Uganda yazifungia asasi 10 za kiraia kuelekea uchaguzi mkuu

Uganda. Serikali ya Uganda imeyafungia mashirika yasiyo ya kiserikali 10, huku ikieleza sababu za kuchukua hatua hiyo.

Uamuzi wa kusitisha kwa muda usiojulikana shughuli za baadhi ya mashirika yasiyo ya kiserikali (NGOs) nchini humo, umefanyika ikiwa ni siku moja kabla ya kufanyika uchaguzi mkuu kesho Alhamisi Januari 15, 2026.

Ofisi ya Kitaifa ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali ya Uganda (National Bureau for NGOs) imetangaza jana Jumanne, Januari 13, 2026 kwamba takriban mashirika 10 yatafungwa kwa muda ili kuruhusu uchunguzi kuhusu shughuli zao.

Mtandao wa Nation Africa umeripoti kuwa, ofisi hiyo imesema imepokea taarifa za kijasusi zinazoonyesha kuwa baadhi ya mashirika hayo yalihusika katika shughuli zinazokiuka au kuhatarisha sheria za Uganda.

Hivyo imeamuru yasitishe shughuli zake kwa muda usiojulikana. Ingawa haikutoa maelezo ya zaidi na kwamba uchunguzi utaamua hatima ya mashirika hayo.

Hata hivyo, aina ya mashirika yaliyolengwa na agizo hilo umeibua shaka kuwa huenda uamuzi huo unahusiana na uchaguzi.

Mashirika yaliyosimamishwa yanahusisha yale ya haki za binadamu, vyombo vya habari na ufuatiliaji wa uchaguzi, ambayo yalikuwa yamerekodi matukio ya ukatili wa polisi dhidi ya waandishi wa habari na pia kuanzisha mifumo ya kufuatilia uwazi wa hatua ya upigaji kura.

Mashirika hayo ni pamoja na jukwaa la kitaifa la mashirika ya kiraia (National NGO Forum), Chapter Four Uganda, Alliance for Election Finance Monitoring (ACFIM), Human Rights Network for Journalists–Uganda (HRNJ-U), na National Coalition of Human Rights Defenders in Uganda (NCHRD-U).

Kila shirika limepokea barua ikieleza madai ya ukiukwaji wa sheria yaliyodaiwa kuufanya. Inadaiwa kuwa National NGO Forum ilikiuka sheria za ndani zinazohusu mashirika yasiyo ya kiserikali, tuhuma zinazofanana na zile zilizotolewa dhidi ya ACFIM na NCHRD-U.

Kwa upande wa Chapter Four, inadaiwa kujihusisha na shughuli zinazohatarisha usalama na sheria za Uganda. Katika barua kutoka kwa Dk Stephen Okello, ambaye ni Katibu wa Ofisi ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali, shirika hilo liliagizwa kusitisha shughuli zake kwa muda kutokana na uzito wa tuhuma zinazolikabili. Muda wa uchunguzi haukuainishwa.

Tuhuma kama hizo pia zilitolewa dhidi ya HRNJ-U, shirika ambalo limekuwa mstari wa mbele kuwatetea waandishi wa habari walioumia au kudhulumiwa na vyombo vya usalama wakati wa mikutano ya kampeni.

Watetezi wa haki za binadamu wameishutumu serikali kwa kuweka vikwazo ili kukwepa uwazi wa uchaguzi.

Pia jana Jumanne, Uganda  ilisitisha huduma za intaneti wakati wa uchaguzi, ikidai kuongezeka kwa taarifa upotoshaji na uchochezi wa vurugu.

 Awali, serikali ilikuwa imesema haitafunga intaneti, lakini ilibadilisha msimamo wake ikisema ushauri huo ulitolewa na vyombo vya usalama.

Naibu Mkurugenzi wa Human Rights Watch barani Afrika, Ashwanee Budoo-Scholtz  amesema kusitishwa kwa muda usiojulikana, kwa misingi isiyoeleweka wala kuthibitishwa, kwa mashirika ambayo kazi zao zinakuza haki za kiraia na kisiasa, ni ushahidi mwingine wa kudharau uhuru wa kujieleza.

“Serikali inapaswa kufuta mara moja maamuzi haya ya kusimamisha mashirika,” amesema.

Mwaka 2024, baadhi ya mashirika yasiyo ya kiserikali pia yalikuwa yamesimamishwa kwa tuhuma mbalimbali za ukiukwaji wa sheria. Agosti 2021, Ofisi hiyohiyo ilisimamisha Chapter Four pamoja na mashirika mengine 53 kwa kukiuka sheria za ndani, ikiwemo madai ya kutumia vibali vilivyokwisha muda wake na kushindwa kuwasilisha taarifa za shughuli zao.