Meatu. Zaidi ya asilimia 80 ya wanafunzi wa darasa la kwanza na kidato cha kwanza katika Shule ya Msingi Mwanhuzi, shule ya sekondari Mwanhuzi na Shule ya Sekondari Meatu, wilayani Meatu mkoani Simiyu, hawajaripoti shuleni licha ya kufunguliwa rasmi Januari 13, 2025.
Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Meatu, Dk Vicent Naano akizungumza Januari 14,2025 wakati wa ukaguzi alioufanya katika shule hizo, ambapo alieleza kusikitishwa na mwitikio mdogo wa wanafunzi.
Dk Naano amesema wazi kuwa uzembe wa wazazi ndiyo chanzo kikubwa cha tatizo hilo.
“Mzazi anayemzuia mtoto kwenda shule leo, anamnyang’anya maisha yake ya baadaye. Kumfanya mtoto kulima, kuchunga mifugo au kubaki nyumbani kwa visingizio visivyo na msingi ni kumuhukumu kuishi kwenye umaskini wa kudumu,” amesema.
Ameongeza kuwa elimu si hiari bali ni wajibu wa kisheria kwa mzazi na mlezi, akisisitiza kuwa Serikali haitaendelea kuvumilia tabia ya kuwanyima watoto haki yao ya msingi ya elimu.
Dk Naano ameonya kuwa endapo hadi Ijumaa, Januari 16, 2026, wanafunzi hao hawataripoti shuleni, hatua za kisheria zitaanza kuchukuliwa dhidi ya wazazi na walezi watakaobainika kushindwa kutekeleza wajibu wao kwa mujibu wa sheria za elimu nchini.
Sweya Jilala ni mkazi wa mjini Mwanhuzi, amesema kuwa matumizi ya watoto kama nguvu kazi bado ni changamoto kubwa.
Amesema kuwa baadhi ya wazazi wameweka kipaumbele kwenye kazi za nyumbani kuliko elimu.
“Mtoto anapochelewa kuanza shule, anaharibiwa mustakabali wake na wa jamii kwa ujumla,” amesema.
Kwa upande wake Rehema Kwilasa mkazi wa Mwanyahina wilayani humo amesema sheria za elimu zipo lakini bado zinahitaji usimamizi mkali.
“Bila kuwabana wazazi wazembe, hali hii itaendelea kujirudia kila mwaka,” amesema.
Naye Masanja Maduhu mkazi wa Mwanhuzi mjini amewataka viongozi wa vijiji na mitaa kuwa mstari wa mbele.
“Elimu si jambo la kuoneana aibu. Mtoto asiye shuleni leo ni tatizo la jamii kesho,” amesema.
