Utamaduni wa Watanzania unayachukulia mambo mazito kwa wepesi. Hii ni tiba ya kimwili na kiakili kwani ukisikia “polepole ndio mwendo”, “haraka haraka haina baraka”, “aliye juu mngoje chini” na mingine yenye mrengo huo, unaweza kuwa salama kuliko mtu mwenye pupa. Mwendapole hajikwai, na akijikwaa haanguki. Na haya yakishakaa akilini, yanaishi ndani ya mtu bila kujali kuwa anahitaji usafiri wa mwendokasi au treni ya SGR.
Mambo yanapokuwa magumu, kuna namna watu kuyaacha yapite. Hii ni fomula muhimu maishani na kila jamii ina msemo wake unayoibeba dhana hiyo. Waswahili tunasema “funika kombe mwanaharamu apite”, akishapita mambo yanaendelea kama kawaida. Ni suala la subira tu ili kuepusha shari inayoweza kujitokeza. Na kwa bahati nzuri, subira hii haigharimu chochote zaidi ya kuleta kheri.
Pamoja na kwamba kila kada huvuta subira ili kufanikiwa, lakini kila moja ina namna zake. Wapigana vita huweza kumwacha adui ashambulie hadi akadhani kuwa ameshinda, kisha humshtukiza na kummaliza kabisa. Kwenye mpira wa miguu kuna mbinu inayoitwa “counter attack”. Hapa adui zenu wanawaruhusu muingie upande wao kuwashambulia, kisha wanawashtukiza na kuwafunga goli la ghafla.
Kwenye mchezo wa ndondi, ngumi za usoni ndizo zinazoongoza kwa alama. Bondia hasimu wako anaweza kukuletea uso usiokingwa mbele yako kama aliyejisahau. Unapojaribu kumshambulia kwa nia ya kuchukua pointi, atakukwepa. Na kwa sababu ameshakusogelea vya kutosha, anakupa shambulizi la ghafla na kukuangusha. Wenyewe wanaita mbinu hii “kuuza sura”. Haina tofauti na counter attack.
Lakini utulivu unaleta tija iwapo utatumiwa kwa faida ya wote. Wapo ambao wanamsubirisha mhitaji, ambaye atalazimika kusubiri jambo lisilokuwepo. Usione ajabu pale anapouliza maswali ya msingi na kurudishiwa majibu ya chapuo. Nasikia kiongozi mmoja alibanwa na swali zito kutoka kwa mwandishi, akajibu “no comment”. Cha kushangaza alisikika akilijibu alipohudhuria mahafali ya mwanaye.
Subira yenye tija kwa msaburi ndiyo inayoleta matokeo mazuri kwenye jamii yoyote. Si lazima watu wapate chakula au pesa baada ya subira yao, lakini hata elimu ya namna ya kuwafanyia wenzao. Kwa mfano siku makocha wawili wa timu hasimu za ligi ya Uingereza, walipoketi pamoja wakati timu zao zikichuana. Mmoja wao aliyejulikana kwa majigambo, alimnyima pumzi mwenzake tangu mwanzoni.
Alimshambulia kwa maneno mfululizo, lakini mwenzake alibaki kimya muda wote. Timu ya kocha mtulivu ikapata bao la kwanza, lakini hata alipoulizwa alijisikiaje baada ya kuzogomwa na kocha mwenzake, bado alibaki kimya. Kocha mjivuni alipunguza maneno baada ya kufungwa, lakini akapigwa bao la pili na mpira ukaisha. Yule mkimya alipoulizwa na waandishi kwa nini hakusema lolote, alijibu, “wakati mwingine ukimya ni silaha tosha”.
“Mvumilivu hula mbivu”. Mtu hutegemea mambo mazuri baada ya kuteseka. Hata yawe mateso ya muda mrefu, akishajua hatma yake ni kula kivulini haimpi shida. Mara nyingi imani yake inakwenda kwa viongozi wake. Imeandikwa kwamba mambo ya duniani yanaakisi ya mbinguni. Hilo linamwongezea utiifu kwa Serikali yake, na atafanya yale tu anayoyasikia kutoka kwa viongozi.
Kwa bahati mbaya mpaka sasa wapo watu wanaofanya siasa kwa lengo la kupata uongozi, lakini wakishaupata wanautumia kujinufaisha wenyewe. Hatuvilaumu vyama kwani vina sera, miongozo na kanuni zinazopingana na wanasiasa uchwara. Hapa tuna jambo na wanasiasa, wao kama wao. Haijalishi walizaliwa humo, walikulia au walirithi kutoka kwa babu zao. Hii inawahusu hata waliotoka uhasimuni na “kurudi nyumbani”.
Wanasiasa huweza kubadilika kwa namna ya kipekee. Ni mwanasiasa tu ndiye mwenye kawaida ya “kufa zaidi ya mara moja”. Anaweza akafia kwenye chama cha upinzani na kufufukia chama tawala. Nina maana anaweza akakumbwa na kashfa za matumizi mabaya ya cheo na ubadhilifu kwenye kambi yake, akafukuzwa na kuibukia kwenye chama tofauti. Huko akaoshwa vizuri na kunadiwa kuwa kiongozi bora.
Wakati mwingine anaweza kuvaa joho la Mwanamapinduzi. Yeyote anayepingana na katiba kandamizi na kudai haki za wananchi ni mhaini wa katiba ile. Lakini akifanikiwa kuwakomboa wananchi dhidi ya katiba hiyo, ataitwa mkombozi. Mandela hakupigania uhuru maana nchi yake ilishakuwa huru. Alichokuwa akipigania ni haki na usawa, kitu ambacho kilimpelekea Nyerere kuanzisha Azimio la Arusha.
Mwanasiasa anaweza kufa kisiasa kwenye chama kimoja, akahamia chama kingine atokakobatizwa upya. Lakini kiongozi anaubeba msalaba mzito kwani anaowaongoza ni wake na wasio wake. Hapana nitakosea nikisema hivyo: Kiongozi anawaongoza waliomtunuku na hata wale waliomkataa. Ni kwa sababu ukikabidhiwa bwawa la samaki ni lazima ukute majani kwa mfano wa taka. Uliyaondoa hayo unawakosa na samaki wenyewe.
Hivi sasa tunao wanasiasa wa zama hizi. Wengine wana siasa za kimtandao, sio zile za Chuo cha Kigamboni. Usishangae huyu atazipinga sera za chama kwa kuwa msimamo wake ni “Mtaji wa chama ni raslimali watu”. Na kweli akakubalika na kuongeza mashabiki kwenye chama kinachombeba. Lakini huyu ndiye mtakayemuengua kwa ukosefu wa maadilili, akaja kutukuzwa upande wa pili. Halafu si ajabu akapata kashfa huko nanyi mkamsafisha. Nina wasiwasi sana na maendeleo yetu.
