Wizara moto kwa mawaziri kudumu mrefu

Dar es Salaam. Katika miongo miwili iliyopita, uteuzi na mabadiliko kwenye Baraza la Mawaziri nchini vimeibua taswira mbili tofauti; wizara ambazo mawaziri wake hubadilika mara kwa mara kana kwamba ni bandika badua, na nyingine zenye uthabiti ambapo mawaziri hukaa kwa muda mrefu.

Mwelekeo huo umeendelea kujitokeza hata katika awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan, ukifungua mjadala mpana na maswali iwapo mabadiliko hayo ni mkakati wa kuongeza ufanisi wa serikali au dalili ya changamoto za kimfumo ndani ya baadhi ya wizara.

Rais Samia, alipowaapisha mawaziri baada ya kuunda baraza lake jipya Novemba 2025, aliweka wazi hatasita na ataendelea kufanya mabadiliko ya mara kwa mara kwa watakaoshindwa kusimamia vyema wizara zao.

Ahadi hiyo ilitimia ndani ya siku 52 hadi Januari 8, 2026, alipofanya mabadiliko ya kwanza katika baraza lake la muhula wa pili.

Miongoni mwa wizara ambazo ambazo zimekuwa kama ‘bandika bandua’ ni Mambo ya Ndani, Maliasili na Utalii, Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Tamisemi, Ulinzi pamoja na Viwanda na Biashara.

Mbali na rekodi za wizara hizo, historia ya Serikali ya Tanzania inaonyesha nafasi ya waziri mkuu ndiyo inayoshikilia rekodi kwa wateule kudumu muda mrefu zaidi madarakani huku Wizara ya Mambo ya Ndani ikiongoza kwa mawaziri kukaa kipindi kifupi zaidi.

Mabadiliko hayo ya mara kwa mara, yanatajwa kuendana na haiba ya mtu, mahitaja ya wizara anayoteuliwa kuongoza na matarajio ya anayewateua, kwa mujibu wa Denis Konga, mhadhiri wa Chuo cha Diplomasia.

 Konga amesema utashi wa mteuaji na mwelekeo wa Serikali kwa wakati husika ndiyo vigezo ambavyo huamua aina ya mtu anayeweza kufaa kuongoza wizara au idara fulani.

“Kuna mambo mengi lakini namna mtu anavyokuwa katika kuishi kwake na watu na mwenendo wake kwa ujumla, vinaweza kuwa na mchango katika uongozi. Hata hivyo, utashi wa kisiasa wa wakati huo ndio unaoamua kuhusu aina gani ya mtu anaweza kutosha kwenye wizara fulani,” amesema.

Akitoa mifano, amesema Wizara ya Mambo ya Ndani ni wizara nyeti, lazima iwe na waziri anayeweza kushuka chini na kuzungumza na watu kwa mahitaji yao ili kujenga imani na jamii, pia ni wizara inayogusa maeneo nyeti yakiwemo Jeshi la Polisi ambalo ni rahisi kulaumiwa na jamii.

“Waziri wa Mambo ya Nje huyu lazima awe mtu mwenye ushawishi, anayeweza kuzungumza na vyombo vya habari kwa lugha nzuri akashawishi mataifa ya nje, akajenga uhusiano mzuri wa nchi na jumuiya za kimataifa, hayo ndiyo ninayoona ya msingi,” amesema.

Amesema japo haya ndiyo mambo ya msingi ya kuangalia, kwa kiasi kikubwa jamii ilishatoka huko, badala yake viongozi wengi kwa sasa huteuliwa kutokana na mwelekeo wa mtawala wa wakati husika.

“Kwa hiyo kikubwa hapo ni utashi wa kisiasa na maono ya anayewateua kwa kuwa ndiye anaamua mtu wa namna gani atafaa kuwa kwenye wizara gani,” amesema.

Kwa upande wake Hamduny Marcel, mchambuzi wa siasa na utawala anasema ingawa suala la uteuzi linategemea uamuzi wa utashi binafsi wa Rais, mabadiliko ya muda mfupi ni ishara ya uwepo wa tatizo.

“Uamuzi wa kuteua au kutengua uteuzi ni mamlaka ya anayeteua, lakini mabadiliko ya muda mfupi yanaashiria kuna tatizo la kiutendaji,” anasema.

Kwa kipindi cha miaka 20 iliyopita, Wizara ya Mambo ya Ndani imeongoza kwa kuwa na mawaziri wengi waliopokezana ama kwa kutenguliwa au kuhamishwa ndani ya miaka miwili.

Ndani ya kipindi hicho, wizara hii imepitia mawaziri wengi kuliko wizara zote, wengi wao wakikaa kwa muda usiozidi miaka miwili.

Baada ya John Chiligati aliyekuwa waziri 2006, aliingia Joseph Mungai (2006–2008), kisha Lawrence Masha (2008–2010) na Shamsi Vuai Nahodha (2010–2012).

Mwaka 2012 wizara ilikabidhiwa kwa Dk Emmanuel Nchimbi (2012–2013), Mathias Chikawe (2014–2015), Charles Kitwanga (2015–2016), Dk Mwigulu Nchemba (2016–2018) na baadaye Kangi Lugola (2018–2020).

Baadaye kijiti kikashikwa na George Simbachawene (2020–2022), Hamad Masauni (2022–2024), Innocent Bashungwa Novemba 2024 hadi Novemba 2025, kabla ya George Simbachawene aliyeongoza kwa mara ya pili na kumpisha Patrobas Katambi.

 “Wizara ya Mambo ya Ndani ni wizara inayosimamia polisi, magereza, uhamiaji na usalama wa ndani wa nchi, katika miaka yote hiyo, mabadiliko ya mara kwa mara yameifanya iwe yenye rekodi ya juu ya mzunguko wa mawaziri kutokana na unyeti wa majukumu yake,” anasema Fulgence Massawe, kaimu Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC).

