Simba yafuata straika Uganda | Mwanaspoti

UNAPOSOMA habari hii tambua kwamba Simba haijalala kwenye usajili na inafanya hesabu zake kubwa kimyakimya, hivi sasa ikiwa imejifungia ikimpigia hesabu mshambuliaji mmoja anayejua kufunga kutoka Uganda.

Simba inafanya mazungumzo na mshambuliaji raia wa DR Congo, Bedia Ikamba, anayekipiga Polisi ya Uganda ambaye ameonyesha ubora katika kufunga mabao pengine zaidi ya Mganda Steven Mukwala Msimbazi zikiwa ni siku chache tangu Yanga ilipokamilisha dili la kiungo Allan Okello kutoka Vipers ya nchini humo.

Taarifa kutoka Uganda ni kwamba bosi mmoja wa juu wa Simba ndiye anayezungumza na Ikamba ambapo sasa faili la mshambuliaji huyo limepelekwa kwa kocha Steven Barker akisubiriwa kutoa majibu ya mwisho.

Ikamba mpaka sasa ndiye anayeongoza kwa ufungaji katika Ligi Kuu Uganda, akifunga mabao sita, akilingana na wenzake wawili Patrick Kadu wa Kitara FC na Muhammad Ssenoga (Express) waliofunga idadi kama hiyo.

“Kuna huyo mshambuliaji Simba inazungumza naye sijajua kama wameshamalizana lakini ni mshambuliaji mzuri ambaye wakiweza kumpata atawasaidia, alisema mmoja wa makocha wa zamani wa Simba ambaye anatoka Uganda.

“Kiongozi (anamtaja), alinipigia akaniambia nitafute wasimamizi wa huyu mchezaji nilishawakutanisha, nimewaachia wao waendelee,” kilisema chanzo.

Hatua ya Simba kuanza kutafuta mshambuliaji mpya imetokana na ripoti ya awali ya kocha Barker ambaye haridhishwi sana na baadhi ya washambuliaji alionao kwenye kikosi hicho. T

Taarifa kutoka Simba zinaeleza Barker anavuta pumzi kwa mshambuliaji mmoja akiwemo Seleman Mwalimu, akitaka kuangalia ubora wake zaidi lakini amepata wasiwasi juu ya ubora wa washambuliaji wengine.

Barker pia anakubali takwimu za Jonathan Sowah lakini akitaka kujaribu kumtengeneza kuona kama anaweza kuwa na utulivu wa kucheza ndani ya eneo la hatari na sio kuwa na mikimbio mbali na hapo.

Mbali na mshambuliaji Simba pia inatafuta beki wa kati mwenye ubora ambaye hesabu zao ni kwamba aje kucheza sambamba na Rushine De Reuck ambaye ubora wake umewakosha makocha na viongozi.

Simba inapiga hesabu za kumuongezea mkataba Rushine ili aendelee kusalia ndani ya kikosi hicho, ambapo sasa inataka kumuongeza kuwa nahodha msaidizi ili kumshawishi akubali kusaini mkataba mpya.