Uwanja wa Gombani waipa jeuri ZFF

MAREKEBISHO yaliyofanyika kwenye Uwanja wa Gombani uliopo Pemba, yameipa jeuri Shirikisho la Mpira wa Miguu Zanzibar (ZFF) kutokana na sasa kuwa na viwanja viwili vyenye hadhi ya kimataifa baada ya New Amaan Complex unaopatikana Unguja.

Hayo ameyasema Ofisa Habari wa ZFF, Mohamed Kabwanga akibainisha kwamba, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) inayoongozwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Hussein Ali Mwinyi, inaendelea kufanya uwekezaji mkubwa katika sekta ya michezo kuelekea Fainali za Kombe la Mataifa Afrika (AFCON) 2027 itakayofanyika Tanzania kwa kushirikiana na Kenya na Uganda.

“Mwaka jana ilichezwa fainali ya Kombe la Mapinduzi hapa lakini ilikuwa katika mazingira ambayo uwanja haujakamilika, baada ya kumaliza fainali ile tukapisha ujenzi uendelee ndio maana hata Ligi Kuu ya Zanzibar haikuwa ikichezwa humu ndani.

“Ukiangalia paa imepigwa ya kisasa tofauti na ilivyokuwa mwaka jana, viti vimefungwa tena kwa utaratibu mwingine. Kati ya kiti kimoja na kingine kuna nafasi ambayo inakufanya ukikaa huchoki. Kuna tofauti kubwa sana na mwanzo.

“Niseme tu hongera kwa Dokta Mwinyi kwa kazi kubwa kupitia wakandarasi waliopewa hii tenda kufanya hapa, wamefanya kwa ukamilifu wake.

“Huu ni wetu sote, kama una timu yako inahitaji kuutumia uwanja huu ifuate utaratibu. CAF Champions League inachezwa hapa, hata CAF Confederation, hata michezo mingine, kuna AFCON inakuja.

“Ukarabati wa viwanja hivi unakuja kutokana na kwamba tuna jambo letu. Zanzibar tuna AFCON 2027 inakuja huku. Tuna Gombani, Amaan na kuna balaa lingine Fumba, huko ndio usiseme,” amesema Kabwanga.

Januari 8, 2025, Rais Mwinyi aliweka jiwe la msingi la ukarabati wa uwanja huo na viwanja vingine katika Wilaya ya Chake Chake, Mkoa wa Kusini Pemba ambapo Uwanja wa Gombani umefanyiwa ukarabati mkubwa, ikiwemo uwekaji wa paa jipya, ujenzi wa kuta, vyumba vya wachezaji, eneo la watu mashuhuri, maegesho, uwekaji wa minara ya taa, mifumo ya maji na umeme, pamoja na ujenzi wa uwanja wa mazoezi pembezoni.