Fainali ya Kombe la Mapinduzi 2026 kati ya Azam dhidi ya Yanga iliyochezwa Jumanne ya Januari 13, 2026, haijawa nyepesi kwani kipute kimepigwa hadi dakika 120 ndipo mshindi akaja kupatikana, huku ubabe ukitawala naYanga ikitwaaa ubingwa wake wa tatu.
Yanga imefanikwia kuchukua ubingwa huo baada ya kushinda kwa penalti 5-4 kwenye mchezo huo.
Hata hivyo, Yanga ilijichelewesha yenyewe baada ya Pacome Zouazoa kukosa mkwaju wa penalti dakika ya 115, ambayo iliokolewa na Aishi Manula baada ya mchezaji wa Azam kuunawa mpira kwenye boxi.
Mechi hiyo iliyochezeshwa na mwamuzi wa kati, Nasir Salum Siyah ‘Msomali’, huku Ally Ramadhan Rajab ‘Kibo’ akiwa mwamuzi msaidizi namba moja na Ali Ahmada Mbwana ‘Kihonda’ ni mwamuzi msaidizi namba mbili, ilishuhudiwa kadi moja nyekundu aliyoonyeshwa nyota wa Azam FC, Cheikna Diakite.
Diakite alitolewa uwanjani dakika ya 73, kufuatia kuonyeshwa kadi ya pili ya njano kwa kumchezea vibaya Kibwana Shomari. Kabla ya hapo, dakika ya 55 alionyeshwa kadi ya njano kwa kumchezea vibaya Dickson Job.
Katika dakika 15 za kwanza, mechi ilikuwa ya kusomana sana, huku rafu za hapa na pale zikifanyika sambamba na mashambulizi machache kila upande ukiingia boksi la mwenzake mara mbili.
Kipindi cha kwanza, muda mwingi mpira ulikuwa katikati ya uwanja huku timu zote zikitumia zaidi upande wa kushoto kutengeneza masambulizi. Yanga ilikuwa inatumia anapocheza Pacome na Chadrack Boka, wakati Azam ikipitia alipokuwa akicheza Landry Zouzou na Cheikna Diakite. Hata hivyo, hakuna aliyetikisa nyavu za mwenzake.
Kipindi cha pili, yalifanyika mabadiliko ya wachezaji kila upande ambapo Azam kipindi cha pili kabla ya kuanza, ilimtoa Feisal Othman, nafasi yake ikachukuliwa na Alobogast Kyobya. Baadaye dakika ya 68, James Akaminko akampisha Yahya Zayd na Ngita Kamanya aliingia kuchukua nafasi ya Jephte Kitambala.
Yanga nayo ilifanya mabadiliko dakika ya 68, Celestine Ecua akampisha Edmund John na Chadrack Boka nafasi yake ikachukuluwa na Mohamed Hussein, kisha Duke Abuya akampisha Mudathir Yahya.
Zilipoongezwa dakika 30 baada ya zile 90 kukosa mshindi, Yanga ikamtoa Edmund John, akaingia Emmanuel Mwanengo, huku Azam nayo ikimtoa Himid Mao, akaingia Sadio Kanoute.
Pamoja na Azam kuwa pungufu lakini walionyesha kiwango bora dakika 30 za nyongeza.
Baada ya dakika 120 mwamuzi aliamuru kuwa ni mikwaju ya penalti ambapo Yanga ilifunga penalti zake kupitia kwa Mwanengo, Prince Dube, Pacome, Mudathir Yahya na Bakari Mwamnyeto.
Huku Azam ikifunga kupitia kwa Zayd, Nuru Kwane, Kanoute na Ngita Kamanya, huku Zouzou akikosa mkwaju wake na kuipa Yanga ubingwa, ikiwa inaendelea kutawala kwenye makombe nchini baada ya msimu uliopita kutwaa makombe yote makubwa.
