Mwanariadha wa kimataifa wa Tanzania na Jeshi la Polisi, Transfora Mussa Ngimbudzi ameondoka nchini leo kwenda Uholanzi kushiriki mashindano ya Montferland Run Half Marathon yatakayofanyika Januari 18, 2026, ikiwa ni mbio yake ya kwanza mwaka huu.
Mashindano hayo yanamkuta Transfora akirejea kwenye jukwaa la kimataifa baada ya msimu uliopita uliogubikwa na changamoto za majeraha yaliyomzuia kushiriki kikamilifu mashindano kadhaa ya nje ya nchi.
Februari mwaka jana, majeraha yalimzuia kushiriki mbio za Valencia nchini Hispania kabla ya kurejea Aprili kushika nafasi ya tatu mbio za kilomita 10 za Lille, nmUfaransa, akitumia dakika 31:53 na kurudia muda wake bora wa kilomita 10.
Baada ya kurejea aliendelea kuonyesha ushindani mzuri kwa kushika nafasi ya pili mbio za Africa Day 10km kabla ya kushinda NBC Dodoma Marathon kilomita 10 mwezi Agosti, akiimarisha hadhi yake kama mmoja wa wanariadha bora wa kike nchini.
Baada ya mafanikio, alipata tena majeraha wakati wa mazoezi, hali ambayo ilimfanya kushiriki kwa shida mashindano ya majeshi ambako hakufanya vizuri.
Nyota huyo alipumzika kujitibu kabla ya kurejea mazoezini Novemba, ambapo Desemba 2025 alihitimisha kwa kumaliza nafasi ya pili mbio za kimomita 21 za Stop GBV, akitumia saa 1 na dakika 13.
Akizungumza akiwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA), kabla ya kuondoka, Transfora amesema maandalizi yamekamilika na anakwenda Uholanzi akiwa na mkakati wa kushindana na kushinda.
“Maandalizi yamekuwa mazuri. Nimejiandaa kimwili na kisaikolojia. Nimeweka mkakati wa mbio hizi na lengo langu ni kupambana hadi mwisho na kushinda”, amesema Transfora.
Amewaomba Watanzania kumwombea afanye vizuri huku akiwaahidi kupambana kupeperusha vyema bendera ya nchi kimataifa.
