Mbunge Mbeya Vijijini kuvalia njuga utunzaji mazingira kulinda vyanzo vya maji

Mbeya. Mbunge wa Mbeya Vijijini, Patali Shida amesema atavalia njuga suala la utunzaji wa mazingira kwa kutoa elimu athari ya mabadiliko ya tabia nchi na kuhamasisha jamii kulinda vyanzo vya maji kwa masilahi ya vizazi vijavyo.

 Hatua hiyo itasaidia kutunza mazingira na kurejesha uoto wa miti ya asili iliyotoweka kutokana na shughuli za kibinadamu.

Patali amesema Januari 12, 2026,wakati akiwa mgeni rasmi kwenye zoezi la upandaji miti 1,000 kati ya 10,000, kwenye Kituo cha Afya cha Mamlaka ya Mji ya Mbalizi,Wilaya ya Mbeya.

“Kumekuwa na changamoto kubwa ya uharibifu wa mazingira hususani ukataji miti onyo na uvamizi wa vyanzo vya maji katika hilo niwatake wananchi kulinda rasilimali hizo kwa  wivu mkubwa kwa masilahi ya vizazi vya sasa na baadaye,”amesema.

Patali amesema ili nchi iwe salama katika masuala ya uchumi na mazingira ni lazima kuelekeza nguvu katika upandaji wa miti na kupinga shughuli za ukataji wa miti kiholela hususani katika vyanzo vya maji.

“Jambo hilo naendelea nalo katika maeneo mbalimbali kwenye ziara zangu najaribu kuwakumbusha wananchi waishi katika misingi ya kutunza na kulinda mazingira ili kurejesha uoto wa miti ya asili,” amesema.

Katika hatua nyingine, Patali ameomba vyombo vya habari kubeba ajenda hiyo kutoa elimu kwa jamii kuhusiana na athari ya kimazingira yatokanayo na uharibifu wa mazingira kwa kukata miti ovyo na kuvamia vyanzo vya maji kwa shughuli za kibinadamu.

Ofisa Maliasili na Utunzaji wa Mazingira Wilaya ya Mbeya, Gerald Shayo amesema lengo ya upandaji wa miti hiyo ni kurejesha uoto wa asili katika vyanzo vya maji na maeneo ya misitu yaliyoharibika huku miti 10,000 imepandwa maeneo mbalimbali.

“Lakini tunatoa tahadhari kwa wananchi kuachana na dhana ya kuchoma misitu kwa ajili ya kilimo kwani wanaangamiza miti mingi na badala yake wailinde,”amesema.

Amesema kuwa asilimia kubwa misitu ya asili inachomwa hususani kwenye maeneo ya mipaka, kutokana na hali hiyo jamii inapaswa kubadilika kwa kuunga mkono jitihada za Serikali katika  kuilinda kwa kugeukia kupanda miti ili kulinda vyanzo vya maji.

Mkazi wa Mamlaka ya Mji wa Mbalizi, Joyce Bakari amesema ili kufikia malengo ya kutunza mazingira ufike wakati elimu kutolewa na sheria zisimamiwe  kikamilifu.

“Jamii bado haina uelewa juu ya utunzaji wa mazingira na uvamizi wa vyanzo vya maji kwa shughuli za kijamii hususani kilimo ni vyema sasa watu wa mazingira kutoa elimu na kuvalia njuga sheria ili kukomesha,”amesema.