Dk Mwigulu atoa maelekezo kulinda kazi za wazawa

Dodoma. Waziri Mkuu Dk Mwigulu Nchemba amezitaka wizara zinazohusika na masuala ya ajira zisimamie kikamilifu utekelezaji wa sheria zinazotaka kazi zinazoweza kufanywa na Watanzania zisifanywe na wageni isipokuwa zile zinazohitaji utaalamu ambao nchi ina upungufu.

Vilevile, Dk Mwigulu amekemea tabia ya baadhi ya wenye nyumba kumpangisha raia mmoja wa kigeni na kumruhusu mpangaji huyo apangishe watu wengine ndani ya nyumba hiyo jambo ambalo ni hatari kwa usalama na pia halina tija kibiashara.

 Dk Mwigulu ametoa agizo hilo leo Jumatano, Januari 14, 2026 alipofungua kikao cha mawaziri, manaibu mawaziri, makatibu wakuu na manaibu makatibu wakuu wa wizara za k­­isekta kujadili fursa za ajira ndani na nje ya nchi.

Agizo hilo linalenga kuongeza fursa za ajira kwa Watanzania kufuatia kuwepo kwa wimbi kubwa la wageni kufanya kazi au biashara zinazoweza kufanywa na Watanzania na kuliwezesha Taifa kukabiliana na changamoto ya upungufu wa ajira.

 “…Kazi zinazoweza kufanywa na Watanzania ziachwe wafanye, si kuruhusu wageni wafanye.

Tusioneane aibu kama tumefungua milango au kulegeza wataalamu wafuatilie. Wageni wafanye kazi za kitaalamu ambazo nchi ina uhaba wa wataalamu.”

Amesema ni lazima wataalamu wa ndani wasimamie sheria ipasavyo na kama kuna maeneo yanayokwamisha wayabainishe na yafanyiwe marekebisho.

“Hatuwezi kuleta watu wanaokuja kufanya kazi ambazo Watanzania wanaziweza.”

Juni 6, 2025, aliyekuwa Waziri wa Viwanda na Biashara, Selemani Jafo alipokea taarifa ya Timu Maalumu ya Ukaguzi wa Biashara zinazomilikiwa na wageni. Katika Soko la Kariakoo, jijini Dar es Salaam.

Jafo ambaye ni mbunge wa Kisarawe alisema Serikali inaangalia uwezekano wa kupeleka hati ya dharura bungeni ili kuwezesha baadhi ya vifungu vya sheria vinavyolenga kulinda biashara za wazawa kuingizwa kwenye Muswada wa Sheria ya Fedha (Finance Bill) wa mwaka huu.

Desemba 2025, Waziri wa Viwanda na Biashara, Judith Kapinga akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam alisema wamezungumza na kampuni mbalimbali kuhakikisha wanatumia wazawa kwenye maeneo yanayopaswa kutumika ili kulinda biashara za wazawa.

Katika hatua nyingine, Dk Mwigulu ametoa wito kwa Watanzania kuwa na wivu na nchi yao kwa kutoruhusu baadhi ya vitu kufanyika, alitolea mfano suala la wenye nyumba kumpangisha raia moja wa kigeni ambaye naye analeta wenzake wengi katika nyumba hiyo hiyo.

“Watanzania tuwe na wivu na nchi yetu, mfano mtu anamkodishia nyumba mgeni kwa Dola 5,000 (za Marekani) kwa mwaka na kisha mgeni huyo anawaleta wenzake 60 na anawakodisha Dola 500 hapo Mtanzania anapata hasara, hii si sawa hata kwa usalama.”

Waziri Mkuu amewaagiza wahusika wafuatilie suala hilo la makazi ili wakae katika utaratibu rasmi.

Dk Mwigulu akizungumza leo Jumatano, Januari 14, 2026 alipofungua Kikao cha Mawaziri, Naibu Mawaziri, Makatibu Wakuu na Manaibu Makatibu Wakuu wa Wizara za Kisekta kujadili fursa za ajira ndani na nje ya nchi.

“Eneo hili liangaliwe wageni wanalundikana na kufanya kazi ambazo Watanzania wangeweza kufanya, hatuwezi kuruhusu hili tunataka wawekezaji.”

Hivyo, Waziri Mkuu ameziagiza wizara zinazohusika zifuatilie suala hilo, pamoja na kuwasisitiza wasimamie utekelezwaji wa sheria kwa sababu kila nchi ina sheria zake na Tanzania inatekeleza majukumu yake kwa kufuata sheria.

 Amesema sheria zimetungwa ili kusaidia kujenga kampuni za Watanzania na kuzikuza, hivyo wizara zinazohusika zihakikishe hazisajili kampuni za kigeni kabla ya kuzifanyia uchunguzi wa kina kwa sababu baadhi ya taarifa zinazowasilishwa si sahihi.