Tamisemi: Halmashauri hizi ziandae uchaguzi mdogo wa mitaa

Dar es Salaam. Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) imezitaka halmashauri nchini kuandaa na kusimamia uchaguzi mdogo wa serikali za mitaa.

Halmashauri hizo ni zile ambazo wenyeviti wake wa mitaa waligombea na kushinda kuwa madiwani kwenye uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, 2025.

Miongoni mwa mitaa hiyo ni ule wa Kumba, ambao mwenyekiti wake, Frank Msimbe aliyeshinda kiti hicho kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa wa mwaka 2024 na kuchaguliwa kuwa diwani wa Msangani, katika Halmashauri ya Kibaha kwenye uchaguzi mkuu wa 2025.

Kwa mujibu wa Sheria ya Serikali za Mitaa (Mamlaka za Miji), Sura ya 288 (Revised Edition 2002) Kifungu cha 60(2) mwenyekiti wa serikali ya mtaa hawezi kuwa diwani kwa wakati mmoja.

Sheria hiyo inaeleza, mwenyekiti wa mtaa akichaguliwa kuwa diwani, Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) au Tamisemi inapothibitisha, anafutwa kuwa mwenyekiti wa mtaa mara moja kwa mujibu wa Kanuni ya 8(1)(c) ya G.N. No. 283/2019 na kifungu cha 60(2) cha Cap. 288, mtu anayeshika nafasi ya kuchaguliwa ya ngazi ya juu (udiwani) anapoteza sifa ya kuendelea na nafasi ya chini (mtaa).

Hata hivyo, katika baadhi ya mitaa, wapo waliokuwa wenyeviti ambao sasa ni madiwani wanaendelea kutumika kwenye nafasi zote mbili kwa wakati mmoja.

Akizungumza na Mwananchi Jumatatu ya Januari 12, 2026,  Katibu Mkuu wa Tamisemi, Adolf Ndunguru amesema kila aliyekuwa mwenyekiti wa serikali ya mtaa na kwenye uchaguzi uliopita akashinda udiwani anapaswa kujiuzulu uenyekiti na halmashauri ya eneo husika mara moja.

Amesema halmashauri ya mtaa husika inapaswa kuitisha na kusimamia uchaguzi mdogo ili kupata mwenyekiti mpya na si yule wa awali kuendelea na majukumu yote mawili kwa wakati mmoja.

“Sheria hairuhusu kuwa mwenyekiti hapohapo ni diwani, kwa kuwa hizo ni chaguzi ndogo, halmashauri za mitaa husika zinatakiwa kuitisha uchaguzi mdogo wa mtaa huo kwa utaratibu uleule wa uchaguzi ili kupata mwenyekiti wa mtaa,” amesema.