Nusu ya kwanza ya Karne ya 20, dunia ilipoteza watu zaidi ya milioni 101 kwa sababu ya vita. Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia (WW1), waliuawa watu milioni 17. Vita ya Pili ya Dunia (WW2), walipoteza maisha zaidi ya watu milioni 84.
Baada ya mapigano ya miaka saba mfululizo, nchi zikiwa zimeharibiwa na vita, vifo vya mamilioni ya watu vikiacha simanzi ya dunia, wawakilishi wa mataifa 50 walikutana San Francisco, California, Marekani, kujadili amani. Hakuna kilichohitajika duniani kama amani. Athari za WW2 zilikuwa hazipimiki.
Aprili 25 hadi Juni 26, 1945, zilikuwa siku 62 za msako wa amani. Kila uso wa mwakilishi, miongoni mwa wawakilishi 50, ulipambwa na tabasamu wakati mkataba wa Umoja wa Mataifa (UN), uliposainiwa Juni 26, 1945. Matumaini yaliyokuwepo ni kwamba uundwaji wa UN, ungeondoa uwezekano wa vita nyingine kutokea.
Wajumbe wale wa mataifa 50 hawakujua kuwa walikosea mno kufanya makubaliano ya kuunda Umoja wa Mataifa kwenye ardhi ya Marekani. Kosa lingine kubwa ni kuifanya New York, Marekani, kuwa makao makuu ya UN.
Haikutimia miezi miwili tangu kusainiwa kwa mkataba wa UN, Marekani ilifanya mashambulizi mawili ya nyuklia, Agosti 6 na 9, 1945, kwenye miji ya Hiroshima na Nagasaki. Watu takriban 246,000 walipoteza maisha.
Jambo moja linaweza kuwa sahihi. Mataifa ya Ulaya yaliyopata athari kubwa ya vita, yangeweza kuwa mabalozi wazuri wa amani. Marekani haikuathirika na vita. Badala yake ilinufaika. Uchumi wa Marekani ulikua kipindi cha WW2, mzunguko wa kibiashara ulikuwa mkubwa, na ajira nyingi zilipatikana.
Ni ujumbe kuwa Marekani ni wafanyabiashara kupitia vita. Unaweza vipi kukabidhi dhamana ya utunzaji amani kwa mtu anayetajirika vitani? Je, ni hadithi ya mchawi mpe mwanao akulelee? Imepita miaka 80 na zaidi ya miezi miwili, tangu UN izaliwe, Oktoba 24, 1945, Marekani bado inaitikisa dunia kwa ushari.
Nchi ni huru, sheria za kimataifa zipo, pamoja na hivyo, mabadiliko ya uongozi wa mataifa mbalimbali duniani, yanajadiliwa Langley, Virginia, Marekani, yalipo makao makuu ya Shirika Marekani la ujasusi wa kimataifa (CIA). Majasusi wa CIA, wamezagaa ulimwenguni, wakichunguza nchi nyingine na kuingilia utawala.
Marekani hawatulii ili kila nchi ifanye mambo yake, inahakikisha inatengeneza masilahi yake kwenye mataifa mengine. Nchi zenye utawala ambao hauendani na masilahi ya Marekani, inakuwa kwenye hatari.
Uvamizi wa Bay of Pigs hausahauliki. Kikosi kilichotengenezwa na CIA, kilichoitwa Brigedi 2506, kiliingia Cuba kumpindua aliyekuwa kiongozi wa nchi hiyo, Fidel Castro, Aprili 17, 1961. Wanajeshi wa Marekani walilazimishwa kusalimu amri ndani ya siku tatu tangu kuanza kwa mapigano.
Korea lilikuwa taifa moja kabla ya Vita Kuu ya Pili ya Dunia. Na ilikuwa koloni la Japan. Baada ya Japan kudhoofishwa na pigo la nyuklia katika miji ya Nagasaki na Hiroshima, lililopigwa na Marekani, Korea iligawanywa. Marekani walichukua Kusini na Urusi Kaskazini. Na hiyo ndio ikawa sababu ya kuundwa kwa nchi mbili, Korea Kaskazini na Korea Kusini.
