Zanzibar kutumia tafiti kupunguza vifo vya mama na mtoto

Unguja. Wakati Zanzibar ikiendelea kuboresha miundombinu ya afya kwa kujenga hospitali na vituo vya afya mijini na vijijini, bado vifo vitokanavyo na uzazi ni tatizo linaloendelea kusumbua.

Hivyo, Wizara ya Afya Zanzibar imesema ina mpango maalumu wa kufanya tafiti zenye lengo la kupunguza vifo hivyo.

Mpango huo unafanywa kati ya Wizara ya Afya Zanzibar na kituo cha Utafiti cha Chinese Medical Development na Nanjing University of Chinese Medicine ya China.

Mpango huo unalenga kujikita zaidi juu ya uimarishaji wa tafiti zitakazosaidia kupata virutubisho mbalimbali ambavyo vitatumika kwa mama wajawazito ili kupunguza sababu kuu za vifo ikiwemo upungufu wa damu na lishe ya watoto wakati wanapozaliwa. 

Akizungumza na Mwananchi leo Jumanne Januari 14, 2026 Mkurugenzi Mkuu wa Wizara hiyo, Dk Amour Suleiman Mohamed amesema bado  Zanzibar inakabiliwa na changamoto ya vifo vitokanavyo na uzazi licha ya Serikali kuchukua jitihada mbalimbali kuhakikisha inapunguza vifo hivyo.

Kwa mujibu wa takwimu za mwaka 2023/24 vifo 134 kati ya vizazi hai 100,000 vimetokana uzazi, licha ya juhudi za  Serikali kupunguza vifo hivyo.

“Vifo vitokanavyo na uzazi vimekuwa tatizo kubwa katika vituo vya afya, wizara inafanya juhudi ili kuendana na malengo ya Shirika la Umoja wa Mataifa (UN) kuwa ifikapo 2030 vipungue kufikia 70 kwa kila vizazi hai 100,000 na watoto 12 kwa kila vizazi hai 1,000,” amesema Dk Amour. 

Amesema, wizara hiyo imejipanga kufikia malengo ya kukabiliana na vifo vya mama na mtoto kwa kuandaa mikakati ikiwemo kuongeza idadi ya wafanyakazi katika hospitali na vituo vya afya.

Naye, Mkurugenzi Kinga na Elimu Wizara hiyo, Dk Salim Slim amesema sababu mojawapo ya vifo hivyo ni tatizo la lishe duni kwa mama wajawazito na watoto.

Ameeleza, tatizo hilo husababisha upungufu wa damu kwa wajawazito kwa kiasi kikubwa na kuchangia vifo vya akina mama na watoto wakati wa kujifungua.

“Mama mjamzito anapokosa lishe na upungufu wa damu husababisha hatari wakati wa kujifungua kwa kukosa damu,” amesema Slim.

Amesema, lishe bora haihitaji gharama kama wananchi wanavyodhani badala yake ni vyakula vya kawaida ambavyo vinapatikana bila ya gharama.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Dk Mngereza Mzee Miraji amesema kuwa tatizo la lishe kwa watoto chini ya umri wa miaka mitano bado lipo hivyo na utafiti huo utakuwa suluhisho la changamoto hizo.

Amesema, kila mmoja ana wajibu wa kutoa mchango wa kuimarisha huduma za afya ya mama na mtoto kwa lengo la kuondokana na vifo vitokanavyo na uzazi.

Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Afya Zanzibar (Zahri), Dk Mayasa Salum Ali amesema lengo la ushirikiano huo ni kutafiti dawa ambazo zina msingi wa tiba na virutubisho ili kutumika kwa mama na mtoto.

Mwakilishi kutoka kituo cha Chinese Medicine Development, Dk Feng Guangqing amesema wataendeleza ushirikiano ulipo baina yao ukiwa na lengo la kuimarisha huduma za afya.