Wananchi Uganda kuamua hatima ya Museveni, Bobi Wine kesho

Kesho, wananchi wa Uganda wanatarajia kupiga kura kumchagua Rais wan chi hiyo atakayeongoza kwa miaka mitano ijayo, akitarajiwa kubeba mustakabali na matakwa ya wananchi wa nchi hiyo ya Afrika Mashariki.

Rais wa Uganda, Yoweri Museveni (81), anayegombea muhula wa saba, anakabiliwa na ushindani mkali kutoka kwa mgombea wa chama cha National Unity Platform (NUP), Robert Kyagulanyi maarufu kama Bobi Wine.

Katika uchaguzi huo utakaojumuisha wagombea wanane wa nafasi ya urais, wananchi wataamua nani awe kiongozi wao huku kukiwa na madai ya ukandamizaji dhidi ya upinzani husasani chama cha Bobi Wine.

Museveni ambaye ameliongoza taifa hilo na chama chake cha National Resistance Movement (NRM) tangu mwaka 1986, amejigamba kushinda tena uchaguzi huo huku akiendelea kuahidi hali bora za maisha kwa Waganda.

Mbali na nafasi moja ya urais, nafasi nyingine zitakazoshindaniwa katika uchaguzi huo ni pamoja na wabunge kwenye majimbo 353 na wabunge wawakilishi wa wanawake 146, mmoja kwenye kila wilaya.

Vilevile, wagombea wengine wa nafasi ya urais, mbali na Museveni na Bobi Wine, ni Frank Bulira, Robert Kasibante, Joseph Mabirizi, Nandala Mafabi, Mugisha Muntu na Mubarak Munyagwa.

Mwanasiasa mashuhuri wa upinzani, Kizza Besigye, ambaye amewahi kumkabili Rais Museveni mara nne katika chaguzi za urais, hakuweza kushiriki safari hii na bado anashikiliwa gerezani akikabiliwa na mashtaka ya uhaini, kufuatia kukamatwa kwake nchini Kenya mwaka 2024. Besigye amekanusha tuhuma hizo, akisisitiza hana hatia.

Wapigakura walioandikishwa katika uchaguzi huo ni 17,658,527 ambapo wanaume ni 8,439,564 sawa na asilimia 47.79 wanawake ni 9,218,963 sawa na asilimia 52.21. Vituo vya kupigia kura nchini humo ni 34,344 katika majimbo 353.

 Hatimaye, baada ya miaka mitano ya mijadala isiyokoma kwenye vyombo vya habari, mabaa, maeneo ya kula nyama choma, vilabu vya afya, mazishi na kila kona ya jamii kuhusu Uchaguzi Mkuu wa 2026, sasa siku hizo zimeisha na uchaguzi umewadia.

Kwa bahati mbaya, kwa uhalisia wa siasa za Uganda, haikuwa muda mrefu tangu vumbi la Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2021 litulie ndipo mjadala wa uchaguzi wa2026 ukaanza. Hili linaonyesha namna siasa zilivyo kiini cha karibu kila jambo nchini humo.

Kwa mujibu wa Tume ya Uchaguzi ya Uganda, kampeni za urais zilizofanyika kwa miezi miwili, zimehitimishwa Januari 13, 2026, siku mbili kabla ya siku ya kupiga kura ambayo ni kesho, Januari 15, 2025.

Kampeni hizo zimekuwa za kukatisha tamaa kwa vyama vyote vya siasa na wagombea wote wanane wa urais.

Badala ya hoja na sera, kilichotawala vichwa vya habari ni ukandamizaji na vitisho dhidi ya wafuasi wa upinzani, kuzuiwa kwa mikutano ya kampeni, pamoja na upendeleo wa vyombo vya habari vinavyomilikiwa na Serikali.

Kampeni hii imeonekana kama ya mwaka 1996, badala ya kuakisi mahitaji na uhalisia wa mwaka 2026. Ikumbukwe kuwa kutokana na janga la Uviko-19, uchaguzi wa 2020 uliendeshwa chini ya kile kilichoitwa “kampeni ya kisayansi”, ambapo mikusanyiko ilizuiwa na wagombea walihimizwa kutumia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii kufikisha ujumbe wao.

