Pwani. Mwanzilishi na Mkurugenzi wa Taasisi ya Flaviana Matata Foundation, Flaviana Matata amesema taasisi hiyo ina dhamira ya dhati ya kuhakikisha watoto wa kike wanapata mazingira salama na rafiki yatakayowawezesha kutimiza ndoto zao.
Hayo ameyasema leo Jumatano Januari 14, 2026 wakati uzinduzi na kukabidi mradi wa matundu 12 ya vyoo kwa wanafunzi wa kike, matundu mawili ya walimu, eneo la kunawia mikono, chumba maalumu kwa wanafunzi wenye mahitaji maalumu, chumba cha kujisitiri kwa wasichana, pamoja na eneo la kuchomea taka, hususan taulo za kike zilizotumika.
Amesema taasisi hiyo wameamua kujenga vyoo kuwaunga mkono walimu ili kuimarisha mazingira yote ya kujifunzia. Hivyo wanasaidia pande zote mbili jambo linalowakilisha heshima, ushirikiano, na dhamira ya pamoja katika elimu.
“Pia, tulijenga vyoo kwa ajili ya walimu kwa sababu tunapowaunga mkono walimu, tunaimarisha mazingira yote ya kujifunzia. Hivyo leo, kwa kweli tunasaidia pande zote mbili: wanafunzi na hii inawakilisha heshima, ushirikiano, na dhamira ya pamoja kwa elimu na heshima.” amesema.
Ameongeza kuwa, “Tunatambua kuwa changamoto za usafi wa mazingira, hususan ukosefu wa vyoo rafiki kwa wasichana, zimekuwa kikwazo kwa elimu yao. Mradi huu ni sehemu ya mchango wetu katika kuhakikisha hakuna mtoto wa kike anayekosa elimu kwa sababu ya mazingira duni.”
Taasisi ya Flaviana Matata imeendelea kuunga mkono jitihada za Serikali katika kuboresha sekta ya elimu na afya kwa kuzindua na kukabidhi rasmi mradi wa vyoo na huduma za maji safi na salama katika Shule ya Sekondari Kiwangwa.
Akizungumza kwa niamba ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge, Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Shaibu Ndemanga ametoa wito kwa wadau mbalimbali wa elimu wa ndani na nje ya nchi kujitokeza kushirikiana na Serikali kwa ajili kuendelea kuboresha maeneo mbalimbali katika sekta ya elimu.
Ndemanga amesema kuwa mradi huo ni mfano wa kuigwa wa ushirikiano kati ya Serikali na wadau wa maendeleo katika kuboresha elimu.
“Serikali inaendelea kuwakaribisha wadau kama Taasisi ya Flaviana Matata kushirikiana nasi katika kutatua changamoto za msingi shuleni. Amesema mradi huo utasaidia kuboresha mazingira ya kujifunzia, hasa kwa watoto wa kike,” amesema.
Waanzilishi wa Safar Global Foundation, Shabnam Safarzadeh na Shay Safarzadeh wamesema taasisi hiyo imefurahi kushirikiana na Taasisi ya Flaviana Matata katika mradi unaogusa moja kwa moja maisha ya watoto wa kike.
“Tunaamini uwekezaji katika afya, usafi wa mazingira na elimu ni uwekezaji wa moja kwa moja katika mustakabali wa jamii. Tutaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuleta mabadiliko chanya,” amesema Safarzadeh.
Hafla hiyo ya uzinduzi ilihudhuriwa pia na viongozi mbalimbali wa serikali, walimu, wazazi, wanafunzi pamoja na wadau wengine wa maendeleo.
Mradi huo unaotekelezwa kwenye Shule ya Sekondari ya Kiwanga mkoani Pwani chini ya Taasisi ya Flaviana Matata kwa ufadhili wa Safar Global Foundation unatarajiwa kuwanufaisha wanafunzi 930 kila mwaka.