Mwanzo wa Vita ya Korea ni Marekani kuitangaza Korea Kaskazini kuwa iliivamia Korea Kusini, hivyo mapambano yalianza. Awali ilionekana kama Marekani isingetumia msuli mkubwa kuikabili Korea Kaskazini. Hata hivyo, Marekani ikiwa imeweka kambi ya vita ambayo hufahamika kama Chosin Reservoir Campaign, Novemba 27, 1950, ilishambuliwa kwa kushitukizwa na China, hivyo mapigano makali yalitokea.
China iliamua kuishambulia Marekani ili kuudhoofisha mpango wake wa kuipiga Korea Kaskazini. Mapambano hayo ambayo yalidumu kwa siku 16 kati ya China na Marekani, huitwa Battle of Chosin Reservoir. Yalianza Novemba 27 mpaka Desemba 13, 1950.
Mwaka 1955 Marekani waliamua kujitosa kwenye Vita ya Vietnam, iliyokuwa inahusisha makundi ya itikadi hasimu, Ubepari na Ukomumisti. Marekani waliingia kusaidia kundi lililokuwa na mrengo wa Ubepari. Moto uliowaka haukuwa mdogo. Vita ilipiganwa miaka 20 mfululizo.
Fuatilia mfululizo wa vipindi vya televisheni vya Homeland. Jinsi CIA wanavyochakata ushawishi wao duniani wakiwa Langley, inaweza kukusaidia kuona ni kwa nini Rais wa Marekani, Donald Trump, ameivamia Venezuela, kisha anapanga mgawanyo wa mafuta ya nchi hiyo.
Ni Marekani iliyoivamia Iraq mwaka 2003 na kumwondoa madarakani aliyekuwa kiongozi wa nchi hiyo, Saddam Hussein. Miaka 23 inakwenda kutimia, Iraq inaendelea kumwaga damu. Marekani imeharibu nchi ya watu. Iraq imekuwa maskani ya vikundi vya ugaidi.
Marekani walitaka na wakafanikiwa kumpindua aliyekuwa Kiongozi wa Libya, Muammar Gaddafi. Ilikuwa mwaka 2011. Miaka 15 inakwenda kukamilika bila Libya kuwa na amani. Imekuwa maskani ya biashara ya utumwa na vikundi vya watu wenye silaha, kila kimoja kujinasibu kuongoza dola. Wananchi wapo kwenye mateso.
Ni aibu kwa nchi ambayo inaongoza kwa chokochoko za kiulimwengu, ndiyo iwe mwenyeji wa umoja ulioanzishwa kwa ajili ya kutokomeza vita duniani. Ilivamia nchi na kubadili viongozi kabla UN haijazaliwa, na inaendelea Umoja wa Taifa ukiwa hai.
Marekani ilimwingiza madarakani, Emilio Aguinaldo, Ufilipino, kisha ikamwondoa Aprili 19, 1901, baada ya kuona hatekelezi masilahi yao. Ni hivyohivyo, walimpindua Salvador Allende, Chile, na kumsimika Augusto Pinochet, halafu wakamwondoa Pinochet, alipokiuka matakwa yao. Haina tofauti na Manuel Noriega, Panama, na Nicolas Maduro, Venezuela.
UN imekuwa jumuiya isiyo na meno. Marekani inafanya inavyotaka popote duniani. Marekani inataka Wapalestina wauawe bila kujitetea, Wamarekani wanasema Israel wanajilinda. Watoto na raia wasio na hatia wanapigwa mabomu wakiwa hospitalini na shuleni Palestina, utetezi ni kuwa wanatafutwa Hamas, kwamba ni kikundi cha kigaidi.
Maandamano makubwa Iran, Marekani inatuhumiwa kuhusika na uratibu. Kisha, Marekani wanataka kukitwaa kisiwa cha Greenland ili kunufaika na madini adimu, uranium na chuma. Dhahiri, Marekani inapenda vita na inaendekeza ubabe. New York haistahili kuwq makao makuu ya UN.
