Musoma. Wakati Joyce (siyo jina halisi) akikumbuka uamuzi alioufanya akiwa na miaka 15, anasema ulikuwa mgumu na wenye ujasiri wa kipekee katika maisha yake.
Akikabiliwa na hatari ya ukeketaji na ndoa ya kulazimishwa, alikimbia nyumbani, akipinga mipango ya familia na desturi zilizokuwa zimeharibu maisha ya dada yake.
Joyce alizungumza na Mwananchi Desemba, 2025 ilipofanya ziara katika wilaya za Butiama, Musoma, Tarime na Serengeti, mkoani Mara, kuchunguza kuhusu madai ya uwepo wa bi
Gazeti la Mwananchi limefanya uchunguzi kwa miezi mitatu Kanda ya Ziwa kuhusu uwepo kwa biashara ya viungo vya sehemu za siri za mwanamke baada ya kukeketwa.
Anasema akiwa mzaliwa katika Kabila la Kikurya, alilazimika kukimbia nyumbani kwao kukwepa kukeketwa.
Akizungumza kwa sauti ya chini anasema: “Wazazi wangu walikuwa wameazimia nikeketwe ili niolewe, wafaidike na mahari.”
Anaeleza kila kitu kilikuwa kimeandaliwa; mialiko imetolewa, nguo na viatu vimenunuliwa na wageni wamealikwa.
“Nilipewa hata upande wa kitenge nitakachovaa. Hakukuwa na majadiliano, ilikuwa lazima,” anasema.
Kilichobadilisha maisha ya Joyce ni kupata taarifa sahihi shuleni, ambako alihudhuria vipindi vya uhamasishaji vilivyoandaliwa na Hope for Girls and Women Tanzania.
Hili ni shirika lisilo la kiserikali linalohamasisha wasichana na wanawake kukabiliana na ukatili, ukiwamo ukeketaji.
“Walituambia hatari za kiafya na madhara ya maisha baada ya kukeketwa. Nilijua siwezi kukubali,” anasema.
Wakati maandalizi ya sherehe yakiendelea, Joyce aliamua kuondoka nyumbani na kutafuta hifadhi nyumba salama ya shirika hilo.
“Haukuwa uamuzi rahisi, nilijua kutakuwa na matokeo hasi,” anasema.
Matokeo hayo yalikuja kwa haraka na maumivu, kwani mdogo wake alilazimishwa kukeketwa badala yake.
“Walipogundua nimekimbia, walisema lazima mtu mwingine azibe nafasi yangu. Mdogo wangu alikeketwa bila ridhaa yake, baadaye aliacha shule na kuolewa,” anaeleza akikumbuka yaliyotokea.
Joyce anasema alipelekwa nyumba salama Mugumu, ambako alikaribishwa na walezi, akiwamo mwanamke anayemtambulisha kama mama Rhobi.
Hayo yakitokea alikuwa kidato cha kwanza. Anasema aliendelea na masomo katika Shule ya Sekondari Mugumu, wilayani Serengeti na akahitimu kidato cha nne.
Kwa msaada na udhamini wa shirika hilo, aliendelea na kozi ya usimamizi wa hoteli na huduma za watalii.
Baada ya kuhitimu, alipata ajira katika sekta ya utalii na sasa anafanya kazi Serengeti kama mtaalamu na mwongoza watalii.
“Nilikimbia mwaka 2017 nilipokuwa na umri wa miaka 15. Leo ninafanya kazi, nina uhuru na ninajitegemea,” anasema.
Joyce anatoka katika familia ya wasichana sita; wawili tu, dada yake mkubwa na mdogo wake, ndio waliokeketwa baada ya yeye kukimbia.
Ndugu zake wengine walisalimika, mabadiliko anayoyaelezea kuwa ni matokeo ya hatua alizochukua na elimu aliyoitoa baadaye kwa wazazi wake.
“Mwanzoni wazazi wangu walinikataa. Walisema hawawezi kuishi na binti ambaye hajakeketwa. Lakini baada ya kumaliza masomo yangu na kupata kazi, mambo yamebadilika,” anasema.
Baada ya msaada wa walezi wa nyumba salama, Joyce alirudi nyumbani kuzungumza na wazazi wake.
“Tulianza kuwaelimisha. Sasa wameona kuwa ukeketaji hauna faida. Mara nyingi binti hupoteza hamu ya shule na hukimbilia kuolewa mapema, hivyo kuanza kukabiliana na ugumu wa maisha katika umri mdogo,” anasema.
Uzoefu wa mdogo wake anasema umekuwa kielelezo cha maumivu.
“Baada ya kukeketwa, alikataa kuendelea na shule na kuolewa. Amekuwa katika hali ngumu ya maisha,” anasema na kuongeza:
“Wazazi wangu sasa wameona tofauti kati ya binti aliyefanikiwa baada ya kukimbia kukeketwa na aliyeshidwa kuendelea na masomo baada ya kukeketwa.”
Anasema: “Hivi sasa hakuna shinikizo kwa wasichana wadogo katika familia yetu. Mdogo wangu mmoja yuko kidato cha pili, wengine wawili bado wapo shule ya msingi.”
Joyce anasimulia: “Wazazi wangu sasa wameapa kutolazimisha mtoto kukeketwa na kwamba chaguo litabaki kuwa lake. Hapo awali, hakukuwa na mjadala, ilikuwa lazima msichana akeketwe. Wazazi sasa wameelewa.”
Anaamini simulizi yake itahamasisha wasichana wengine walioko hatarini kutafuta na kupata msaada.
