TANZANIA NA INDONESIA KUIMARISHA USHIRIKIANO WA MAENDELEO KATIKA KILIMO NA NISHATI

Na. Joseph Mahumi na Saidina Msangi, WF, Dodoma.

Tanzania na Indonesia zimekubaliana kuendeleza zaidi ushirikiano wa kimaendeleo katika sekta mbalimbali za kiuchumi na kijamii ikiwemo kilimo na nishati kwa faida ya nchi hizo mbili.

Hayo yamebainishwa jijini Dodoma, baada ya Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omary (Mb), kukutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Indonesia nchini Tanzania, Mhe. Tri Yogo Jatmiko Avetisyan.

Akizungumza katika kikao hicho, Mhe. Balozi Omar, ameishukuru Serikali ya Indonesia kwa mchango wake mkubwa katika kusaidia sekta mbalimbali za uchumi wa Tanzania ikiwemo sekta za madini, kilimo na mifugo tangu kuanzishwa kwa uhusiano wa kidiplomasia mwaka 1964.

“Mwaka huu ni maadhimisho ya miaka 62 tangu kuanzishwa kwa uhusiano wa kidiplomasia kati ya Tanzania na Indonesia, na uhusiano wetu umeendelea kuimarika zaidi kadiri miaka inavyosonga mbele, na pia tumeona ziara kati ya viongozi wetu Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alipotembelea Indonesia, na Mhe. Prabowo Subianto Rais wa Indonesia alipokuja Tanzania, hii ni ishara ya uhusiano thabiti unaojengwa juu ya heshima na ushirikiano wa kweli,” alisema Mhe. Balozi Omar.

Aidha, Mhe. Balozi Omar alisema kuwa, dhamira ya Indonesia katika kukuza maendeleo endelevu na kupunguza umasikini imechangia kubadilisha kwa kiasi kikubwa maendeleo ya kijamii na kiuchumi nchini Tanzania kupitia misaada ya kifedha, ushauri wa kitaalamu, na programu za kujenga uwezo.

Aidha Mhe. Balozi Omary aliwaalika wawekezaji kutoka Indonesia kuja kuwekeza nchini katika sekta mbalimbali za kiuchumi na kijamii ikiwemo kilimo, uongezaji thamani wa mazao, madini, viwanda, nishati, miundombinu, afya, elimu na utalii.

Kwa upande wake, Balozi wa Indonesia nchini Tanzania, Mhe. Tri Yogo Jatmiko Avetisyan, alisema kuwa katika kuhakikisha kuwa nchi hizo zinadumisha ushirikiano zaidi ya Watanzania 170 wamepata manufaa kupitia programu hizo za kujenga uwezo katika sekta mbalimbali ikiwemo kilimo, mifugo, nishati, madini, uvuvi na fedha.

“Tutahakikisha tunaimarisha zaidi uhusiano huu kwa kuongeza kuwajengea uwezo wataalmu wa Tanzania ili maeneo yote tuliyokubaliana kushirikiana yanaleta tija na ustawi mpana wa uhusiano wa nchi hizi mbili,” alisema Mhe. Balozi Avetisyan.

Kikao hicho kilihudhuriwa pia na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Bi. Amina Khamis Shaaban, Naibu Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango, Dkt. Blandina Kilama, Kamishna wa Idara ya Fedha za Nje Wizara ya Fedha, Bw. Rished Bade, Kamishna Msaidizi Idara ya Usimamizi wa Deni la Serikali, Bi. Tiba Kisonga na maafisa wengine waandamizi kutoka Wizara ya Fedha na ubalozi wa Indonesia nchini.

Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), akimkabidhi Balozi wa Indonesia nchini Tanzania, Mhe. Balozi Tri Yogo Jatmiko Avetisyan, zawadi iliyokuwa na bidhaa zinazozalishwa nchini Tanzania ikiwemo korosho na kahawa, baada kikao walipokutana na kufanya mazungumzo, katika ukumbi wa mikutano wa Waziri wa Fedha, Treasury Square, jijini Dodoma.

Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), akisalimiana na Balozi wa Indonesia nchini Tanzania, Mhe. Balozi Tri Yogo Jatmiko Avetisyan, walipokutana na kufanya mazungumzo, katika ukumbi wa mikutano wa Waziri wa Fedha, Treasury Square, jijini Dodoma.

Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), akizungumza wakati wa kikao na Balozi wa Indonesia nchini Tanzania, Mhe. Balozi Tri Yogo Jatmiko Avetisyan, alipofika kwa ajili ya mazungumzo, katika ukumbi wa mikutano wa Waziri wa Fedha, Treasury Square, jijini Dodoma.

Waziri wa Fedha wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), akiongoza kikao cha mazungumzo na Balozi wa Indonesia nchini Tanzania, Mhe. Balozi Tri Yogo Jatmiko Avetisyan, ambaye alifika kwa ajili ya mazungumzo, katika ukumbi wa mikutano wa Waziri wa Fedha, Treasury Square, jijini Dodoma.

Balozi wa Indonesia nchini Tanzania, Mhe. Balozi Tri Yogo Jatmiko Avetisyan, akizungumza katika kikao na Waziri wa Fedha Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), walipokutana na kufanya mazungumzo, katika ukumbi wa mikutano wa Waziri wa Fedha, Treasury Square, jijini Dodoma.

Waziri wa Fedha wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb) (wa nne kulia), na Balozi wa Indonesia nchini Tanzania, Mhe. Balozi Tri Yogo Jatmiko Avetisyan (wa tano kulia), wakiwa katika picha ya pamoja na Viongozi na Wataalamu kutoka Wizara ya Fedha, Tume ya Mipango na Ubalozi wa Indonesia, baada ya kikao cha mazungumzo kilichofanyika katika ukumbi wa Waziri wa Fedha, Treasury Square, jijini Dodoma. Kutoka kushoto Kamishna Msaidizi Idara ya Usimamizi wa Deni la Serikali, Bi. Tiba Kisonga, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Bi. Amina Khamis Shaaban na Kamishna wa Idara ya Fedha za Nje Wizara ya Fedha, Bw. Rished Bade. Kutoka kulia ni Katibu wa Balozi wa Indonesia Bw. Antidius Karoli Kalisa, Mkuu wa Idara ya Utamaduni, siasa na Mambo ya Kijamii Bw. Michael Bastian Supit na Naibu Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango, Dkt. Blandina Kilama,

(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, WF, Dodoma)