Dar es Salaam. Upelelezi wa kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili mfanyabiashara, Fabian Mazali (56) umekamilika.
Wakili wa Serikali Roida Mwakamele ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, leo Jumatano Januari 14, 2025 wakati kesi hiyo ilipotajwa.
Mazali anakabiliwa na mashtaka 21 yakiwemo ya kutakatisha fedha, kutengeneza ripoti au hati ya tathimini ya uongo ya viwanja na kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu zaidi ya Sh2 bilioni.
Mwakamele ametoa taarifa hiyo, mbele ya Hakimu Mkazi Kuu, Ushindi Swallo.
“Kesi imeitwa kwa ajili ya kutajwa na upelelezi wake umekamilika, hivyo tupo katika hatua za kuwasilisha nyaraka na taarifa muhimu Mahakama Kuu kwa ajili ya kuzisajili,” amedai Mwakamele.
Amedai kutokana na hali hiyo, aliomba mahakama iwapangie tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa na kuangalia kama nyaraka hizo zimeshasajiliwa.
Hakimu Swallo amekubaliana na ombi la Jamhuri na kuahirisha kesi hiyo hadi Januari 27, 2026.
Mshtakiwa amerudishwa rumande kutokana na mashtaka ya kutakatisha fedha yanayomkabili, hayana dhamana kwa mujibu wa sheria.
Katika shtaka la kwanza, Mazali anadaiwa tarehe isiyojulikana kati ya Januari 2023 katika mkoa wa Dar es Salaam, akiwa na nia ya kudanganya, alitengeneza hati ya uongo ambayo ni ripoti ya tathmini ikionyesha thamani ya nyumba ya makazi iliyopo katika Kiwanja Na. 1, Kitalu V, eneo la Buyuni Nyamaronda ni Sh634milioni, wakati akijua kuwa taarifa hiyo si ya kweli.
Katika shtaka la pili hadi la saba inadaiwa tarehe isiyojulika kati ya Aprili 2023 hadi Novemba 28, 2024 mshtakiwa alitengeneza hati ya uongo ya ripoti ya tathmini kuonyesha thamani ya nyumba iliyopo Bunju ina thamani ya Sh719 milioni, nyumba iliyopo Buyuni inathamani ya Sh813 milioni na nyumba iliyopo Kigamboni ina thamani ya Sh883 milioni, wakati akijua kuwa ni uongo.
Shtaka la nane na la tisa, mshtakiwa akiwa na nia ovu, alitengeneza hati ya uongo iitwayo taarifa ya kina ya Msajili wa Kkampuni ikionyesha ni mmoja wa wakurugenzi wa kampuni ya Natgroup Limited pamoja na mmiliki wa hisa 3,500 katika kampuni hiyo wakati akijua kuwa taarifa hiyo si ya kweli.
Katika shtaka la 10 hadi ya 15, Mazali anadaiwa kati ya Juni 19, 2023 jijini Dar es Salaam kwa makusudi na kwa udanganyifu, alipata dhamana ya mkopo wa usambazaji wa mafuta kutoka Kampuni ya First Assurance Company kwa niaba ya United Group Limited yenye thamani ya Sh 2.3bilioni kwa kutumia nyaraka za uongo.
Shtaka la 16, Septemba 30, 2023 mshitakiwa alipokea Sh2.3 bilioni, wakati akijua fedha hizo ni zao la kosa la awali la kupata mkopo kwa njia ya udanganyifu.
Shtaka la 17 ni la kutakatisha fedha ambapo, mshtakiwa anadaiwa Novemba 7,2023 alipokea Sh461 milioni, huku akijua kuwa fedha hizo ni zao la kosa la kupata mkopo kwa njia ya udanganyifu.
Mshtakiwa huyo anadaiwa Julai 19, 2023, alitakatisha Sh461 na shtaka la 19, anadaiwa kutakatisha Sh10 milioni kutoka kwenye akaunti ya kampuni ya Natgroup kwenda kwa Godson Simanga, huku akijua kuwa fedha hizo ni zao la kosa tangulizi la kupata mkopo kwa njia ya udanganyifu.
Shtaka la 20, Mazali anadaiwa Agosti 3, 2023 ndani ya Jiji la Dar es salaam, alijifanya kuwa yeye ni Mkurugenzi wa kampuni ya Natgroup na alihamisha kiasi cha Sh50milioni kutoka akaunti ya kampuni ya Natgroup kwenda kwa Veronica Ringo huku akijua fedha hizo ni mazalia ya kosa ya tangulizi la kujipatia mkopo kwa njia ya udanganyifu.
Mahakama iliendelea kuelezwa kuwa Septemba 26, 2023 ndani ya Jiji la Dar es Salaam, mshtakiwa akijifanya kuwa yeye ni Mkurugenzi wa kampuni ya Natgroup Limited na kuhamisha Sh246 milioni kutoka akaunti ya kampuni hiyo kwenda kwenye akaunti yake yenye jina la Fabian Mazali huku akijua kuwa fedha hizo ni zao la kupata mkopo kwa njia ya udanganyifu.
Kwa mara ya kwanza, Mazali alisomewa kesi hiyo ambayo haina dhamana, Desemba 30, 2025.