“Nataka wajue inawezekana kukataa kufanyiwa ukatili huo. Elimu na msaada vinaweza kubadilisha kila kitu katika maisha ya msichana,” anasema.
Kwa upande wake, Jamila (si jina halisi) mwenye miaka 25, anasimulia hadithi yake ya ujasiri.
Anasema aliazimia kutokeketwa baada ya kuona madhara waliyoyapata dada zake wawili.
“Wakati maandalizi yakifanyika kwa ajili yangu, nilikuwa nimeazimia kuwa kamwe sitapitia njia waliyopita dada zangu,” anasema.
Akiwa na umri wa miaka 12, alitafuta msaada kwa mwalimu wake.
“Nilieleza kila kilichokuwa kikiendelea. Aliahidi kunisaidia lakini aliniambia kwa wakati ule nirejee nyumbani,” anaeleza.
Maandalizi yote yalikuwa yamekamilika. Ingawa mama yake alikataa ukeketaji kwa kuelewa madhara yake, hakuweza kupinga uamuzi wa familia, hasa wanaume.
Siku moja kabla ya sherehe, Jamila alirudi kwa mwalimu wake. “Nilimwambia maandalizi yamekamilika kwa ajili ya kukeketwa kesho yake. Ilikuwa tukeketwe mimi na binamu yangu, kama ilivyo desturi,” anasema na kueleza mwalimu aliingilia kati mara moja.
“Aliniambia nisirudi nyumbani siku hiyo. Nilibaki nyumbani kwake huku akiendelea kunitafutia msaada,” anasema.
Anaeleza baadaye gari liliwasili nyumbani kwake, akachukuliwa na kupelekwa polisi kisha nyumba salama ya Shirika la Hope.
Jamila anasema wakati huo alikuwa na miaka 12. Katika familia ya wasichana watatu, wawili walikeketwa na yeye ndiye pekee alisalimika baada ya kukimbia.
“Polisi walihakikisha usalama wangu kabla ya kupelekwa Serengeti,” anasema na kubainisha kuwa akiwa huko maisha yake yalichukua mwelekeo tofauti.
Anasema alipata fursa ya kuendelea na masomo akahitimu kidato cha nne na baadaye kidato cha sita akapata ufaulu wa daraja la kwanza.
Alijiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) ambako alisoma Shahada ya Sanaa na Usimamizi wa Sheria, akahitimu mwaka 2024.
Anasema amefanya kazi katika sekta ya sheria, akijitolea katika mashirika ya utetezi, akijifunza masuala ya haki na usawa.
Sasa anajihusisha na masuala ya uongozi na utetezi, baadhi zikifanyika mtandaoni, zikilenga uwezeshaji na uhamasishaji.
Ndugu zake waliokeketwa bado wapo nyumbani, mmoja ameolewa na mwingine anaendelea na maisha yake.
“Najua maisha yangu yangekuwa tofauti kama nisingekimbia ukeketaji,” anasema.
Anatoa ujumbe akisema: “Wazazi lazima waheshimu na kulinda haki za watoto wa kike. Desturi nyingi hatarishi zinaendelea kwa sababu wasichana hawana chaguo.”
“Kama binti anataka elimu, anapaswa kuungwa mkono. Wasichana wana ndoto, malengo na uwezo na wanastahili kulindwa, kupewa nguvu na nafasi ya kutengeneza maisha yao,” anasema.
“Kungekuwa na nyumba salama, nisingekeketwa. Sikuwa na mahali pa kukimbilia, ndiyo maana nilifanyiwa ukatili huu.”
Hayo ni maneno ya Rhobi Samwelly, yanayoonesha maumivu ya utoto wake, yaliyosababishwa na desturi hatari ya kitamaduni ambayo hakuikubali.
Wazazi wake walipogundua wakati wake wa kukeketwa umewadia, hakuwa na uwezo wa kujikinga au kupata msaada wowote kutoka kwa jamii, akalazimika kubaki bila ulinzi.
Miaka kadhaa baadaye, aligundua kutokuwapo kwa nyumba salama ndiyo sababu kuu inayosababisha wasichana wengi kulazimishwa na hatimaye kukeketwa.
Akizungumza na Mwananchi anasema ili kuwalinda, alianzisha Shirika la Hope for Girls and Women Tanzania mwaka 2017.
Anasema shirika hilo limeokoa na kuwalinda wasichana 3,757 na kwamba, kati ya Novemba na Desemba, 2025 zaidi ya wasichana 200 waliokolewa na kufanya idadi ya wasichana waliookolewa kufikia takribani 4,000.
Samwelly anasema uzoefu wake binafsi unaendelea kuwa kichocheo cha kujitolea kwake.
Hata hivyo, anataja changamoto kubwa anayokabiliana nayo ni ukosefu wa gari la kuaminika kwa ajili ya kuitikia taarifa zinazowasilishwa kwa dharura, kukosekana kwa uhakika wa chakula na nguo kwa wasichana waliokimbia.
“Tunapopokea taarifa, lazima tuchukue hatua mara moja,” anasema.
Licha ya vikwazo, anasema mradi wa kukabiliana na ukeketaji unabaki na nyumba salama zitabaki kuwa suluhisho kwa wasichana walio hatarini.
Kwa sasa anasimamia nyumba mbili salama zilizoko Serengeti na Butiama na kwamba, dhamira yake ni kupanua mpango huo katika wilaya zingine za Mkoa wa Mara na maeneo mengine ya Tanzania.
“Nawaalika wadau kuunga mkono juhudi hizi za kukomesha mila hizi potofu ndani ya jamii yetu,” anasema.