Mwili wa dereva bodaboda wakutwa juu ya kaburi Tabora

Tabora. Mwili wa Hamisi Nchambi maarufu Ngosha ambaye ni dereva bodaboda umekutwa juu ya kaburi katika makaburi ya Miemba, kata ya Malolo, Manispaa ya Tabora.

Inadaiwa watu hao wasiojulikana wametelekeza mwili wa kijana huyo ambapo  pikipiki yake haikukutwa eneo la tukio.

Akizungumzia tukio hilo leo Jumatano, Januari 14, 2026, Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Costantine Mbogambi amesema Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi wa matukio hayo huku likiwasaka usiku na mchana wote wanaohusika na matukio hayo na kuwatia nguvuni.

“Tunaendelea kuwasaka watu hawa  na watatiwa nguvuni ili sheria  ichukue mkondo wake kwa sababu kila mmoja ana haki ya kuishi,” amesema Mbogambi.

Tukio hilo ni la pili la aina hiyohiyo kutokea ndani ya Januari hii ambapo la kwanza  lilitokea kata ya Tumbi wiki moja iliyopita.

Shuhuda  wa tukio hilo, Rashidi Mrisho amesema alipigiwa simu na mama yake kuwa kijana huyo amefariki makaburini lakini mikono yake imefungwa kwa nyuma na pikipiki haipo.

Mwili wa kijana Hamisi ukiwa juu ya kaburi ukiwa umefungwa miguu na mikono na watu wasiojulikana.

Amesema bodaboda huyo ni kijana mwaminifu na ndio wakati wote  amekuwa akiagizwa kubeba abiria na bidhaa muhimu za nyumbani,  na kazi zote hizo amekuwa akizifanya kwa uaminifu.

“Kwa leo hatujui cha kusema kwa sababu tumekuwa tukisikia tu kwamba kuna mtu kauawa, tulikuwa tukishituka lakini tunachukulia tu ile kawaida lakini leo ameuawa huyu mtu wetu kabisa tumeumia sana,” amesema Mrisho.

Hamisi Saidi jirani wa marehemu Hamisi, amesema wamepokea taarifa kuwa Ngosha amefariki dunia kwa kuuawa jambo ambalo limewashangaza kwa sababu anafahamika sio mtu mkorofi

. “Sasa labda hiyo pikipiki mpya ndio sababu.”

“Tunahisia tu kwamba labda ameuawa kwa sababu ya hiyo pikipiki kwa kuwa ni mpya, maana kwa uzoefu wetu ukiona bodaboda ameuawa na pikipiki imechukuliwa ujue ni mpya tu, inaumiza sana kutoa uhai wa mtu kwa sababu ya kitu kinachoweza kununulika,” amesema.

Kaimu kamanda wa polisi mkoa wa Tabora Costantine Mbogambi akitoa taarifa ya matukio ya mauaji ya boda boda.

Aidha Katibu wa bodaboda mkoani humo, Dotto Mwamtuya amelaani tukio hilo huku akiiomba Serikali kuangalia kwa karibu matukio kama hayo kwani kazi ya bodaboda ni moja ya ajira za vijana hivyo yakiwa yanatokea matukio kama hayo wataogopa kufanya kazi.

“Vijana wamejiajiri kupitia kazi hii na wanapata kipato, wanaendesha familia zao lakini sasa wataanza kuogopa ikiwa hali ndiyo hii, maana yule wa Tumbi alifungwa hivihivi kama huyu na akauawa sasa Serikali kwa kweli ituangalie,” amesema.