Ndugu wakacha miili miwili ajali ya basi na lori Morogoro

Morogoro. Zikiwa zimetimia siku 14 tangu kutokea kwa ajali ya basi na lori na kusababisha vifo vya watu 10 na majeruhi 23, miili miwili iliyohifadhiwa katika Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Morogoro mpaka sasa haijatambuliwa na hakuna ndugu aliyejitokeza kutaka kufanya utambuzi.

Akitoa taarifa hiyo Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Morogoro, Dk Joseph Kway amesema licha ya wataalamu kutoka ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali kuweka kambi hospitalini hapo tangu Desemba 31 ilipotokea ajali hiyo, lakini mpaka sasa hakuna ndugu aliyekwenda kuchukuliwa sampuli za vinasaba (DNA) kwa ajili ya kuitambua.

“Kwenye ajali hii watu 10 walifariki dunia na 23 walijeruhiwa, hapa hospitalini kwetu tulipokea miili tisa na mwili mmoja ulihifadhiwa katika kituo cha afya Mikese, miili tisa kati ya ile tuliyoipokea hapa ilikuwa imeungua kiasi cha kushindwa kutambulika kwa njia ya kawaida, hata hivyo miili minne ilitambuliwa kwa njia ya DNA na hii miwili mpaka leo hii Januari 14 haijatambuliwa na hakuna ndugu yeyote aliyejitokeza kufanyiwa DNA,” amesema Dk Kway.

Dk Kway amesema utaratibu wa kuhifadhi miili ya marehemu katika hospitali hiyo umewekwa ni siku 14 baada ya hapo halmashauri itachukua jukumu la kuizika.

“Utaratibu huu upo kwa zile maiti ambazo zimekufa katika mazingira ya kawaida, lakini kwa hizi maiti ambazo zimetokana na ajali kubwa ama majanga, Serikali huwa inatoa utaratibu na maelekezo hivyo kwa hii miili iliyokosa utambuzi tunasubiri maelekezo ya Serikali,” amesema Dk Kway.

Kuhusu majeruhi Dk Kway amesema aliyebaki hospitalini hapo ni mmoja ambaye tayari ameshafanyiwa upasuaji wa kwanza na kwa sasa anasubiri upasuaji wa pili ambao utafanyika Ijumaa ya Januari 16.

Amesema majeruhi huyo aliumia sehemu kubwa ya mwili na alihitaji uangalizi wa katibu na matibabu makubwa ya kibingwa, hata hivyo kwa sasa anaendelea vizuri na baada ya upasuaji wa pili ataruhusiwa kurudi nyumbani.

Awali Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Alex Mkama alisema ajali hiyo imetokea usiku wa Desemba 31 eneo la Maseyu barabara ya Morogoro -Dar es Salaam baada ya basi la abiria la kampuni ya Mawio lililokuwa likitoka Morogoro kwenda Tanga kugongana uso kwa uso na lori la mizigo kisha kuwaka moto.

Kwa mujibu wa Kamanda Mkama chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa dereva wa lori ambaye aliyapita magari ya mbele yake bila ya kuchukua tahadhari na hivyo kugongana na basi hilo.