiyoambukiza, yakiwemo shinikizo la damu na kisukari, ambayo huathiri watu wengi wakiwa katika umri wa nguvu kazi.

Hayo yamesemwa leo Jumanne Januari 13, 2025 na Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Benjamin Mkapa, Profesa Abeli Makubi wakati akizungumza kwenye hafla ya utiaji saini wa mkataba wa ushirikiano wa matibabu baina ya watumishi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, kampasi ya Mkwawa iliyofanyika hospitalini hapo.

Profesa Makubi amesema licha ya watumishi kuwa mstari wa mbele kutoa huduma kwa baadhi yao huchelewa kupima afya zao, jambo linaloathiri afya zao kwa kiasi kikubwa na kupelekea vifo vya mapema.

“Tuna jukumu la kuzuia vifo vya awali kwa kuzingatia taratibu za afya ikiwemo upimaji wa afya na kuanza matibabu mapema,” amesema Profesa Makubi.

Amesisitiza kuwa mbali na kuondoa hatari ya vifo huduma hizi, pia, hupunguza gharama za matibabu na kuongeza uwezekano wa kupona haraka ikiwa mgonjwa atazingatia maelekezo ya wataalamu.

Naye Rasi wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Mkwawa, Profesa Method Semiono amesema kupitia mkataba huo wanakusudia kufanikisha utoaji wa huduma za awali na matibabu ya jumla kwa watumishi wa taasisi hiyo ambao wapo zaidi ya 500.

Profesa Semiono amesema awali walikuwa wakikosa huduma bora za afya kutokana ukosefu wa utaratibu mzuri wakati wa matibabu, hali iliyosababisha baadhi ya watumishi kukata tamaa za kutafuta huduma za afya kwenye taasisi za uhakika.

“Si kwamba hatupendi kupima afya, isipokuwa utaratibu mbovu huwanyima wengi nafsi ya kupima afya zao na kujikuta wakiishia kununua dawa ili kujitibu, kitu ambacho si sahihi kitaalamu,” amesema Profesa Semiono.