Msimu wa kampeni wa mwaka 2025 ulipaswa kujengwa juu ya uzoefu huo. Uchaguzi wa mwaka 2020 ulipaswa kuwafundisha wanasiasa kwamba kampeni, kuanzia ngazi ya ubunge hadi urais, inaweza kufanyika kikamilifu kupitia vyombo vya habari. Mbali na kuwa nafuu kwa gharama, njia hii huokoa muda na nguvu, na muhimu zaidi hufikia watu wengi zaidi.

Kwa mfano, kuonekana kwenye kituo cha redio Jinja au Mbarara, Gulu au Masaka kunaweza kusikilizwa na watu takribani 30,000. Hii inaweza kuonekana idadi ndogo kwa redio, lakini kwa mkutano wa hadhara uwanjani au viwanja vya Boma, ni umati mkubwa unaovutia macho.

Mabango ya kampeni yanayofifia kwa jua au mvua, au kuraruliwa na wapinzani, huendelea kubaki salama kwenye mitandao ya kijamii, bila kugharimu mamilioni ya shilingi kuchapishwa.

Kwa vipimo vyote, kampeni ya kisayansi ya mwaka 2020 ilikuwa na manufaa na ilipaswa kuwa kiwango kipya. Badala yake, wagombea wa urais na wengine walirejea katika mtindo wa kampeni wa miaka ya 1990 unaosisitiza mabango na mikusanyiko ya watu.

Miongoni mwa wagombea vijana zaidi katika kinyang’anyiro hiki, Bobi Wine wa NUP (43) ndiye ambaye mtu angeweza kudhani angekuwa mstari wa mbele kuelewa mwelekeo wa teknolojia unaounda uchumi na jamii ya karne ya 21. Bobi Wine angeweza kusukuma ajenda ya kidijitali na matumizi ya teknolojia za kisasa ili kuijenga upya Uganda.

Badala yake, kama walivyo wagombea Museveni wa NRM na Nandala Mafabi wa FDC, Bobi Wine aliahidi mambo ya kawaida ya enzi za analojia — ajira, shule bora na hospitali bora.

Mgombea wa ANT, Meja Jenerali mstaafu Mugisha Muntu, hasa, alikuwa wa kukatisha tamaa licha ya kuwa na sifa nyingi za kumuinua. Muntu amekuwa akionekana kama mwanasiasa wa wasomi au anayependwa na wasomi. Kwa wanasiasa wengi, hili huonekana kama dosari kwa kuwa hupenda kuonekana kama “mtu wa watu”.

Hata hivyo, katika masoko ya kisiasa, hilo ni mgawanyiko muhimu. Muntu angekumbatia taswira hiyo na kuelekeza kampeni yake kwenye miji mikubwa 10 badala ya kutumia miezi mitano kuzunguka vijijini na hatimaye kupata kura zisizozidi 100,000, huku akishindwa kuwavutia wakulima wadogo na kupoteza fursa ya kushawishi wasomi wa mijini.

Wanajeshi wengi wa sasa na waliostaafu wanamheshimu kwa uadilifu na nidhamu yake. Alipaswa kujua hilo na kujenga ujumbe wa kampeni juu ya sifa hizo. Ingawa alisisitiza nidhamu katika hotuba yake kwa vyombo vya habari wakati wa uteuzi, katika kampeni za vijijini alionekana kuiacha ajenda hiyo na kurejea ahadi zilezile za kawaida.

Hali ilikuwa kama hiyo kwa Nandala Mafabi, ambaye alifanya kampeni nchi nzima bila kupata mvuto mkubwa. Akiwa tayari ana uungwaji mkono mkubwa katika eneo la Bugisu, angeweza kuacha baadhi ya maeneo kama magharibi na kuelekeza nguvu zake Bugisu, Busia na labda Busoga.

Katika mikutano kadhaa, alisisitiza taaluma yake ya uhasibu na kuahidi uwajibikaji na huduma bora. Kwa maandishi, ujumbe wake ulikuwa na mantiki, lakini alishindwa kugusa hisia za ndani zaidi. Baada ya yote, rushwa iliyokithiri Uganda kwa zaidi ya miaka 35 si kwa sababu ya uhaba wa wahasibu au wakaguzi wa hesabu.

