Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amemtaka Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda na Naibu wake, Hamis Mwinjuma maarufu Mwana FA kuacha malumbano na badala yake washirikiane kikamilifu katika utekelezaji wa majukumu yao ya kazi.
Rais Samia amesema hatasita kuwaweka kando viongozi watakaoshindwa kufanya kazi kwa ufanisi kutokana na migogoro ya ndani, akisisitiza Serikali yake inahitaji utendaji siyo migongano.
Mkuu huyo wa nchi ametoa onyo hilo leo Jumanne Januari 13, 2026, Ikulu ya Chamwino, mkoani Dodoma wakati wa hafla ya kuwaapisha mawaziri na mabalozi wapya aliowateua hivi karibuni.
Rais Samia Suluhu Hassan akimuapisha Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda leo Jumanne Januari 13, 2026 Ikulu ya Chamwino, Dodoma. Picha na Ikulu
Katika mabadiliko mdogo ya baraza la mawaziri aliyoyafanya hivi karibuni, Rais Samia alimpandisha Makonda kutoka naibu wa wizara hiyo na kuwa waziri alichukua nafasi ya Profesa Palamagamba Kabudi ambaye alimteua kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Ikulu- Kazi Maalumu.
Aidha, aliyekuwa Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Patrobas Katambi aliteuliwa kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi akichukua nafasi ya George Simbachawene ambaye uteuzi wake ulitenguliwa.
Rais Samia katika hotuba yake fupi amesema:”Nimeona nikupandishe (Makonda) uwe Waziri wa Michezo, na nadhani hizi pilika ndizo zinazokufaa. Wewe siku moja kuamua kufunga mitaa ukafanya nyama choma si kazi kubwa kwako, ni kazi rahisi.”
Amesema Wizara ya Michezo ina vijana wengi, hivyo Makonda na Naibu wake Hamis Mwinjuma wataweza kufanya kazi vizuri kwa kushirikiana.
“Naelewa wote ni vijana na wote ni wadogo. Sitaki kwenda kusikia mizozo huko. Kagawaneni majukumu yenu, kila mmoja asimame kwenye wajibu wake na Makonda utakuwa msimamizi mkuu wa kumuangalia mwenzio,” amesema.
Viongozi mbalimbali wakila kiapo katika nyadhifa tofauti serikalini, katika hafla iliyofanyika leo Jumanne Januari 13, 2026 Ikulu Chamwino, Dodoma. Picha na Ikulu
Rais Samia amesisitiza hataki kusikia migogoro katika wizara hiyo, akionya endapo atasikia hali hiyo, wote wawili wataondolewa, akibainisha amewapeleka kufanya kazi na siyo kulumbana.
Akizungumza kuhusu mabalozi wapya aliowaapisha, Rais Samia amewataka kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu na kulinda heshima ya Taifa popote watakapopangiwa.
“Tunatarajia mtaenda kuiwakilisha Tanzania, kupeperusha bendera ya Taifa na kufanya kazi kwa kushirikiana na mtakaowakuta kule. Ninyi ni wasemaji wa nchi katika maeneo mtakayopangiwa; ukishusha heshima, ujue Taifa lako umelishusha heshima,” amesema Rais Samia.
Mabalozi aliowaapisha wanaosubiri kupangiwa vituo vya kazi ni Cyprian Luhemeja ambaye alikuwa Katibu Mkuu, Ofisi ya Makamu wa Rais- Muungano na Mazingira, Zena Ahmed Said ambaye kabla ya uteuzi alikuwa Katibu Mkuu Kiongozi wa Zanzibar na Waziri Rajabu Salum.