Mbali na wizara hiyo, Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki katika kipindi cha miaka mitano ya karibuni, imekabiliwa na mabadiliko ya haraka ya mawaziri.

Katika mabadiliko hayo, kuanzia Machi 2019 hadi Januari 2026 wameshapita mawaziri sita, akianza Profesa Palamagamba Kabudi (2019 – 2021), Balozi Liberata Mulamula (2021  hadi 2022), Dk Stergomena Tax aliyeongoza 2022 hadi 2023.

Baadaye kijiti kilichukuliwa na January Makamba aliyeshika 2023 hadi 2024 kabla ya Balozi Mahmoud Thabit Kombo aliyeteuliwa kuanzia Julai 2024 hadi sasa, na kuifanya wizara hiyo kuwa miongoni mwa zenye mabadiliko kila baada ya muda mfupi.

Wizara nyingine ni Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa kambayo awali mawaziri walikuwa wanakaa muda mrefu, lakini kwa miaka karibuni wanabadilika kila mara.

Aliyekaa muda mrefu ni Dk Hussein Mwinyi ambaye sasa ni Rais wa Zanzibar, aliyeiongoza kwa vipindi viwili kuanzia 2008 hadi 2012 na tena kuanzia 2014 hadi 2020, akitimiza jumla ya takribani miaka 10. Baada yake, Elias Kwandikwa alikaa kuanzia 2020 hadi 2021 (alipofariki dunia), kabla ya wizara hiyo kuongozwa na Stergomena Tax kuanzia 2021 hadi 2022.

Aidha, Innocent Bashungwa alichukua nafasi hiyo kuanzia 2022 hadi 2023, kabla ya Stergomena Tax kurejea kuanzia 2023 hadi 2025 alipoteuliwa Rhimo Nyansaho anayeiongoza sasa.

Wizara nyingine ni Maliasili na Utalii ambayo kuanzia 2006 hadi sasa ni 11 ikianza na Profesa Jumanne Maghembe (2006 – 2008), Shamsa Mwangunga (2008 – 2010) na Ezekiel Maige Waziri (2010 – 2012).

Wengine ni Khamis Kagasheki (2012 – 2013), Lazaro Nyalandu (2014 – 2015), Profesa Jumanne Maghembe (2015 –2017), Hamisi Kigwangalla (2017 – 2020),  Dk Damas Ndumbaro (2020 – 2022),  Pindi Chana (2022 – 2023) kisha Angellah Kairuki, Mohamed Mchengerwa na  Ashatu Kijaji wa sasa.

Wizara nyingine iliyoshuhudia mabadiliko ya mara kwa mara ni Tawala za Mikoa na Serikali na Mitaa (Tamisemi) ambayo tangu 2006 hadi leo imeongozwa na mawaziri 12.

Kuanzia mwaka 2005 hadi 2008 ilikuwa Chini ya Mizengo Pinda aliyempisha Steven Wasira (Februari 2008 – Mei 2008), Celina Kombani (2008-2010), George Mkuchika (2010-2012) na Hawa Ghasia (2012-2015) na George Simbachawene aliyehudumu kuanzia 2015 hadi 2017.

Waliofuata ni Suleiman Jafo, Ummy Mwalimu, George Simbachawene, Innocent Bashungwa,  Angella Kairuki, Mohammed Mchengerwa na  Profesa Riziki Shemdoe anayeiongoza wizara hiyo.

Wizara ya Viwanda na Biashara nayo imekuwa na mabadiliko ya kila mara.

Wizara ya Viwanda na Biashara nayo imekuwa na mabadiliko ya kila mara. Baada ya Nazir Karamagi (2006–2007) aliingia Basil Mramba (2007–2008) na Mary Nagu (2008–2010) kisha Cyril Chami (2010–2012), Abdallah Kigoda (2012- 2015) na Charles Mwijage (2015 2018) aliyempisha Joseph Kakunda (2018– 2019).

Pia walipita Innocent Bashungwa (2019- 2020), Geoffrey Mwambe (2020–2021), Kitila Mkumbo (2021– 2022), Ashatu Kijaji na sasa Judith Kapinga.

Tofauti na rekodi za mabadiliko ya muda mfupi, Wizara ya Fedha imeonyesha uthabiti kwa mawaziri wake kukaa kwa muda mrefu zaidi kuliko wizara zingine nyingi ikiwa ikiwa imeongozwa na mawaziri wawili tu kipindi cha miaka 10.

Baada ya Zakhia Megji, Mustafa Mkulo  na William Mgimwa, kuanzia Novemba 2015 hadi Machi 2021 wizara hiyo iliongozwa na Dk Philip Mpango hadi alipokabidhi mikoba hiyo kwa Dk Nchemba kuanzia Machi 2021 hadi Novemba 2025, kabla ya uteuzi wake kuwa Waziri Mkuu.

Kuanzia Novemba 2025 hadi sasa wizara hiyo inaongozwa na Balozi Khamis Mussa Omar.

Wizara nyingine ambayo imekuwa ikiguswa kila mara ni Wizara ya Nishati na Madini, hata hivyo baada ya kugawanywa mwaka 2017, wizara mbili za Nishati na ile ya Madini zimekuwa na mabadiliko ya wastani ikilinganishwa na wizara nyingine.

Wizara ya Nishati kwa upande wake, imeongozwa na Medard Kalemani na Dk Doto Biteko kwa kipindi cha zaidi ya miaka mitano iliyopita hadi Novemba 2025, Deogratius Ndejembi alipoteuliwa kuiongoza hadi sasa.