Kwa uhalisia, ujumbe wake ungeweza kuwa — kwa lugha laini — hoja kwamba ni zamu ya mashariki mwa Uganda kupata uongozi wa juu, ikizingatiwa kuwa eneo hilo halijawahi kutoa rais tangu uhuru. Hoja hiyo ingeweza kuuzika kisiasa.

Pia, alipaswa kushughulikia chuki iliyopo katika baadhi ya maeneo kutokana na nafasi yake katika mgawanyiko wa chama cha FDC, kama njia ya kurejesha uungwaji mkono.

Kwa upande wake, mgombea wa NRM, Rais Museveni, aliendesha kampeni yenye ujumbe unaochanganya. Yeye, zaidi ya wagombea wengine, anafahamu kuwa siasa si sera pekee bali pia utambulisho na hisia za haki.

Sababu mojawapo ya muungano wa Popular Resistance Army na Uganda Freedom Fighters ya Yusufu Lule mwaka 1981 ilikuwa kupanua mvuto wake zaidi ya Banyankore na Banyarwanda. Vivyo hivyo, uteuzi wa makamu wa rais Mkatoliki au mawaziri kutoka maeneo fulani ulikuwa mkakati wa kisiasa.

Hata hivyo, katika kampeni ya 2025–2026, alielekeza takribani asilimia 90 ya ujumbe wake kwenye masuala ya uchumi wa maendeleo na mikopo midogo. Ziara yake iligeuka kuwa tathmini ya kitaifa ya Mpango wa PDM — mbegu hapa, mbuzi pale, fedha kwa Saccos, nyavu za uvuvi kwa maeneo ya mwambao.

Inaonekana hakuzingatia kuwa chuki kubwa dhidi ya NRM katika baadhi ya maeneo si kwa sababu ya umaskini pekee, bali pia ni matokeo ya adhabu bila uwajibikaji na kufungwa kwa wafuasi wa upinzani.

Mwishowe, yeyote atakayetangazwa mshindi mwishoni mwa wiki hii hatakuwa chaguo bora kwa mlima wa matatizo magumu yanayoikabili Uganda leo. Huenda suluhu ya changamoto hizi ikahitaji zaidi ya Serikali ijayo pekee.

Katika kipindi cha kampeni, mikutano ya Bobi Wine na NUP imekuwa ikikumbana na vyombo vya dola ambapo inapigwa mabomu ya machozi kuwatawanya wananchi, jambo ambalo linaongeza hofu siyo tu kwa wananchi, bali pia viongozi wa chama hicho.

“Kila siku kuna sababu 99 zinazotufanya tuachane na mapambano kwa sababu ni hatari,” anasema Bobi Wine. “Lakini kuna sababu moja kubwa ya kuwa jasiri — upendo, hamasa, uungwaji mkono na mshikamano.”

Hofu kuhusu usalama wake, imechochewa na vitisho vya mara kwa mara kutoka kwa mtoto wa Rais na Mkuu wa Majeshi, Muhoozi Kainerugaba. Katika chapisho moja kwenye mitandao ya kijamii, Kainerugaba alipendekeza kuwa angeweza “kukata kichwa” cha Bobi Wine kama angeruhusiwa — kauli iliyokosolewa vikali kimataifa.

Mmoja wa walinzi wa Bobi Wine baadaye alionekana mahakamani akiwa hawezi kutembea bila msaada, ni ishara ya wazi ya mateso baada ya kuripotiwa kupotea. Kwa Wine, ujumbe ni wazi.

“Huyu si mtu wa kawaida,” anasema. “Anaongoza jeshi, polisi, magereza… yuko juu ya sheria.”

Hata hivyo, ukandamizaji haujapunguza dhamira ya harakati hizo. Wine mara nyingi hujitaja kama “rais wa gheto,” akisisitiza mizizi yake na uhusiano wake na Waganda wa kawaida wanaopambana na ukosefu wa ajira na gharama za maisha za juu.