Mwaka 2025 ulikuwa mzuri kwa Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma) ambacho kilipata nguvu mpya baada ya wanachama wapya kutoka Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kujiunga na chama hicho.
Kundi la wafuasi hao wa Chadema lilikipa uhai mpya Chaumma hasa baada ya baadhi yao kupewa nafasi za juu katika uongozi wa chama hicho na hivyo kukiweka katika ramani ya kisiasa huku kikitabiriwa kutoa ushindani mkali kisiasa.
Hata hivyo, tangu kufanyika kwa uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, 2025, chama hicho kimekuwa kimya, viongoni wake hawaonekani hadharani kwa shughuli za kisiasa wala kutoa kauli au matamko ya kisiasa juu ya mambo yaliyotokea nchini.
Kimya hiki kimeibua mjadala mtandaoni ambapo wadau mbalimbali wa wanasiasa wakiuliza “Chaumma iko wapi?” Wengine wanadai makada waliotoka Chadema na kujiunga na chama hicho kipya hawana raha ndani ya chama hicho na wanatamani kurudi Chadema.
Uongozi wa Chaumma umetupilia mbali hisia tofauti za wadau huku kikidai kwamba kimejifungia kupanga mikakati kabambe na kitakaporejea kitarudi na nguvu kubwa tofauti na kilipoanza mwaka jana.
Naibu Katibu Mkuu wa Chaumma Bara, Benson Kigaila, mmoja wa vigogo waliotoka Chadema, anasisitiza kwamba madai ya kuwa chama kipo kimya ni kujidanganya, akisema wanaofikiri hivyo wasubiri waone harakati za chama hicho baada ya mikakati kukamilika.
“Tunaendelea na mipango yetu, tutakapokuja hadharani watajua ajenda zetu, wao waendelee kusema hivyo ila sisi tunajua nini tunafanya na chama chetu ni imara zaidi ya jana na kipo hai zaidi mwaka huu,” anasema.
Anaongeza kuwa chama kina amani na makada wake wanafuraha ndani na kwamba kimejifungia kikifanya mikakati yake na kikimaliza vikao vya ndani vya mkakati kitarudi uwanjani kuweka wazi ajenda zake.
“Sisi tupo, tuna amani na furaha mioyoni mwetu kuwa ndani ya chama hiki. Wale wanaosema hatuna amani na chama chetu wasubiri tumalize vikao vyetu vya ndani,” anasema Kigaila, akisisitiza kwamba chama kinaendeshwa kwa mikakati thabiti na si kwa kupima upepo.
Chaumma kilivuna mamia ya wanachama kutoka Chadema, baadhi yao wakapewa nyadhifa kwenye chama chao kipya, wakiwa na matumaini ya kuunda chama chenye mwelekeo mpya wa kisiasa, hata hivyo, baadhi wameonyesha hisia zao zimegawanyika.
Mwananchi limefanya mahojiano na baadhi ya makada hao ambapo wanabainisha mitazamo tofauti miongoni mwao wakati baadhi yao wakionyesha kufurahishwa na mwenendo wa Chaumma, baadhi wanaonekana kukata tamaa na kutamani kujiondoa kwenye chama hicho.
Dorcus Francis, aliyekuwa mgombea ubunge katika jimbo la Kawe jijini Dr es Salaam, anaonyesha imani yake kwa chama hicho kipya, akisisitiza kuwa hana mpango wa kurudi Chadema wala kukihama chama hicho.
“Mimi sina mpango wa kurudi Chadema. Mimi ni mwanasiasa na mwanadiplomasia na mwelekeo wangu wa siasa nje ya Chadema ni mzuri sana. Na mambo mazuri sana na makubwa kabisa yanakuja kwenye safari yangu ya kisiasa kuelekea 2030,” anasema na kuongeza:
“Suala siyo najisikiaje kuwa Chaumma au chama chochote. Mimi nimejifunza sio najisikiaje, bali naleta impact (athari gani) gani kwenye jamii yangu iwepo katika jukwaa lolote la siasa,” anasema kada huyo.
Kwa Dorcus, chama si kigezo, bali nafsi yake binafsi na uwezo wake wa kuleta mabadiliko ndio msingi wa imani yake.
