RAIS DKT. MWINYI AFUNGUA RASMI UWANJA WA MPIRA WA MIGUU WA GOMBANI, PEMBA

::::::::

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, ameufungua rasmi Uwanja wa mpira wa miguu wa Gombani uliopo Wilaya ya Chake Chake, Mkoa wa Kusini Pemba.

Hafla hiyo imehudhuriwa na Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Said Shaib Mussa, pamoja na viongozi mbalimbali wa Serikali, wadau wa michezo na wananchi.


Akizungumza katika hafla hiyo, Rais Dkt. Mwinyi amesema kuwa kukamilika na kufunguliwa kwa uwanja huo ni ushahidi wa dhamira ya dhati ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuendeleza na kuimarisha miundombinu ya michezo. 

Amesisitiza kuwa uwekezaji huo unalenga kukuza vipaji vya vijana, kuimarisha afya ya jamii, kuimarisha mshikamano wa kitaifa, pamoja na kuchochea maendeleo ya kiuchumi kupitia utalii wa michezo.

Aidha, Rais Dkt. Mwinyi ameeleza kuwa Uwanja wa Gombani utakuwa chachu muhimu ya maendeleo ya michezo, kwa kutoa fursa kwa vijana kushiriki michezo ya ushindani, kuandaa mashindano ya kitaifa na kimataifa, na hivyo kuitangaza Zanzibar katika medani ya kimataifa.

Kufuatia ufunguzi huo, Uwanja wa Gombani unatumika leo, Januari 13, 2026, kuanzia saa 10:30 jioni, kwa mchezo wa fainali ya Kombe la Mapinduzi, unaovikutanisha timu za mpira wa miguu za Azam FC na Young Africans SC, ikiwa ni sehemu ya shamrashamra za Maadhimisho ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar.