Mbeya. Wakati zaidi ya Sh100 bilioni zikitarajia kukusanywa kupitia mazao manne ya kimkakati wilayani Kyela mkoani Mbeya, wakulima wa mazao hayo wataondokana na changamoto ya soko kufuatia mikakati iliyowekwa na Chama Kikuu cha Ushirika wilayani humo (Kyecu).
Mazao hayo ni cocoa, ufuta, mbaazi na korosho ambayo yamejumuishwa kwenye mfumo wa stakabadhi ghalani ‘TMX’ ikiwa ni mpango mkakati wa kumnufaisha mkulima juu ya kilimo chake.
Akizungumza leo Januari 14,2026 Meneja Mkuu wa Kyecu, Aman Hankungwa amesema ili kufikia malengo hayo, wanaendelea kusimamia vyema uzalishaji bora wa mazao kuendana na uhitaji na ushindani wa soko ndani na nje.
Amesema kwa kipindi cha mwaka mmoja hadi Machi 31, 2027 wanatarajia kukusanya zaidi ya Sh100 bilioni, hali ambayo itazingatia masilahi ya mkulima kwa kuwahakikishia soko na bei yenye tija.
“Kwa zao la cocoa tunatarajia kuvuna kilo 9 milioni, ambapo kwa bei ya elekezi ya Sh10,000 tutavuna Sh90 bilioni, ufuta tunatarajia kuvuna tani 1,000 sawa na kilo 1 milioni, ambapo makusanyo yatakuwa Sh1.5 bilioni, korosho tani 300 kwa bei ya Sh1,800, sawa na Sh540 milioni”
“Kwa upande wa zao la mbaazi, tunatarajia kuvuna tani 300, ili kufikia malengo, tunataka uzalishaji uongezeke na wenye bora kulingana na uhitaji na ushindani wa soko la ndani na nje,” amesema Hankungwa.
Ameongeza kuwa mpango wa Kyecu ni kutoa miche bora 8,000 ya korosho Aprili mwaka huu, ambazo zimeandaliwa kwa ubora kupitia bodi ya korosho nchini, lakini kuondoa changamoto kwenye upatikanaji wa viuatilifu kwa mkulima.
Amefafanua kuwa mafanikio hayo yataendana na masilahi ya mkulima kwani kabla ya mazao hayo kuingizwa kwenye mfumo wa stakabadhi ghalani, bei haikuwa nzuri na wakulima hawakuwa na uhakika wa soko.
“Kwa maana hiyo wakulima wote watafikiwa na elimu juu ya kilimo bora chenye kuzingatia mahitaji ya mlaji na soko kwa ujumla, tumejipanga kuweka bei shindani kama ilivyo kwenye zao la cocoa, kwa kuwa tutakuwa na viwanda kwa ajili ya uchakataji” amesema.
Mkulima wa zao la ufuta, Benson Edson amesema bado changamoto kubwa ni gharama za uendeshaji wa zao hilo akiomba chama hicho na Serikali kuangalia uwezekano wa bei za mbolea.
“Tunatumia gharama kubwa kuandaa kilimo hiki, tunaomba bei ifanane na nguvu ileile anayotumia mkulima, tunaridhishwa na juhudi za uongozi wa Kyecu namna wanavyotupa matumaini,” amesema Edson.
Naye mkulima wa zao la mbaazi, Selina Mwansasu amesema hatua za Kyecu kuweka zao hilo kwenye mfumo wa TMX, inaenda kuwabadilishia maisha kwa kuwapa uhakika wa soko na bei kama yalivyo mazao mengine.
“Hata msimu uliopita kwa kuanzia tuliona nafuu, kimsingi juhudi ziendelee tuone tukiuza kwa bei ya juu ili kutusaidia sisi wakulima tunaotegemea zaidi kilimo hiki” amesema Selina.