Wakiwa na mtazamo tofauti na Dorcus, wapo pia makada ambao wanaona Chaumma kimekosa mwelekeo wa kutimiza ajenda yake kisiasa wakidokeza kuhama chama hicho kutafuta chama kitakachosaiduia kutimiza ndoto zao.
Masanja Katambi, aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Magharibi, anaeleza kutoridhishwa na siasa za ndani ya Chaumma na kuonyesha kuwa anaweza kuachana na chama hicho wakati wowote.
“Nataka kutoka. Hakuna amani ya moyo. Viongozi wakuu thinking capacity (uwezo wa kufikiri) ni tofauti na yangu,” anasema.
Anaongeza kuwa: “Chaumma wana prove wrong (wanakosea) kwa hilo, lakini kwa Chadema mimi siwaoni nao kama wana mkakati wa kuunganisha watu kuitoa CCM, hawana viongozi wa kuwaongoza kwenye ukombozi,” anasema.
Katambi anaona kukosekana kwa mikakati mahsusi kunamfanya kufikiri kutafuta jukwaa jingine la kisiasa ili kutimiza malengo yake.
Wataalamu wa sayansi ya siasa wanasema chama cha siasa kinapaswa kuwa na mpango kazi wa mwaka mzima ili kubaki na shughuli za kufanya kwenye jamii, wakitahadharisha kuwa kukosekana kwa mpango wa mwaka.
Wanasema chama kinaweza kuwa cha misimu na hivyo kuibuka wakati wa uchaguzi na kupotea mara uchaguzi unapopita kwa kukosa kazi ya kufanya nje ya kampeni za uchaguzi.
Mtaalamu wa sayansi ya siasa wa Chuo Kikuu cha Zanzibar (Suza), Profesa Mohamed Makame anasema uhai wa chama cha siasa unatokana na shughuli ambazo chama kinafanya, akionya kuwa chama kukosa majukumu ya kufanya ni ishara ya uongozi dhaifu.
“Chama cha siasa kinapaswa kuwa na mpango kazi wa mwaka mzima wa majukumu ya kufanya, tofauti na hapo chama kisipojiwekea mpango kazi wa mwaka mzima hakiwezi kuwa taasisi imara, hivyo hakitaweza kuwa na kazi ya kufanya wakati usio wa uchaguzi,” anasema.
Kwa upande wake, mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Udsm), Dk Sabatho Nyamsenda anasema ni haki kwa kila mtu kuanzisha na kujiunga au kuhama chama cha siasa akitaja kuwa kusuasua kwa vyama vya siasa kuashiria udhaifu wa uongozi ndani ya chama na kuathiri ukuaji wachama husika.
Kuhusu Chaumma, anasema chama hicho kiliibuka na kuwa na ushawishi baada ya kupokea vigogo waliohama kutoka Chadema, hata hivyo kimya chao baada ya uchaguzi kinatoa tafsiri nyingi na swali kuhusu mustakhabali wake na mshikamano wake.
“Vigogo waliotoka Chadema kwenda Chaumma walitumia haki yao kikatiba, hata hivyo kimya chao kinatoa maswali mengi, yakiwemo uhaba wa fedha za kuendeshea shughuli za chama au kukosa matumaini ya matarajio waliyokuwa nayo wakati wakijiunga nacho,” anasema.
Anasema kimya kilichotawala Chaumma baada ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, 2025 unaweza kuwa na athari chanya na hasi kwa maendeleo ya siasa nchini, akisema Chaumma kwa upande wake inaweza kuathirika vibaya.
Dk Nyamsenda anasema kuibuka na kunyamaza kwa chama hicho kunaweza kuvunja mioyo wafuasi wake na wale waliokuwa na matumaini mapya na chama hivyo na hivyo kuathiri ukuaji na ushawishi wa chama hicho.
Kwa upande wa athari chanya, Dk Nyamsenda anasema hali hiyo inaweza kuwa fursa kwa chama walichokihama Chadema, ambacho kilikuwa mwathirika wa kuwapoteza makada wake waliokuwa viongozi wakuu waliokipigania chama katika mapito yenye historia ndefu.
“Kwa Chaumma kukaa kimya jumla kunatoa hatari ya kupotea kwa chama hicho kwani wafuasi wao watapoteza matumaini na hivyo kudhorota kwa chama hicho na shughuli zake kwa umma,” anasema.
